Cheyo: Serikali Inatafuta Namna ya Kuukwepa Mchakato wa Katiba



Dar es Salaam. Mwenyekiti wa chama cha DP, John Cheyo amesema Serikali inatafuta njia ya kuukwepa mchakato wa katiba kwa kuleta miaka mitatu ya kutoa elimu kwa wananchi.

“Watanzania tunatatizo moja kubwa la kutokuambiana ukweli na kusifiana na hili ni tatizo. Serikali imezungumza juu ya elimu, kitu ambacho kinawatia wasiwasi ni darasa la watu milioni 60 kwa kipindi cha miaka mitatu, ni kama vile Serikali inatafuta njia ya kuukwepa mchakato huu kwa ujanjaujanja,”amesema.

Cheyo ametoa kauli hiyo jana Jumatano Septemba 13, 2023 wakati akichangia katika mkutano maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa na wadau wa demokrasia kutathimini mapendekezo ya kikosi kazi na hali ya siasa.

“Sisi wazee tusiposema tutakuwa tunadanganya. Mimi nashauri kikao hiki ni cha baraza la wadau, kamati ya uongozi ya baraza kingekaa na kwenda kukutana na Rais na kuona hili la elimu ni mwendelezo,” amesema.


Cheyo aliyewahi kuwa mbunge wa Bariadi Mashariki alikuwa akijenga hoja juu ya suala la elimu ya Katiba kutolewa kwa miaka mitatu akisema “Watanzania tusiwaone hawawezi kuzunguma, Mzee Warioba ametembelea nchi nzima, Jaji Kisanga naye alitembea nchi nzima, Kikosi kazi kimezungumza, Bunge la Katiba limekaa live. Mimi nilikuwa mbunge wa Katiba, tumekula hela nyingi, leo tuzitupe kwenye 'dust bin' na Rais alikuwa makamu mwenyekiti wa Bunge la Katiba!"

Alisema sababu kubwa ya waliotoka ndani wakati wa Bunge la Katiba ilikuwa ni muundo wa Serikali, “lile kundi lilitaka Serilali tatu na CCM piga ua wanataka Serikali mbili.

Kauli hiyo inakuja ikiwa siku mbili zimepita tangu Rais Samia Suluhu Hassan atoe msimamo wa Serikali wa kuanza na kutoa elimu ya katiba kwa wananchi ili waielewe huku akionya jambo hilo sio la wanasiasa pekee.


"Wote tunakubaliana na suala la kutaka maboresho ya katiba, lakini jambo hili ni mchakato sio suala la wanasiasa pekee..ni mali ya wananchi,"alisema Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia katika mkutano maalumu wa baraza la vyama vya siasa na wadau wa demokrasia Septemba 11, 2023 jijini Dar es Salaam.

Mwananchi

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad