Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limetangaza kuwepo kwa changamoto ya upungufu wa umeme wa Megawati 400 katika vituo vyao vya uzalishaji umeme nchini.
Shirika hilo limesema upungufu huo unachangiwa na ongezeko la mahitaji ya umeme kutokana na kukua kwa shughuli za kiuchumi, upungufu wa maji kwenye vituo vya kufua umeme unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na matengenezo yanayoendelea kwenye visima vya gesi asilia na mitambo ya kuzalisha umeme kwa gesi asilia.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Gissima Nyamo- Hanga alisema kufuatia hali hiyo baadhi ya maeneo nchini yamekua yanakosa huduma ya umeme kwa nyakati tofauti.
Amesema Shirika hilo limepokea na tayari limanza kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Nishati na tayari jitihada mahususi za utekelezaji kukabiliana na changamoto hii zimeanza kwa kuharakisha matengenezo ya mitambo ya kuzalisha umeme na ya visima vya gesi asilia kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
"Ni matarajio yetu kuwa ndani ya mwezi Oktoba kutakamilika kwa matengenezo hayo kutawezesha kupata nafuu ya makali ya upungufu wa umeme na ndani ya miezi sita tutahakikisha tunaondokana na kadhia hii ya upungufu wa umeme," amesema Hanga
Aidha amesema Shirika linaendelea kukamilisha utekelezaji wa mradi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Julius Nyerere litakalokuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2115 ambao mpaka sasa umefikia asilimia 92.
"Pindi mradi huu utakapokamlika na kuingizwa kwenye gridi ya Taifa utachangia kuimarika kwa hali ya umeme nchini kwa kiasi kikubwa," amesema Hanga na kuongeza
"Shirika linawashukuru wateja wake na kuwaomba kwa wavumilivu katika kipindi hiki cha mpito na kwamba Tanesco itaendelea kutoa taarifa za upatikanaji wa umeme kwa kadri hali itavyozidi kuimarika," amesema