Dk Slaa: Ubalozi utabaki historia, nitaendelea kusema

Dk Slaa: Ubalozi utabaki historia, nitaendelea kusema


Dar es Salaam. Muda mfupi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumvua ubalozi Dk Willbrod Slaa, mwanasiasa huyo amesema kazi aliyoifanya itabaki kuwa historia, lakini ataendelea kusema anachokiamini moyoni mwake.

Taarifa ya kuvuliwa ubalozi kwa Dk Slaa imetolewa leo Septemba 1, 2023 na Ikulu, bila kutoa sababu ya hatua hiyo, ikihitimisha miaka sita ya uanadiplomasia tangu alipoteuliwa na Hayati Rais John Magufuli Novemba 23, 2017.

Akizungumza na Mwananchi leo Septemba 1, Dk Slaa aliyewahi kuwa Katibu mkuu wa Chadema kabla ya kujiuzulu mwaka 2015, amekiri kuiona taarifa ya Ikulu.

"Watu walikupa kitu chao wakachukua, sasa unawahoji nini tena?" amehoji.

Siku za hivi karibuni Dk Slaa amekuwa akiikosoa Serikali na Agosti 13 alikamatwa na Polisi na kupelekwa mkoani Mbeya ambako aliunganishwa na Wakili Boniface Mwabukusi na kada wa Chadema, Mdude Nyagali wakihusishwa na makosa ya uchochezi.

Alipoulizwa kuhusu ukosoaji wake huo, Dk Slaa amesema, "Mimi najitambua, nitaendelea kusema kile ambacho nakiamini kwa moyo wangu na kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.

"Najitambua kwamba ninasimama wapi kwa kwenye issue za Taifa langu, kwa hiyo nitaendelea kufanya kazi kwa ajili ya Taifa langu."

Alipoulizwa kama hajutii kupoteza ubalozi, alisema kazi hiyo kwake itabaki kuwa historia.

"Mimi nimesomea PhD kwa kusota, ubalozi nimefanya kazi yangu na itabaki kwenye historia sasa najutia nini?

"Nchi nilizotumikia ndio zinajua kwamba walikuwa na balozi wa aina gani katika kipindi changu, kwamba walikuwa na balozi wa aina gani," amesema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad