Hatima Uchunguzi Mwanamke Aliyefia Mahabusu Kujulikana
Uamuzi wa uchunguzi wa chanzo cha kifo cha mwanamke anayedaiwa kufariki dunia akiwa mahabusu katika kituo cha Polis Mburahati jijini Dar es Salaam, Stella Moses sasa unatarajiwa kutolewa Septemba 21, mwaka huu.
Uamuzi huo ulipangwa kutolewa na Mahakama ya Korona, leo Jumanne Septemba 12, 2023, baada ya kukamilisha Mwenendo wa uchunguzi imiwa ni pamoja na kupitia majumuisho ya hoja za mlalamikaji.
Hata hivyo mahakama hiyo inayoketi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam Kivukoni (Kinondoni) iliyoko katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki, Kinondoni, imeshindwa kutoa uamuzi huo na badala yake imesogeza mbele tarehe ya uamuzi huo mpaka Septemba 21 kutoka na kutokukamilika.
Korona aliyeendesha shauri hilo, Jackline Rugemalira, ambaye ni Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, amesema kuwa hakuweza kukamilisha kuandika uamuzi huo kutokana na sababu za kiafya, tatizo lililomlazimu kufanyiwa upasuaji nje ya nchi.
Stella alifariki dunia usiku wa Desemba 20, 2020, akiwa mahabusu kituoni hapo alikojisalimisha baada ya kupata taarifa kuwa alikuwa anahitajika, tukio ambao lilizua mvutano mkubwa baina ya Polisi na ndugu wa marehemu kwa kile wanachodai kuwa ni mazingira tata ya kifo hicho.
Katika tukio hilo lililoripotiwa kwa kina na Mwananchi katika toleo la Desemba 23, 2020, Jeshi la Polisi lilidai kuwa mwanamke huyo alifariki dunia baada ya kujinyinga akiwa mahabusu.
Ndugu wa marehemu walipinga taarifa hizo wakidai kuwa kulikuwa na utata wa mazingira ya kifo hicho na badala yake walitaka ufanyike uchunguzi huru ili kujua chanzo halisi cha kifo cha ndugu yao.
Hata hivyo Jeshi la lilipuuza madai yao hayo na hatimaye familia ililazimika kufanya mazishi bila hata kupewa matokeo ya uchunguzi wa chanzo cha kifo hicho uliofanywa na Hospitali ya Muhimbili.
Hivyo miaka miwili baadaye ndugu wa marehemu walifungua shauri la maombi dhidi ya viongozi wa Jeshi la Polisi na uongozi wa Hospitali ya Muhimbili kwa kutokutimiza wajibu wao.
Shauri hilo lilifunguliwa na shemeji wa marehemu Emmanuel Kagongo dhidi ya Viongozi wa Jeshi la Polisi na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni (Kinondoni) akiomba mahakama hiyo iridhie kufanya uchunguzi huru.
Walalamikiwa katika shauri hilo ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (Inspekta Jenerali wa Polisi – IGP), Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam (ZPC) na Kamanda wa Polis Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RPC).
Wengine ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Mburahati (OCD), Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika hati ya maombi hayo ya jinai mchanganyiko namba 3 ya mwaka 2022, aliomba mahakama hiyo iridhie kufanya uchunguzi huru ili kujua ukweli wa mazingira ya kifo cha ndugu yao.
Awali, Serikali iliweka pingamizi dhidi ya shauri lililofunguliwa na familia ya marehemu ikitaka litupiliwe mbali kwa madai kuwa tayari imeshafungua shauri rasmi la uchunguzi wa chanzo cha kifo hicho.
Baada ya mvutano wa muda mrefu baina ya mawaili wa pande mbili, yaani wakili wa familia ya marehemu, Peter Madeleka na mawakili wa Serikali tofautitofauti walioendesha shauri hilo kwa nyakati tofautitofauti, hatimaye mahakama hiyo iliridhia maombi hayo.
Mahakama hiyo katika uamuzi uliotolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Franco Kiswaga ilisema kuwa itaendelea na shauri lililofunguliwa na familia na kwamba nyaraka zilizomo ndani ya jalada la Serikali zitakuwa ni sehemu tu ya mwenendo wa shauri lililofunguliwa na familia.
Katika uchunguzi huo, mahakama iliwahoji watu mbalimbali kupata ushahidi kuhusiana na mazingira ya kifo cha mwanamke huyo.
Miongoni mwao ni askari wa kituo hicho cha Polisi, daktari kutoka Muhimbili aliyesimamia uchunguzi wa sababu za kifo cha mwanamke huyo, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni (RPC), sasa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai.
Uamuzi huo ndiyo utakaoweka wazi mazingira na sababu za kifo cha mwanamke huyo na kama Mahakama hiyo itajirodhisha kuwa mwanamke huyo hakujinyinga bali aliuawa, basi itaelekeza hatua za kisheria za kuchukua dhidi ya watuhumiwa.
Kwa mujibu wa Wakili Madeleka, ndani ya jalada la kesi hiyo kuna taarifa mbili za uchunguzi wa chanzo cha kifo hicho, moja iliyofanywa na Dk Malima wa Jeshi la Polisi inayoeleza kuwa Stella alijinyonga, ambayo ilipokewa mahakamani hapo pamoja na ya Muhimbili inayoeleza kuwa alikufa kutokana na majeraha.