Waandishi washambuliwa kwa mikuki, mishale Ngorongoro

Waandishi washambuliwa kwa mikuki, mishale Ngorongoro


Ngorongoro. Zaidi ya vijana 200 wanaodhaniwa ni wa jamii ya Kimasai (morani), wa eneo la Enduleni, Wilaya ya Ngorongoro, Mkoani Arusha jana waliwavamia na kuwajeruhi waandishi wa habari na mkalimani waliyeambatana naye.


Waandishi hao wapo wilayani humo kwa ajili ya kufuatilia mchakato wa uhamaji kwa hiari wa wananchi ndani ya hifadhi hiyo kwenda Msomera wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga unaofanywa na Serikali.


Waandishi waliojeruhiwa ni Ferdinand Shayo wa ITV, Denis Msacky (mwandishi wa kujitegemea), Habib Mchange (Jamvi la Habari), mkazi mwingine wa Ngorongoro, Lengai Ngoishie na Janeth Joseph (mwandishi wa habari hii).


Majeruhi hao wanapatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Fame, iliyopo wilayani Karatu, mkoani Arusha.


Mwandishi huyo alieleza kuwa, wakati wakiendelea kutoa elimu hiyo, waliibuka baadhi ya watu waliokuwa wakiwafukuza wananchi waliokusanyika kusikiliza yaliyokuwa yakizungumzwa.


Licha ya kuwataka waondoke, wananchi waligoma kuondoka ili wasikilize kilichokuwa kikizungumzwa.


Vijana hao walikuwa wamebeba mapanga, mikuki, sime na mishale. Wakati tukio hilo linatokea Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Oleshangai alikuwepo eneo la tukio na baada ya vijana hao kuvamia na kujeruhi aliondoka eneo hilo.


Alipotafutwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mwangwala kuzungumzia suala hilo, alisema anatuma askari kufika eneo hilo la tukio.


Mwandishi wa habari hii alisema walipokuwa wakiendelea kusikiliza yale ambayo yalikuwa yakizungumzwa katika kusanyiko lile ndipo kulipoibuka kundi la vijana wakiwa wamebeba silaha na kuanza kuwashambulia waandishi hao, kwa mapanga, mikuki na mishale na kuwasababishia majeraja katika miili yao,” alieleza Janeth.


Alisema awali wananchi walipoanza kufukuzwa katika eneo hilo Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Ole Shangai alikuwa amekaa pembeni akiwa amegeuzia wananchi mgongo, huku akiendelea na mazungumzo na watu aliokuwa amekaa nao, vijana wengine wakipanda na kushuka kwenye gari lake huku wengine wakionekana makundi kwa makundi.


“Dakika chache baada ya mbunge huyo kuondoka, waliibuka vijana hao zaidi ya 200 wakiwa na silaha na kuanza kuwashambulia waandishi wa habari, huku wengine wakijiokoa kwa kukimbilia kwenye magari,” amesema.


Alipotafutwa kwa simu jana kuzungumzia suala hilo, mbunge huyo alisema aliondoka eneo hilo baada ya kumaliza shughuli zake mnadani. “Nilikuwepo mnadani kama mwananchi mwingine nikiuza ng’ombe, baada ya muda nikawaambia wenzangu ngoja niende nyumbani nikameze dawa, hivyo nikaondoka. “Nilikuja kusikia hili tukio baadaye na sihusiki kwa namna yoyote,” amesema.


 Akizungumza Mwananchi hospitalini hapo, muuguzi wa zamu, Siana Nkya alisema aliwapokea majeruhi hao saa 12 jioni na wanaendelea na vipimo zaidi kujua kama kuna madhara makubwa.


Alipopigiwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi Justine Masejo ili azungumzie tukio hilo, alijibu kwa kifupi yupo kikaoni na kukata simu.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad