The Cask Bar yafungwa Mwanza "Hana leseni miaka miwili, halipi kodi"



Serikali wilayani Ilemela mkoani Mwanza imeifunga bar maarufu ya The Cask Bar & Grill jijini Mwanza kwa tuhuma za ukwepaji kodi kwa kipindi cha miaka miwili.


Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela, Kiomono Kibamba, amesema uongozi wa bar hiyo umekwepa kodi ya Serikali na kuendesha biashara zaidi ya moja eneo hilo hilo.


Akizungumza katika eneo hilo la Bar Mkurugenzi wa Ilemela, Kiomoni Kibamba amesema mmiliki wake amekiuka masharti ya uendeshaji wa biashara ikiwemo kukosa leseni ya biashara kwa kipindi cha miaka miwili.


"Tumeona ni busara kuanzia kesho afunge biashara zake mpaka hapo aatakapotatua changamoto za ukiukwaji wa masharti ya leseni za biashara.


"Kuna biashara anafanya ya matangazo ambayo ni marufuku kuchanganya biashara tofauti na leseni uliyopewa. Hana leseni ya biashara ya vileo kwa miaka miwili mfululizo, kuna shida nyingine za mapato ambazo pia tumezibaini.


"Tumeona leo (jana) kuna vitu vimeshapikwa, kwa hiyo sio busara kufunga leo lakini kuanzia kesho afunge mpaka atakapotatua. Hapa ana biashara mbili, mgahawa na vileo zote hana leseni kwa miaka miwili, kwa hiyo watu wanakunywa tu hapa lakini hakuna leseni. Mapato ni zaidi ya Tsh milioni 10 au 15 ambazo zimepotea.


"Tunapenda wafanyabiashara wafanye biashara wakue, lakini wafanye kulingana na masharti ya leseni, wao wapate na Serikali ipate. Niwasihi wafanyabiashara wote wa Ilemela kufanya biashara zao kwa kufuata sheria,” amesema Kibamba.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad