Baada ya Kuzitolea Mbavuni TIMU za Bongo, Simon Msuva Atoa Kauli Nzito Kuhusu Simba na Yanga
Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva amepanga kufunga zaidi ya mabao 10 kwenye msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu Algeria ‘Ligue Professionnelle 1’ akiwa na JS Kabylie, huku akifunguka alivyowatosa Simba na Yanga.
Msuva alitambulishwa usiku wa Jumatatu kuwa mchezaji rasmi wa JS Kabylie baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya zaidi ya Sh1 bilioni.
Mshambuliaji huyo ambaye pia alikuwa akihusishwa na CR Belouizdad, alisema, “Namshukuru Mungu kwa sababu kila kitu kimekaa sawa, kilichobaki ni kuwafanyia kazi tu, nasubiri kwa hamu kuanza msimu mpya nikiwa na JS Kabylie, ni moja ya klabu kubwa na yenye historia nzuri.”
Msimu uliopita Msuva aliichezea Al-Qadsiah FC ya Ligi Daraja la Kwanza Saudi Arabia nusu msimu na kupachika mabao manane.
Nyota huyo wa zamani wa Raja Casablanca na Difaa El Jadida za Morocco, aliendelea kusema,
“Nimejiwekea malengo ya kufunga zaidi ya mabao 10, nataka kuisaidia timu kufikia malengo, najua tabia ya timu za Kiarabu kwa sababu nimecheza soka Morocco na mara kadhaa nimekutana na timu za Algeria kwenye michuano ya kimataifa.”
JS Kabylie ambayo ilianzishwa miaka 77 iliyopita ni miongoni mwa timu zenye mafanikio kwenye soka la Algeria, imebeba ubingwa mara 14 ligi kuu nchini humo, mara tano kombe la Algeria, huku upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika ikibeba mara mbili kwenye miaka ya 1981 na 1990.
Msimu mpya wa Ligi Kuu Algeria unatarajiwa kuanza kutimua vumbi mwezi ujao.
KUHUSU SIMBA NA YANGA
Msuva ambaye alikuwa kwenye rada za Simba na Yanga alisema licha ya kufuatwa na klabu hizo kwa nyakati tofauti hakuona kuwa ni wakati sahihi kwake kurejesha majeshi kwa kucheza soka la kulipwa nyumbani.
“Najiona bado nina nafasi ya kuendelea kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, ndio maana ilikuwa ngumu kwangu kukubaliana na ofa za Simba na Yanga ambazo zilikuwa nzuri tu, wakati ukifika nitarudi na kumalizia mpira wangu nyumbani hilo lipo wazi,” alisema nyota huyo.