ALIYEKUWA kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima amefichua kinachoendelea nchini humo, kwa upande wa hali ya hewa na jinsi mashabiki wa soka walivyo na hamu ya kukiona kikosi cha Wanajangwani, kikicheza dhidi ya Al -Merrikh, Septemba 16.
Yanga itavaana na Al Merreikh Uwanja wa Pele, Rwanda ukiwa ni mchezo wa kwanza wa hatua ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Niyonzima alisema hali ya hewa ni nzuri, mvua zinanyesha kiasi, jambo analoliona haliwezi kuwadhuru chochote wachezaji na mashabiki wa Yanga wanaosafiri kwa wingi kwenda kuisapoti timu yao.
“Mashabiki wa Rwanda wanaipenda sana Yanga na wana hamu ya kuwaona wachezaji na kwenda kuwaunga mkono siku ya mechi, kwa hilo tu wakija huku hawawezi kujisikia wapweke, watakutana na ndugu zao wanaowaunga mkono.”
“Ukiondoa mashabiki mimi mwenyewe nitakuwa wa kwanza kwenda kuwapokea, kama unavyojua Yanga ilinikarimu sana kwa maana ya mashabiki na viongozi walinipokea vizuri, mimi ni nani nishindwe kwenda kuiunga mkono itakapokuja huku Rwanda, hiyo ni lazima na siyo ombi.”
Alisema anatambua mchezo utakuwa mgumu ila anaamini Yanga inaweza ikapata ushindi kulingana na kufanya vyema kwenye michezo iliyopita dhidi ya Asas ya Djibout, ikishinda jumla ya mabao 7-1 mchezo wa nyumbani na ugenini, yote ikipigwa Uwanja wa Azam Complex, Chamanzi.
“Yanga ina kikosi kizuri kinachoweza kupambana kupata matokeo dhidi ya Al-Merrikh, kikubwa ni wachezaji kujituma hakuna kinachoshindikana nje,” alisema.