Na. George Rugambwa – Butainamwa, Kagera.
Tumsifu Yesu Kristo. Amani na Usalama.
Nataka niwape tafakari ndogo ya sehemu ya Kanisa Katoliki katika amani na ustawi wa jamii yetu na ninaomba nitumie mfano wa jirani zetu Rwanda mwaka 1994. Idadi ya Wakatoliki ilikuwa 65%, Waprotestanti 9%, Waislamu 1%. Dini nyingine na wasio na dini wanagawana hiyo 25% inayobaki.
Kama tunavyojua Rwanda ina makabila makubwa mawili, Wahutu na Watusi. Maaskofu akiwemo aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kigali Vincent Nsengiyumva, wakawa nyuma ya siasa za kibaguzi kwa miaka 14.
Askofu Nsengiyumva akawa Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya National Republican Movement for Democracy and Development (NRMDD) au Kiswahili Vuguvugu la Jamhuri la Demokrasia na Maendeleo.
Hiki kilikuwa ndicho chama tawala chini ya Wahutu kuanzia mwaka 1975 hadi mwaka 1994 pale Kagame na Rwandan Patriotic Front (RPF) walipoitwaa Kigali baada ya watu zaidi ya laki nane wengi wao Watusi kupoteza maisha katika mauaji ya Kimbari.
Ukabila ulitumika kupandikiza woga au chuki dhidi ya wengine, jambo ambalo mara nyingi husababisha migogoro na vita, kama ilivyokuwa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka wa 1994. Picha ya John Isaac/ UN.
Mwaka 1990 Vatican ilimuonya Askofu Nsengiyumva kuachana na siasa lakini hakutii ipasavyo. Sijui kama mnaelewa. Huyu alikuwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Kigali Rwanda na wakati huo huo Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Chama Tawala na Kiongozi wa Maaskofu wote wa Katoliki Rwanda.
Chama chake cha Wahutu kilishiriki kupanga mauaji ya Watusi. Chini ya uongozi wake maaskofu Rwanda waliishi kwenye majumba ya kifahari yakijengwa kwa misamaha ya kodi kwenye huduma na biashara za kanisa.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Rwanda, nchi ndogo yenye uchumi mkubwa wa kilimo, ilikuwa na msongamano mkubwa wa watu barani Afrika. lakini baadaye mwaka 1992 hali ikawa ni tofauti. Picha ya History.com.
Juni 7, 1994, kikosi kidogo cha Wanajeshi wa Kagame wa RPF walimvamia na kumuua yeye na maaskofu wengine wawili na mapadri kumi na kusema wanahusika kwenye mauaji ya ndugu zao. Askofu Nsengiyumva alikuwa na marafiki maaskofu, mapadri na watawa Tanzania na amefika hapa mara nyingi hadi miaka miwili kabla ya kifo chake.
Wakristo wenzangu, nachotaka kusema ni kwamba viongozi wetu wa dini ni binadamu wenye ajenda zao. Uzuri baadhi ya mambo yao mnayajua pia. Akili za kuambiwa changanya na za kwako.
Nawatakia Ibada Njema ya Jumapili Agosti 20 2023.