Dar es Salaam. Jumla ya watahiniwa 1,397,370 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi utakaofanyika Septemba 13 na 14 nchini kote.
Kati ya watahiniwa hao, 654,652 ni wavulana sawa na asilimia 46.85 na wasichana ni 742,718 sawa na asilimia 53.15.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Said Ally Mohamed ametumia fursa hiyo kuwataka watu wote wanaohusika na mitihani hiyo kuzingatia sheria na kujiepusha na aina zote za udanganyifu.
Dk Mohamed amesema kwa wanafunzi watakaobainika kufanya udanganyifu matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa kanuni za mitihani na wahusika wengine watachukuliwa hatua za kwa mujibu wa sheria.
Mbali na kufuta matokeo ya watahiniwa amesema baraza hilo halitasita kuvifungia vituo vya mitihani ambavyo vitabainika kuratibu vitendo vya udanganyifu.
“Tunaamini wanafunzi wameandaliwa vyema katika kipindi chote cha miaka saba, hatutegemei kuona watahiniwa wanafanya udanganyifu kwa kuwa tutawafutia matokeo. Si kitu tunachokipenda kuona mtoto amesoma miaka saba halafu anafutiwa matokeo,” amesema Dk Mohamed.
Katibu Mtendaji huyo ametumia fursa hiyo kuwataka wakuu wa shule kutekeleza majukumu yao ya usimamizi kwa kuzingatia mwongozo wa usimamizi na kuepuka kuingilia usimamizi wa watahiniwa ndani ya vyumba vya mtihani.