TIMU ya Yanga imetinga hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Asas FC ya Djibouti.
Yanga inafuzu hatua hiyo kwa ushindi wa jumla ya mabao 7-1, baada ya mchezo wa kwanza uliochezwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi kushinda
Mabao ya wenyeji yamefungwa na Maxi Nzengeli aliyefunga mawili dakika ya saba na 90, Hafiz Konkoni dakika ya 45, Pacome Zouzoua (55) na Clement Mzize (69).
Bao la kufutia machozi kwa wageni limefungwa kwa mkwaju wa penalti na nyota wa timu hiyo, Tito Lukciir Madul Mayor katika dakika ya 85.
Zifuatazo ni dondoo za mchezo huu wa marudiano:
Tangu kocha, Miguel Gamondi ateuliwe kukiongoza kikosi cha Yanga Juni 24, mwaka huu, akichukua nafasi ya Nasreddine Nabi aliyetua FAR Rabat ya Morocco huu ndio mchezo wa kwanza kwake kuruhusu bao ndani ya dakika 90 katika michuano ya kiushindani.
Mchezo wa kwanza kwa Gamondi alianza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC katika nusu fainali ya Ngao ya Jamii, kisha kupoteza fainali mbele ya Simba kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya timu hizo kutoka suluhu ndani ya dakika 90.
Baada ya hapo ikahamishia nguvu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali ambapo aliichapa ASAS FC ya Djibouti kwa mabao 2-0, yaliyofungwa na Stephane Aziz KI na Kennedy Musonda.
Gamondi hakuishia hapo kwani wapinzani waliendelea kutaabika kwani katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu alianza kwa kishindo baada ya kuichapa KMC mabao 5-0.
Mabao ya Yanga katika mchezo huo yalifungwa na Dickson Job, Stephane Aziz KI, Hafiz Konkoni, Mudathir Yahya na Pacome Zouzoua.
Ushindi kwa Yanga unaifanya kutinga hatua ya kwanza ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo sasa itakutana na El Merreikh ya Sudan.
Yanga inakutana na El Merreikh iliyoitoa AS Otoho d'oyo ya Congo Brazzaville kwa faida ya bao la ugenini, baada ya timu hizo kufungana bao 1-1 katika mechi ya kwanza iliyochezwa wiki iliyopita kisha jana kutoka suluhu.
Yanga itaanzia ugenini katika hatua inayofuata nchini Rwanda ambako El Merreikh imechagua Uwanja wa Huye kuutumia katika mechi zake za nyumbani ambao hutumiwa na timu ya Mukura Victory Sports ya nchini humo.
Mechi ya mkondo wa kwanza itachezwa kati ya Septemba 15-17, huku ile marudiano ikichezwa kati ya Septemba 29 hadi Oktoba Mosi ambapo mshindi wa jumla atafuzu moja kwa moja hatua ya makundi itakayoanza kati ya Novemba 24-26.