Marekani. Spika wa Bunge la Marekani, Kevin McCarthy jana Jumanne Septemba 12, 2023 alitangaza kuwa analiagiza Bunge hilo kufungua hati ya uchunguzi wa kumuondoa madarakani Rais Joe Biden kutokana na shughuli za kibiashara za familia yake kuhusishwa na rushwa.
Endapo agizo hilo litafanikiwa itakuwa ni histotia kwa nchi hiyo ikiwa ni miezi michache imesalia kuelekea Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo wa mwaka 2024.
McCarthy amesema: "Uchunguzi wa Bunge hadi sasa unatoa picha ya utamaduni wa ufisadi katika familia ya Rais Biden"
Wakati hayo yakiendelea pia wanachama wa chama pinzani cha Rais Biden, Republican wanafuatilia kwa karibu biashara na shughuli za mtoto wa Rais, Hunter Biden.
"Haya ni madai ya matumizi mabaya ya madaraka, kizuizi na rushwa, na yanastahili uchunguzi zaidi wa Bunge," amesema McCarthy huku akitangaza kuwa analielekeza Bunge likiongozwa na Kamati ya Uangalizi kufungua uchunguzi rasmi wa mashtaka hayo.
Wakati hayo yanaendelea taarifa kutoka Ikulu ya Marekani kupitia msemaji wake, Ian Sams ilijibu mashambulizi hayo kwa kuyaita ni ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu.
"Hizo ni siasa mbaya kuelekea Uchaguzi Mkuu. Wanachama wa Republican waliopo bungeni wamekuwa wakimchunguza Rais kwa miezi tisa, na hawajapata ushahidi wowote wa kufanya makosa," alisema msemaji Ian Sams.