Tamu, Chungu za Makonda wa Kike Mabasi ya Abiria

 

Tamu, Chungu za Makonda wa Kike Mabasi ya Abiria

Safari yangu inaanza saa 11 alfajiri ya Julai 18 mwaka huu, kutoka nyumbani Tabata kuelekea Shekilango jijini Dar es Salaam katika kituo kidogo cha mabasi yanayokwenda mikoani.


Nikiwa nje ya gari ninalopanda namuona binti akifungua buti la gari na kuweka mizigo. Namsogelea na kumuuliza kama ni mhusika, ananijibu; "Mimi ni kondakta wa gari hili, wewe unashukia wapi? kama mwisho nitakupeleka upande wa pili kama njiani leta begi lako hapa."


Namjibu sina mzigo, nakaa pembeni nikimuangalia anavyofanya kazi kwa kuwa ni mazoea kwa wanaume kufanya shughuli hii.


Baada ya dakika 20 anakuja kijana wa kiume kumsaidia. Wanapomaliza kupakia mizigo binti anakabidhiwa karatasi. Nafuatilia kujua ni ya nini, nabaini ni orodha ya majina ya abiria.


Sawa na abiria wengine, naingia ndani ya gari kukaa kwenye kiti changu. Saa 12:15 asubuhi safari inaanza kutoka Shekilango kuelekea Kituo cha Mabasi cha Magufuli kilichopo Mbezi Luis.


Hakuna msongamano Barabara ya Morogoro, tunatumia dakika chache kufika kituoni kupakia abiria wengine na kama ilivyokuwa awali, binti anashuka kupakia mizigo. Saa moja asubuhi gari linaondoka, tunaendelea na safari.


Tunapofika Kibamba Shule, binti anasimama mlangoni, anawatangazia walio nje; “Kuna yeyote anayekwenda Dodoma.”


Hakuna anayekuja kupanda, hivyo safari inaendelea. Tunapofika Mto Ruvu, binti anachukua kipaza sauti, anatusalimia na kutukaribisha. Anajitambulisha jina lake (kwa kulitaja) na dereva ni John.


Anatupa maelekezo kuhusu safari, vituo tutakavyosimama na cha mwisho kitakuwa Dodoma. Anatuhimiza kufunga mkanda kwa ajili ya usalama wetu, pia anatuomba kila mmoja kusali kwa imani yake.


Navuta subira, kisha namuita. Namuomba tuzungumze kuhusu kazi yake ya ukondakta. Anakuwa mgumu kukubali ombi langu, ananieleza anaweza kufukuzwa kazi kwa kuzungumzia mambo kuhusu kampuni yake.


Namshirikisha dereva John kuhusu lengo langu, naye kwa kutumia ishara anamruhusu kuzungumza. Hata hivyo, ananipa sharti, hatapenda jina lake liandikwe gazetini, hivyo tunakubaliana nitamwita Janeth (si jina halisi). Ananieleza tukifika sehemu ambazo hazitakuwa na pilikapilika za abiria tutazungumza.


Tunapofika Dumila mkoani Morogoro, anapata wasaa wa kuzungumza nami, ananiita tunakaa jirani na dereva John na kuanza mazungumzo.


Kondakta Janeth


Ananiambia ana miaka 22 na ana Shahada ya Sheria na Biashara aliyotunukiwa na chuo kimoja nchini India. Tangu amerudi nchini ni miezi sita na anashinwa kuomba kazi aliyosomea kwa kusubiri vyeti vyake vihakikiwe na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).


Wakati anasubiri uhakiki, ananiambia hakuona sababu ya kukaa nyumbani, hivyo alianza kusaka vibarua.


Ananisimulia kuna siku alikutana na rafiki wa dada yake akamwambia kuna kazi ya ukondakta akimwambia ina faida.


Hata hivyo, ananieleza kupata kazi ya ukondakta si rahisi, kwa kuwa kuna changamoto nyingi na hasa unapokuwa huna mtu wa kukusaidia. Anasema wapo wanaotoa rushwa ya ngono ili kuajiriwa.


Kwake ilikuwaje? Ananieleza alipeleka maombi kwa kampuni aliyoelekezwa na rafiki wa dada yake ambaye ni kondakta mzoefu.


Kutokana na kushikwa mkono, ananiambia haikuchukua muda mrefu aliitwa kwa ajili ya usaili.


"Nilikwenda kwenye usaili, nikaambiwa nimepata kazi. Nilitakiwa kuanza mafunzo ya nadharia ambayo yalidumu kwa siku tatu kisha nilipelekwa mafunzo ya vitendo ndani ya gari. Nilifanya vizuri nikakabidhiwa gari na kuanza kazi rasmi pasipo kuwa na msimamizi," ananiambia.


Janeth ananieleza licha ya kupata kazi, hakuna mkataba zaidi ya kulipwa fedha za kujikimu. “Nilishachoka kukaa nyumbani, sikufikiri mara mbili, nilikubali kuanza kazi Machi mwaka huu.”


Tunapofanya mazungumzo ananiambia ana mwezi wa tatu kazini. Kwa safari fupi ananiambia hulipwa posho ya Sh20,000 na Sh30,000 kwa safari ndefu.


Janeth ananieleza kampuni imewapangia chumba (geto) kwenye mikoa ambayo hawana makazi ya kudumu, ambacho hukaa wafanyakazi wote watakaokuwa safarini mkoani humo.


Kwa wasiopenda kuchangia malazi ya pamoja, ananiambia wanaruhusiwa kulala nyumba za wageni.


"Sipendi kuchangia chumba, tumelelewa katika mazingira tofauti, hivyo wapo wanaolala geto na wengine lodge (nyumba ya wageni) muhimu unatakiwa kufika kazini mapema kupakia mizigo ya abiria," anasema.


Ananieleza akiwa jijini Dar es Salaam hulala nyumbani kwao Mbezi Luis. Asubuhi hupanda pikipiki hadi Shekilango linakoegeshwa gari.


Janeth ananiambia tangu alipoanza kazi hiyo hajawahi kupata mapumziko kutokana na uchache wa makondakta wanawake katika kampuni yao.


Hali hiyo anasema inamsababishia mgogoro wa mara kwa mara na mpenzi wake ambaye hakupenda afanye kazi hiyo, akihofu kwamba atasalitiwa.


"Huwa navumilia na kuendelea na kazi kwa kuwa pia nisipokwenda napoteza kipato cha siku. La muhimu ni kwamba, namshirikisha dereva ninapohisi sipo vizuri kwa sababu ikitokea nimepumzika nitakuwa nimejifukuzisha kazi," anasema.


Saa 8.30 mchana tunafika kituo cha mabasi Nanenane mkoani Dodoma. Hapa wanashuka baadhi ya abiria. Janeth anaendelea na kazi akitueleza kituo cha mwisho cha safari ni katikati ya Jiji la Dodoma.


Ni mwendo wa dakika 15 tu, hivyo saa 8.45 mchana tunafika mwisho wa safari. Anashusha mizigo akisaidiana na kijana mmoja.


Namuuliza Janeth, unaelekea wapi baada ya hapa. Ananiambia, “Naingia ofisini kukabidhi nyaraka, nikitoka nitakwenda na dereva gereji kuhakikisha kila kitu kipo sawa ndipo nitakwenda hotelini kupumzika ili kuendelea na safari kesho.”


“Siwezi kwenda kulala kwenye chumba tulichopangiwa kutokana na mazingira. Kama unahitaji kufahamu tulikopangiwa utachukua bodaboda atakupeleka. Wewe sema walipopangiwa makondakta wa gari hili (analitaja) unapelekwa,” ananiambia.


Nachukua pikipiki namwelekeza dereva kwa kadiri ya maelekezo ya Janeth. Ninapofika nyumbani hakuna mtu.


Ninapouliza niliowakuta naelezwa wahusika ninaowatafuta huingia hapo saa tatu usiku kutokana na mazingira ya kazi zao.


Harakati za Zainab


Katika mazungumzo yetu, napata habari ya kondakta mwingine, Zainab Aboubakar, anayesafiri kati ya Dodoma- Mwanza- Tarime -Bariadi na Bukoba.


Naamka alfajiri naelekea eneo la Mnada Mpya jijini Dodoma, naanza safari ya kwenda Mwanza nikishuhudia utendaji kazi wa Zainab, mkazi wa Mwanza mzaliwa wa Babati mwenye elimu ya Diploma ya Uuguzi.


Tukiwa ndani ya basi, ananiambia ameanza kazi Mei, 2022, baada ya kumaliza chuo na kukaa muda mrefu nyumbani akisubiri ajira.


Ananiambia ukondakta ni kazi pekee anayoitegemea kwa sasa ili kufikia malengo aliyojiwekea, hivyo anaifanya kwa weledi.


Zainab mama wa mtoto mmoja ananieleza kabla ya kuanza kazi hiyo, alikuwa gereji ambako alikuwa akifua vitambaa vinavyofunika viti vya magari kwa ujira wa Sh5,000.


Ananiambia kuna mtu alimshika mkono na kumuingiza katika ukondakta akieleza; “Kuna dada alikuwa kondakta katika kampuni nilikofanya kazi awali. Aliomba kwa msimamizi nikakubaliwa.”


Hata hivyo, kuna jambo lilitokea kama anavyonieleza; “Nilipoanza kazi akaona wote aliokuwa nao karibu wamemtenga. Ili asipoteze kazi au kipato akanipeleka sehemu nyingine akaniambia unatakiwa kujiongeza ili kuwa na kipato zaidi.”


Ananiambia; “Nilimwamini kwa kila aliloniambia kwa kuwa yeye ni mwenyeji katika kazi hii. Akaanza kunitafutia wanaume akiniambia usipochangamka itakula kwako, huku akinitafutia kampuni nyingine akidai kwa ajili ya masilahi. Kumbe alikuwa akinichafua nionekane nina matatizo hivyo siwezi kudumu kwenye ajira.”


Anasimulia wakiwa katika mizunguko aliambiwa na bosi wake hawezi kuendelea na kazi kwa kuwa anaichafua kampuni kwa kuwa na tabia mbaya, hivyo kuondolewa kazini mara kwa mara.


Zainab ananiambia alishangazwa na maelezo hayo, hivyo alirudi nyumbani kwake Mafinga mkoani Iringa alikokuwa akiishi kwa wakati huo.


Ananieleza alishawahi kufukuzwa kazi siku tatu baada ya kuajiriwa, lakini alipata kampuni nyingine iliyomlipa posho Sh15,000.


Kutokana na posho hiyo na mgawo kidogo kutokana na abiria wanaopakia njiani pamoja na vifurushi, anasema alianza kujiwekea akiba.


Zainab akijiita mpambanaji ananiambia alihamia Dodoma anakoendelea na kazi ya ukondakta katika kampuni inayomlipa posho ya safari ya Sh40,000.


Ananieleza changamoto inayomkabili ni kutokuwa na mkataba wa ajira, hivyo hufanya kazi kwa shaka kwa kuwa muda wowote unaweza kufukuzwa.


“Kwa kukosa mikataba wakati wowote unaweza kufukuza kazi na bosi. Wakati mwingine hata dereva akisema simtaki kondakta fulani basi kazi huna,” ananieleza.


Hapa ananisimulia kisa nilichoshuhudia asubuhi. “Utakuwa shuhuda wakati unasubiri usafiri uliona naondoka lakini gari likasimamishwa nikashushwa. Niliambiwa safari yangu imeishia pale. Kwa kweli niliamini kazi yangu imeisha lakini nilihamishiwa basi hili.”


Ananieleza posho wanayolipwa ni ndogo kwa kuwa wanapaswa kulipa kodi kwenye vyumba walivyopanga.


"Kampuni inatupa posho kidogo kwa madai kuwa wamepanga nyumba kwa ajili ya kupumzika wafanyakazi hili si sawa kwa kuwa inamnyima uhuru mfanyakazi kutokana na kuchangia chumba,” ananiambia.


Kazi hii ananiambia haina likizo, ukiitaka na kazi hauna, pia haina mapumziko kwa wale wenye safari za kila siku.


Ananieleza endapo ikitokea ajali barabarani hakuna wanacholipwa kupitia mifuko ya jamii kwa kuwa hawana mkataba, pia bima za afya.


"Mtu unaumwa inakubidi unywe dawa za maumivu ili kuendelea na safari. Ukiwahi kufika unaomba kijana akusaidie halafu unakwenda hospitali," ananieleza.


Katika kazi ya ukondakta ananiambia hakuna usawa wa kijinsia kwa kuwa dereva anaheshimika zaidi na linapotokea tatizo ndani ya gari kondakta ndiye anaonekana mzembe.


Nahitimisha mazungumzo na Zainab ninaposhuka kituo cha Nata mkoani Mwanza saa 12.30 jioni.


Miadi na Jackline


Asubuhi na mapema naamka naanza safari ya kwenda Dar es Salaam. Baada ya siku moja, naanza nyingine ya kwenda Arusha nikiwa na kondakta Jackline ambaye tulishaweka miadi awali.


Jackline mkazi wa Arusha ananiambia ana elimu ya Shahada ya Usimamizi wa Kumbukumbu. Ananisimulia rushwa ya ngono kwa makondakta wanawake inaonekana jambo la kawaida na wakati mwingine mabinti hutumika kwa kazi hiyo ili kuvutia wateja.


Ananiambia baadhi ya wasimamizi wa mabasi hutafuta mabinti wenye mvuto kutoka vijijini na kuwapa kazi ya ukondakta, huku wakijua lengo lao ni kuvutia biashara.


“Wanaletwa mabinti kutoka vijijini waliomaliza kidato cha nne wanafundishwa kazi. Wakiwa katika majaribio hurubuniwa na kujikuta wakijihusisha kimapenzi na dereva au kondakta,” ananieleza.


Jackline anaeleza makondakta wa kiume wamekuwa kikwazo katika utendaji kazi wao, kwani wanapokataliwa kimapenzi huwanyima posho itokanayo na fedha inayokusanywa njiani.


"Hawa ndugu zetu wakati mwingine wanatupa mitihani, utakuta dereva anakomalia penzi unajizungusha kumnyima mwisho wa siku unaona anakuletea kisirani kwenye kazi na kukunyima mgawo wa njiani," anasema.


Chanzo cha safari


Kondakta Zena Zubeir, mkazi wa Tanga ndiye chanzo cha mimi kufanya safari kuangalia changamoto wanazozipitia.


Zena mwenye elimu ya Shahada ya masuala ya benki tulikutana jijini Dar es Salaam na katika mazungumzo alinieleza mapito anayopitia ikiwa ni pamoja na kutukanwa na abiria, huku utu wake ukitwezwa kwa kufanya kazi ya ukondakta.


Ananiambia wazazi wake walitarajia angekuwa na kazi nzuri baada ya kumaliza chuo, hivyo kuacha kuwategemea lakini ameishia kulipwa posho ya Sh10,000 kwa safari.


Zena ananiambia gari lao baada ya safari huegeshwa ama Kigamboni au Chanika ambako hana ndugu, hivyo hulazimika kulipia chumba na anapokosa fedha hulala ndani ya gari.


"Posho Sh10,000 ulipe chumba na kula haitoshi, hivyo ukubali kulala kwenye gari au kwenda na dereva atakapolala. Mara nyingi tunategemea kupata fedha kutokana na abiria wanaopanda njiani au kusafirisha vifurushi. Kusipokuwa na abiria wengi unaweza kukaa siku nne pasipo kusafiri," ananieleza Zena.


Ananiambia kuna wakati hutamani kuacha kazi lakini swali analojiuliza; “Nitapata wapi kazi nyingine?"


Zena anasema anapoitazama familia yake kwamba inamtegemea inabidi aendelee kukomaa na kazi.


Wasemavyo madereva


Dereva John Ezekiel, ananieleza kazi ya ukondakta kwa wanawake ni ngumu, hukutana na vishawishi vingi, vinavyohitaji ujasiri kuvikabili.


"Unakuta binti analipwa posho ndogo ya Sh10,000, ili kujikimu anakubali kulala na dereva au vijana atakaokutana nao mwisho wa safari. Siyo kampuni zote zinafanya safari kila siku, nyingine zinasubiri kupata abiria," anasema.


Kwa mujibu wa Ezekiel, wangekuwa na mkataba na kulipwa kila mwezi kama ilivyo kwa baadhi ya madereva, hata rushwa ya ngono ingepungua.


Ananieleza mkataba ungewezesha mtu kuajiriwa kulingana na elimu yake, kupata kipato stahiki na wasigefukuzwa kazi kiholela.


"Waajiri wengi wa mabasi wanakwepa gharama, hawataki kutoa mkataba kwa kufahamu mahitaji muhimu ikiwemo bima ya afya na mfuko wa jamii. Kama huna mkataba kufukuzwa ni dadika tu na hakuna kuuliza," ananieleza na kuongeza;


"Tunasafiri na mabinti hawa, wakati mwingine abiria wa njiani hatuwapakii hadi mwisho ili kusaidia kuongeza kipato kwa mtu anayelipwa posho ya Sh10,000 unategemea anaishi vipi kama si kuanza ‘kudanga’. Asilimia kubwa ya makondakta wanawake wamesoma elimu nzuri, ni kutokana na uhaba wa ajira wamejikuta huku."


Dereva, Hussein Ally ananiambi kuna kampuni zimeamua kuwa na makondakta wanawake ili kuvutia wateja. Pia wanaaminika si wezi na wana kauli nzuri kwa abiria.


Ananiambia, "Unakuta kakosewa lakini anamuomba msamaha abiria ili tu aendelee kulinda kibarua chake. Wamesoma lakini wanadhalilishwa na abiria. Waajiri na hata wasimamizi wao wakikosea wanawasema mbele za watu kitu ambacho si kizuri."


Kwa upande wake, dereva Joseph Shio anaona baadhi yao hawajui ni kwa nini wanafanya kazi hiyo, lakini wanaojitambua wapo makini na wana nidhamu kazini.


Ananiambia wapo matajiri wanaowatumia mabinti hao kingono, hivyo kuwatengenezea mazingira ya kuwa na jeuri kwa madereva, hivyo kushindwa kufanya kazi pamoja.


Shio ananieleza kuna makondakta wanaume wanaowachezea mabinti hao kutokana na kipato chao kuwa kidogo.


“Hatujuani afya zetu na mabinti wanakutana na watu tofauti. Wakijiheshimu wanakuwa salama kwa sababu wanaume huwa tunajaribu tukiona unaelekea tunamalizana," anasema Shio.


Ananiambia mabinti hao pia wapo wanaorubuniwa na abiria wenye kipato wakiwaahidi kuwapatia ajira kwenye kampuni zao.


Wasimamizi wa mabasi


Meneja msaidizi wa kampuni ya mabasi ya Tilisho ya jijini Arusha, Loveness Japhet ananieleza wana makondakta wanawake katika magari yao na wanaheshimu misingi ya sheria na utaratibu wa kazi.


Ananiambia wao hutoa mishahara kila mwezi na bonasi kwa wafanyakazi bora, pia huwapa mapumziko na likizo ya uzazi kwa kuwa ni haki yao.


Loveness ananiambia kampuni yao inazingatia usawa wa kijinsia na hakuna aliye juu zaidi ya mwingine. Inapotokea tatizo la kinidhamu, mhusika husimamishwa kazi ili kutumikia adhabu na ikitokea akarudia huondolewa kazini.


“Kuna wafanyakazi wetu wamefunga ndoa na wamekutana kwenye kazi mwanamke akiwa kondakta na mwanamume dereva. Ikitokea tukaona kazi hazifanyiki vizuri na tukigundua tatizo ni ndoa tunamruhusu aende kutumikia ndoa kwanza, ikiwa sawa anaweza kurudi kazini,” ananieleza.


Kwa upande wake, Abbas Mohamed, msimamizi wa magari yanayotoa huduma Kanda ya Kati na Kanda ya Ziwa, ananiambia wanajua changamoto zinazowakabili makondakta wanawake na kwamba,


wanajitahidi kuboresha posho zao.


"Kuna dereva anafanya kazi huu mwaka wa tatu hana mkataba ukisema tuanze kuoneana huruma kutokana na jinsia inakuwa ngumu, hizi kazi zinahitaji uvumilivu. Ni muhimu kupambania malengo yao waweze kutoboa," anasema Mohamed.


Mtazamo wa wazazi


Mkazi wa Dar es Salaam, Joseph John ananiambia hakubaliani na mwanawe Janeth kufanya kazi ya ukondakta.


Ananieleza elimu yake haiendani na kazi anayoifanya, licha ya gharama kubwa waliyotumia kumsomesha.


"Mzazi yeyote matumaini yake ni kuona matunda ya alikowekeza fedha zake, hususani katika kupata kazi nzuri kulingana na elimu aliyopata. Leo hii binti yangu kaangukia katika ukondakta naumia sana.


"Nilimwambia sijapenda kazi hii, akaniambia baba nitakaa nyumbani hadi lini wakati sina kazi na nimeshaomba sehemu nyingi wanahitaji uzoefu wa miaka mitano, hivyo kaamua kupambana huko," ananieleza John.


Anasema hofu ya familia katika kazi ya ukondakta ni mtazamo wa jamii, kuiona kuwa inafanywa na watu waliokata tamaa ya maisha. Pia, ajali za barabarani kwani endapo ikitokea amejeruhiwa kampuni haina cha kumlipa kwa kuwa si mwajiriwa.


Naye Juma Kingole, mkazi wa Babati ananiambia kazi ya ukondakta kwa watoto wa kike ni kudhalilisha familia kutokana na kujinyima kwao kusomesha watoto na matokeo yake wanakosa kazi walizosomea.


"Nimepambana kuhakikisha mwanangu anasoma na kuipa heshima familia, mwishowe anafanya kazi ya kuzurura kwenye magari kwa kuwa kondakta. Japokuwa anatuma anachokipata lakini si malengo yetu yeye kuwa kondakta," ananieleza Kingole, mlezi wa Jackline.


Kwa upande wake, Agness Zephania, mkazi wa Mwanza anayemuombea mwanawe afikie malengo yake, ananiambia hana pingamizi kwake kufanya kazi hiyo kwa kuwa anaishi maisha mazuri na anaweza kulea mjukuu.


Ananieleza mwanawe alipopata mimba alirudi Mwanza hadi alipojifungua. Mtoto alipofikisha mwaka mmoja alimuachia na kwenda kutafuta kazi aliyosomea jijini Dodoma, lakini hakufanikiwa na kuamua kuwa kondakta.


"Mwanangu ni kila kitu kwetu, ametujengea nyumba ya kuishi, anasomesha wadogo zake na analea mtoto wake kutokana na kazi ya ukondakta. Anakuja kutusalimia anapopangiwa safari ya kuja huku, ninachomwambia kila siku kazi anayofanya ni ngumu, muhimu kujitunza na kuwa makini na maradhi," ananieleza Agness, mzazi wa Zainab.


Maoni ya wadau


Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga anasema rushwa ya ngono imekuwa tatizo kubwa katika taasisi mbalimbali na kutokana na uhaba wa ajira baadhi hukubali kuutoa utu wao.


Anasema wasichana wanaolalamika hawajatambua haki zao na wapi waende kupata msaada.


"Tulipofanya uchunguzi wa sehemu ambayo wafanyakazi wanalipwa fedha kidogo tulibaini ni katika sekta ya usafirishaji, iwe madereva na makondakta pia,” ananieleza.


Anashauri kuwe na chama cha makondakta wanawake ili iwe rahisi kushughulikia changamoto zinazowakabili. Chama hicho hakipo kwa sasa.


Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Usawa wa Kijinsia Tanzania (Sukita), Msafiri Mwajuma, anasema wamiliki wa mabasi watambue kazi ya ukondakta haina jinsia, hivyo mwanamke ana haki ya kuifanya.


“Hakuna ajira iliyoandikwa hii ni ya mwanamume na hii ya mwanamke, sema sisi wenyewe kwa maono yetu ndiyo tuliotofautisha. Mfumo dume ni adui wa maisha ya mwanadamu, hivyo si vizuri kwa msichana anapoomba kazi ya ukondakta kumlaghai ili kutumia kipawa chake.


“Rushwa ya ngono ni kosa kama yalivyo makosa mengine, mwanamke ana haki ya kutafuta ujira kwa kujiajiri au kuajiriwa na hata kumiliki mali,” anasema.


Shirika la Kazi Duniani


Mratibu wa Ukimwi, Usalama na Afya kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO), Gretrude Sima, anashauri makondakta wanawake kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kupata jukwaa la kusemea matatizo yao na kupata haki.


“Sheria imetoa uhuru wa vyama na haki ya kujumuika. Mtu hatakiwi kuachishwa kazi kwa sababu anajumuika kwenye vyama vya wafanyakazi,” anasema.


Ananieleza ni wajibu wa mwajiri kumpa mkataba mwajiriwa ili kupata mahitaji muhimu, yakiwamo bima ya afya na mifuko ya jamii.


“Katika mkataba anatakiwa aorodheshe vitu vya msingi ambavyo mfanyakazi anapaswa kupewa endapo ikitokea changamoto itakuwa rahisi kujulikana,” anasema.


Sima ananiambia ni haki ya mfanyakazi kwenda likizo baada ya kufanya kazi kwa miezi sita na kwamba, kuna baadhi ya kampuni hutengeneza utaratibu wake kuepuka likizo.


USULI


Ofisa Kazi Mfawidhi Mkoa wa Dar es Salaam, Vaileth Ndeza anasema kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, mwajiri anatakiwa kutoa mkataba wa ajira.


Anasema sheria imetaja iwe ni mtumishi wa serikalini, mashirika ya umma, sekta binafsi na kazi zisizo rasmi inatakiwa kila mfanyakazi apewe mkataba.


Ndeza anasema endapo mwajiri atakiuka utaratibu, anatakiwa kufikishwa mahakamani na sheria kuchukua mkondo wake.


"Kama naanza kazi leo natakiwa kuwa na mkataba wa maandishi ili kufahamu kile ninachokwenda kukifanyia kazi,” anasema.


Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini kifungu cha 14 kinaeleza mikataba ya maneno inaruhusiwa ijapokuwa mfanyakazi ni lazima apewe taarifa ya maelezo ya maandishi.


Hata hivyo, haishauriwi kuingia mkataba wa maneno wa ajira kwa sababu itakapotokea suala la utaratibu wa kisheria jukumu la kuthibitisha au kukanusha sharti la ajira linalodaiwa litakuwa ni la mwajiri.


Kama mwajiri atashindwa kutoa mkataba wa ajira au taarifa ya maelezo ya maandishi basi atashindwa kuthibitisha sharti lolote lililotajwa na mgogoro unaweza kuamuliwa dhidi yake.


Hivyo ni muhimu kumpatia mfanyakazi mkataba wa maandishi au angalau taarifa ya maelezo ya maandishi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad