Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Mbarali na madiwani katika kata sita za Tanzania Bara, na uchaguzi utafanyika Septemba 19, 2023.
Mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhani Kailima amesema NEC ilipokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhusu uwepo wa nafasi wazi ya Ubunge katika Jimbo la Mbarali, kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Francis Mtega.
Kailima amesema wagombea watachukua fomu kuanzia tarehe 13 hadi 19 Agosti, 2023, siku ya uteuzi itakuwa tarehe 19 Agosti, 2023 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 20 Agosti, 2023 hadi tarehe 18 Septemba, 2023.
Amezitaja kata zitakazofanya uchaguzi mdogo kuwa ni Nala iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, mkoani Dodoma, Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza, Old Moshi Magharibi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na Marangu Kitowo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, Mtyangimbole iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na Mfaranyaki iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.