Yote Aliyoyasema Rais Samia Mkutano wa BRICS

 

Yote Aliyoyasema Rais Samia Mkutano wa BRICS

Wakati viongozi wa umoja wa mataifa yanayochipukia kiuchumi (Brics), wakitangaza kuzipokea nchi sita kuwa wanachama wapya kuanzia mwaka ujao, Rais Samia Suluhu Hassan ametaka ushirikiano wa umoja huo na Afrika kujikita kwenye kufungua fursa barani humo, ili kufikia azma ya Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDGs). Ili kufikia malengo hayo, alisema kuna haja ya kuuimarisha Umoja wa Mataifa ili kuongeza ushirikiano wa mataifa, huku akipendekeza kubadilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili liwe na uwakilishi wa haki. Brics, inayoundwa na nchi za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini, zilikubaliana katika mkutano wao kuzifanya Argentina, Ethiopia, Iran, Saudi Arabia, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuwa wanachama kamili kuanzia Januari Mosi, Katika mkutano huo wa siku tatu uliohitimishwa jana huko Johannesburg, Afrika Kusini, viongozi zaidi ya 50 kutoka mataifa yasiyo wanachama wa Brics walihudhuria, akiwemo Rais Samia. Takribani nchi 40 duniani zimeonyesha nia ya kuwa wanachama, huku 23 zikiwa tayari zimetuma maombi yao. Wanachama wa Brics wamekubaliana kulipanua kundi hilo kwa kuongeza wanachama wapya waliokidhi vigezo.


Alichosema Rais Samia Akihutubia mkutano huo, Rais Samia alisema Brics inatoa nafasi ya kuja na mikakati ya haki na usawa katika kushughulikia masuala ya kiuchumi kupitia ushirikiano wake na bara la Afrika. Alisema kuna haja ya kuuimarisha Umoja wa Mataifa ili kuongeza ushirikiano wa mataifa katika masuala mbalimbali hasa sasa ambapo chombo hicho kimefikisha miaka 78. “Tanzania, kwa sababu hiyo, ingependa kupaza sauti kwamba kuna haja ya kubadilisha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulifanya liwe na uwakilishi wa haki, thabiti na linaloakisi hali halisi za siasa za kijiografia za sasa,” alisema Samia na kuongeza kuwa Tanzania inaunga mkono ushirikiano jumuishi. Alisema matarajio ya Tanzania ni kuona kwamba masuala ya Afrika na vipaumbele vyake, vinaendelea kuchukua nafasi kwenye mikutano ijayo ya Brics. “Ushirikiano wa Brics na Afrika unatakiwa kujikita katika kufungua fursa muhimu katika bara hili ili kufikia malengo ya Agenda 2063 na Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDG) ambayo yanahusisha kuimarisha soko huru la Afrika,” alisema.


Wanachama wapya Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa alitangaza kwamba Brics itapokea wanachama wapya sita baada ya kuwa wamekubaliana katika kikao chao, huku nchi za Afrika zikiongezeka kufikia tatu ambazo ni Afrika Kusini, Misri na Ethiopia. “Tumeamua kuzikaribisha Argentina, Misri, Ethiopia, Iran, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuwa wanachama kamili wa Brics. Uanachama wao utaanza rasmi Januari Mosi, 2024,” Rais Ramaphosa aliuambia mkutano huo wa kilele jijini Johannesburg. Lakini kundi hilo ambalo hufanya uamuzi kwa makubaliano, lilikuwa limekubaliana juu ya “kanuni elekezi, viwango, vigezo na taratibu za mchakato wa kuipanua Brics. “Upanuzi huu wa wanachama ni wa kihistoria,” alisema Rais wa China, Xi Jinping ambaye taifa lake ndilo lenye nguvu zaidi katika kundi la mataifa yasiyo ya Magharibi ambayo yanawakilisha robo ya uchumi wa dunia. “Upanuzi huo pia ni mwanzo mpya wa ushirikiano wa Brics. Utaleta nguvu mpya katika utaratibu wa ushirikiano wa Brics na kuimarisha zaidi amani na maendeleo ya dunia,” aliongeza Rais Jinping.


Brics kuwa na sauti duniani Akizungumzia ongezeko la wanachama wa Brics, mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Denis Konga alisema hiyo inaonyesha kushindwa kwa nchi za Magharibi katika kutatua changamoto za dunia, hivyo kundi hili alisema linajiona limetengwa, sasa wanatengeneza nguvu nyingine ya kulinda maslahi yao katika siasa na uchumi wa dunia. “Ukiangalia mataifa yaliyoongezeka, hamna taifa dhaifu, yote yana nguvu kiuchumi. Nchi kama Iran, Falme za Kiarabu, hii itaifanya Brics kuwa na sauti katika siasa na uchumi wa dunia,” alisema Konga. Kuhusu manufaa ya Brics kwa mataifa yasiyo wanachama kama Tanzania, Konga alisema yatanufaika kwa kuweka msukumo kwa mataifa ya Magharibi kutekeleza mipango yao kwa kuhofia kwamba wasipofanya watapata msaada upande wa pili wa Brics. “Tanzania haifungamani na upande wowote, kwa hiyo sasa inaweza kuomba usaidizi kwenye nchi za Brics, kwa maana kwamba kama nyinyi hamtatupa tutakwenda upande wa Magharibi’. Kwa hiyo kutakuwa na pande mbili zenye nguvu na nchi zetu zitachagua nani wa kushirikiana naye,” alisema. Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed alipongeza kile alichokiita “wakati mzuri” kwa nchi yake. “Ethiopia iko tayari kushirikiana na wote kwa ajili ya utaratibu unaojumuisha na wenye mafanikio wa kimataifa,” alisema kwenye mtandao wa X.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad