Dar es Salaam. Waziri Mkuu, mstaafu Jaji Joseph Warioba ameeleza wasiwasi wake kuhusu hatua ya Serikali ya kutaka kuanza kutoa elimu ya Katiba Mpya kwa miaka mitatu, akisema ni muda mrefu kwa mchakato huo.
“Tumefikia mahali kama kuna utashi wa kisiasa, tunaweza kuamua juu ya haya mabadiliko, inanipa wasiwasi, ni kama tunataka kuanza upya mchakato huu. Unaona mijadala hii ya Katiba inavyoingilia shughuli zetu za maendeleo, nadhani imefika wakati tufanye uamuzi,” amesema Jaji Warioba.
Jaji Warioba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, ameeleza hayo Ijumaa Agosti 31, 2023 katika mahojiano wa Azam TV yaliyofanyika nyumbani kwake wilayani Kinondoni, mkoani Dar es Salaam.
Juzi aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro, alisema watatoa elimu ya mabadiliko ya katiba kwa miaka mitatu, akisema kwamba utafiti walioufanya umeonekana kuwa zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania hawaifahamu Katiba na hata wengine hawajawahi kuiona.
Kauli hiyo, Dk Ndumbaro iliwaibua wadau mbalimbali wakiwemo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) na Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), waliokosoa hatua hiyo, wakisema inalenga kuchelewesha mchakatao huo.
Katika maelezo yake, Jaji Warioba amesema wakati akiwa mwenyekiti wa tume hiyo, wananchi walishiriki na walitoa elimu ya kutosha kuhusu Katiba Mpya, akisema walisambaza nakala za Katiba za Tanzania na Zanzibar.
Mbali na hilo, walifanya machapisho kueleza yaliyo katika Katiba na kusambamba katika maeneo mbalimbali ikiwemo vijijini, akisema kwa namna yanayoendelea hivi sasa huwezi kusema wananchi hawana elimu kuhusu mchakato huo.
“Kwa jinsi walivyoipanga sioni kama wanaweza kutoa mwanga zaidi kuliko walionao hivi sasa, Kamati ya Mukandala (Profesa Rwekiza), imechukua maoni ya kutosha na wananchi wanajua. Mimi natafsiri Serikali ingesema hatuwezi kupata Katiba Mpya sasa hivi, waseme mapema kuliko hivi,” amesema na kuongeza;
“Tunachohitaji sasa ni utashi wa kisiasa, vyombo vya habari vinazungumza sana kuhusu Katiba Mpya, ndivyo vinavyofikisha ujumbe kwa Watanzania sambamba na vyama vya siasa. Wananchi wamepata elimu ya kutosha kuhusu Katiba Mpya,” amesema Warioba.
Jaji Warioba aliyewahi kuhudumu katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki, amesema kinachotakiwa hivi sasa ni kwenda kura za maoni, akisema hawaelewi wanaosema mchakato uanze upya.
Mwananchi