Yanga Washindwe Wenyewe tu Ratiba Ligi Kuu Msimu Mpya
YANGA ishindwe yenyewe tu kwa namna neema ilivyoiangukia mapema kabla ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na michuano ya CAF haijaanza kutokana na ratiba ilivyowakalia utamu.
Ligi Kuu Bara inatarajiwa kuanza Agosti 15 na Yanga imepangwa kuanzia nyumbani katika mechi tatu mfululizo, kisha hata kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ikipata ulaini kwa kutakiwa kucheza zote jijini Dar es Salaam.
Yanga itaanza Ligi Kuu dhidi KMC, kisha kuialika JKT Tanzania na Namungo zote hizo zitapigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, wakati huo huo za CAF Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) dhidi ya Asas FC ya Djibouti zote zitapigwa hapohapo.
Sababu ya Djibouti kuomba mechi ya nyumbani na ugenini kucheza Tanzania zinatajwa ni viwanja vyao kutokidhi kanuni za FIFA, hivyo ni faida kwa Yanga kujipanga zaidi kutumia uwanja wa nyumbani.
Yanga mara baada ya mchezo wa Ngao ya Jamii watarudi kujiweka sawa na mchezo wao wa hatua ya kwanza unaotarajiwa kuchezwa kati ya Agosti 18-20 dhidi ya Asas FC ya Djibouti.
Lakini taarifa mbaya kwa Yanga ni kwamba Simba itamalizia mechi zake zote tatu za ligi nyumbani katika mbio za ubingwa.