Dodoma. Ni matumaini mapya. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya majaribio ya tiba ya virusi vya Ukimwi (VVU) kutarajiwa kuanza nchini Denmark kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Tiba hiyo iliyosubiriwa kwa muda mrefu inatarajiwa kuanza baada ya matokeo ya majaribio ya awali ya maabara, yaliyofanywa na timu mbili za wanasayansi wa Australia kwa ushirikiano na wenzao kutoka Denmark kuonyesha matumaini ya kupata dawa.
Matumaini haya yanakuja ikiwa imepita miaka 40 tangu Ukimwi uingie Tanzania, huku takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zikionyesha karibu watu milioni 40 wanaishi na VVU duniani.
Mwakani pamoja na Denmark, majaribio ya dawa hiyo pia yataanza huko Melbourne, Australia. Utafiti wa Australia umehakikisha kuwa, dawa ya Oncologic venetoclax ina uwezo wa kuchunguza seli katika mwili wa binadamu ambazo zinaathiriwa na virusi, suala ambalo lilikuwa gumu kwa tafiti zote zilizofanywa kwa miaka 40 iliyopita.
Kutokana na uwezo wa dawa hiyo, vidonge vyenye jina la kibiashara la Venclexta vilitengenezwa awali ili kupambana na saratani ya damu.
Ilithibitishwa nchini Marekani mwaka 2016 na tangu wakati huo kwa mujibu wa madaktari, tayari imesaidia maelfu ya wagonjwa wa saratani.
Uchunguzi na hatimaye utumiaji wa dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo unawezesha kuzuia kuongezeka kwa virusi vya Ukimwi, hali inayozuia uharibifu wa kinga ya mwathiriwa mara moja.
Mwathirika anapotumia dawa za kufubaza makali kwa kufuata masharti ya dozi, virusi hupunguza kasi ya kuzaliana, lakini anapoacha huzaliana kwa wingi na kupunguza kinga za mwili, hivyo hupata magonjwa nyemelezi.
Hata hivyo, baadhi ya Watanzania wamekuwa na maoni tofauti.
“Majaribio haya yamekuwa ya muda mrefu sasa, sijajua kwa nini mpaka leo hii dawa haijapatikana, bado tunasubiri kuona sasa maana majaribio haya angalau yamefika hatua ya mwisho,” alisema Hamisi Nelum, mkazi wa Mpwapwa mkoani Dodoma.
Mratibu wa muunganiko wa mashirika yanayofanya uchechemuzi kuhusu masuala ya VVU (Compass Tanzania), Francis Luwole alisema kuna umuhimu wa kuwa na tiba kwani waviu milioni 1.7 nchini kila siku lazima watumie dawa za kufubaza makali ya Ukimwi (ARV) ambazo upatikanaji wake kwa asilimia 93 nchi unategemea wafadhili.
“Kwa mwezi mgonjwa mmoja anatumia zaidi ya Sh4 milioni kuhakikisha anapewa dawa na vipimo. Sasa matumizi ya ARV siyo endelevu pindi ikitokea hakuna hizo fedha wanaoishi na maambukizi watasitisha huduma ya dawa na wanapata magonjwa nyemelezi,” alisema Luwole.
Tafiti nchini
Tafiti mbalimbali za chanjo zimekuwa zikiendelea nchini. Utafiti wa kundi la watu wa Afrika (Africos) ambao unafanyika katika nchi nne za Afrika ambazo ni Tanzania, Afrika Kusini, Nigeria na Kenya umesaidia kuboresha huduma za matibabu kama vile upatikanaji wa ARV.
Mtafiti wa Virusi vya Ukimwi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr), Kanda ya Mbeya, Dk Reginald Gervas alisema utafiti huo ni wa kwanza kuwahusisha watu wa Afrika na utasaidia matibabu rafiki kwa wananchi.
Alisema awali utafiti kuhusu maambukizi ya virusi vya Ukimwi ulikuwa unafanyika kwenye nchi zilizoendelea, hivyo utafiti huu kuhusisha Waafrika utasaidia kutoa tiba sahihi kwa watu wanaoishi na Ukimwi.
“Utafiti wa Africos ambao unasaidia utafiti wa Ukimwi umesaidia kuboresha sera ya matibabu, kupunguza usugu wa dawa, pamoja na ushauri wa upatikanaji wa huduma za pamoja za Ukimwi na magonjwa yasiyoambukiza,” alisema Dk Gervas ambaye pia ni Mratibu wa Africos.
Naye, Meneja wa Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini Nimr mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Dk Nyanda Ntinginya alisema wameendelea kufanya tafiti na kuratibu utafiti wa Africos pamoja na maabara inayotembea ili kuwapatia wananchi tiba sahihi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Mapambano ya VVU nchini
Mapambano yalianza baada ya kuwagundua wagonjwa watatu wa kwanza Novemba, 1983 katika Hospitali ya Ndolage mkoani Kagera. Baada ya hapo Ukimwi ulienea kwa kasi kubwa.
Mwaka 1984 wagonjwa wengine wapya wapatao 106 walitambuliwa na idadi iliongezeka kufikia 295 mwaka 1985, na wagonjwa 1,121 mwaka 1986.
Mwaka 1999, Serikali ilitangaza VVU kuwa janga la Taifa, na mapambano yaliimarishwa zaidi baada ya kuanzishwa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) mwaka 2001. Mwaka 2003 Tanzania ilianza kutumia dawa za kufubaza makali ya ugonjwa huo (ARV).
Hali ya maambukizi
Kwa mujibu wa ripoti ya Juni, 2021 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kiwango cha maambukizi ya VVU kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi ni asilimia 4.9, miongoni mwao asilimia 6.3 ni wanawake.
Ofisa Ufuatiliaji na Tathimini wa Tacaids, Nyangusi Laiser alisema maambukizi mapya katika maeneo ya mjini ni asilimia 5.5, huku ya vijijini yakiwa ni asilimia 4.2. Idadi ya watu wanaoishi na VVU kufikia Novemba mwaka 2021 ni milioni 1.7.