Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema wamekuwa na muda wa kutosha kujiandaa na mchezo wa mkondo wa pili kuwania tiketi ya kutinga hatua ya makundi ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya Al Merrikh
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari mapema leo kuelekea mchezo huo utakaopigwa Jumamosi, Septemba 30 saa 1 usiku, Gamondi amesema wachezaji wote wako tayari kupambana katika mchezo huo muhimu katika historia ya Yanga
"Tumekuwa na muda wa kutosha kujiandaa na mchezo huu. Maandalizi ni mazuri, tuko tayari kucheza kandanda safi na kuwapa furaha Wananchi kwenye mchezo huu"
"Moja ya mambo yaliyonileta Yanga ni pamoja na michuano ya ligi ya mabingwa. Hii ndio michuano mikubwa zaidi barani Afrika kwa ngazi ya klabu. Nafahamu tuna zaidi ya miaka 25 hatujacheza hatua hii"
"Malengo na mipango yetu ni kuona tunapata matokeo mazuri na kufuzu hatua ya makundi. Pamoja na ushindi tuliopata mchezo wa kwanza, tutacheza mchezo huu kama matokeo ni 0-0 tutakuja uwanjani kupambana kama ni fainali na nitatumia tiimu yangu bora zaidi ili kuhakikisha tunapata matokeo tunayohitaji," alisema Gamondi
Gamondi amesema wachezaji wake wote wako tayari kwa mchezo huo wakiwa na ari, morali kubwa jukumu lake ni kuchagua wachezaji 11 ambao watakuwa na jukumu la kuhakikisha Yanga inaibuka na ushindi ili kutinga hatua ya makundi