KESI YA MJANE WA BILIONEA MSUYA: Shahidi aacha maswali taarifa ya mauaji

 

KESI YA MJANE WA BILIONEA MSUYA: Shahidi aacha maswali taarifa ya mauaji



Shahidi wa 24 katika kesi ya mauaji ya Aneth Msuya, amehitimisha ushahidi wake huku akiwa ameibua maswali kuhusu uhalali wa kielelezo kimoja kati ya viwili vilivyopokewa na Mahakama katika kesi hiyo kuhusu taarifa ya awali ya tukio la mauaji ya Aneth.


Shahidi huyo F832 Sajenti Obadia Joseph kutoka Makao Makuu ya Upelelezi Dodoma, Kitengo cha Kupambana na Kuzuia Madawa ya Kulevya alihitimisha. Ushahidi wake leo, Jumatatu, Septemba 11, 2023 baada ya kuhojiwa maswali ya dodoso na mawakili wa utetezi ukiwa ni mwendelezo wa mahojiano hayo yaliyoanza Ijumaa iliyopita.


Hata hivyo ameibua na kuacha maswali kadhaa baada ya  kuwasilisha kielelezo kingine na kupinga kielelezo kingine kama hicho kilichopokewa mahakamani kuwa si halali isipokuwa alichokiwasilisha yeye.


Hii ni kwa sababu kielelezo hicho ambacho shahidi huyo amekipinga, kilitolewa na shahidi wa upande wa mashtaka baada ya kuombwa na mawakili wa utetezi na waendesha mashtaka hawakupinga.


Kesi hiyo namba 103 /2018 inamkabili Miriam Steven Mrita ambaye ni mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara tajiri maarufu wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya; na mwenzake Revocatus Everist Muyella maarufu Ray.


Aneth ambaye aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo) jijini Dar es Salaam, alikuwa mdogo wa Bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai mkoani Kilimanjaro Agosti 7, 2013.


Machi Mosi, 2022, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilipokea nakala kivuli ya Ilani ya Kwanza (taarifa ya awali ya Polisi ya tukio la mauaji ya Aneth) na kuiorodhesha kama kielelezo cha Tatu cha upande wa utetezi (DE3).


Kielelezo hicho kilitolewa na shahidi wa nne wa upande wa mashtaka, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Richard Mwaisemba, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kigamboni (OC-CID), wakati akitoa ushahidi wake,


SSP Mwaisemba alitoa kielelezo hicho ambacho ni nakala kivuli, baada ya kuombwa na Wakili Peter Kibatala anayemwakilisha mshtakiwa wa kwanza, Miriam; wakati akimhoji maswali ya dodoso shahidi huyo kuhusiana na ushahidi wake alioutoa na upande wa mashtaka haukuwa na pingamizi.


Lakini Ijumaa iliyopita, Septemba 8, Mwaka huu, shahidi huyo wa 24, Sajenti Obadiah pia aliwasilisha mahakamani hapo Ilani ya Kwanza nyingine kuhusiana na mauaji hayo, ambayo pia ilipokewa na Mahakama na kuwa kielelezo cha 17 cha upande wa mashtaka (PE17).


Shahidi huyo hakuwepo katika orodha ya mashahidi wa Jamhuri waliokuwa wamebainishwa lakini aliongezwa katika orodha hiyo kwa lengo la kuwasilisha Kielelezo hicho kupingana na Kielelezo cha awali baada ya shahidi wa 22 kuelezea kushangazwa na namna Upande wa utetezi ulivyoipa taarifa hiyo.


Shahidi huyo wa 22, Mkuu wa Upelelelezi mkoa wa Arusha (RCO) Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) David Paulo Mhanaya, ambaye alikuwa Mkuu wa timu ya upelelezi wa kesi hiyo wakati akihojiwa na Wakili Kibatala kuhusiana na Ushahidi wake baada ya kuoneshwa taarifa hiyo alitahamaki na kuhoji wameipata wapi.


Shahidi huyo baada ya kukabidhiwa na Wakili Kibatala Kielelezo hicho ili amuulize maswali kutoka kwenye kielelezo hicho, aliieleza mahakama kuwa anafurahi Wakili huyo kumpatia taarifa hiyo, lakini akahoki akitaka wakili aeleze alikoipata akidai kuwa ni taarifa za ndani za Jeshi la Polisi.


Lakini Wakili Kibatala alimueleza kuwa hicho ni kielelezo cha mahakama kilichotolewa na askari mwenzake, kisha akaanza kumhoji maswali mbalimbali kuhusiana na taarifa zilizomo.


Baada ya shàhidi huyo kumaliza ushahidi wake ndipo kesho upande wa mashtaka ulipiwasilisha taatifa ya kumuongeza shàhidi huyo wa 24 Sajenti Obadia pamoja na kielelezo kingine Ili kupinga kielelezo cha awali.


Katika ushahidi wake  akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi Paul Kimweri, Sajenti Obadia alisema kuwa mwaka 2016 wakati tukio la mauaji ya Aneth linatokea alikuwa akifanya kazi Polisi makao makuu Dar es Salaam, kitengo cha kumbukumbu ya makosa ya jinai dhidi ya binadamu.


Majukumu yake yalikuwa ni kupokea taarifa zote za makosa ya jinai kutoka mikoa maalumu ya Kipolisi Dar es Salaam, yaani Kinondoni, Ilala na Temeke, na kwamba Mei 30, 2016  kutoka Mkoa wa Temeke.


Akilinganisha vielelezo hivyo viwili shahidi huyo alieeza kuwa kielelezo PE17 ndio nakala halisi aliyoipokea na kuitunza na ndio halali huku akisema kuwa kielelezo DE3, si halali kwa kwanza si ni nakala kivuli na si zao la kielelezo PE17.


Vilevile alidai kuwa hata baadhi ya taarifa zilizomo ndani ya nyaraka hizo mbili zinatofautiana ikiwa ni pamoja na mamna ya ujazaji wa taarifa hizo ndani ya fomu hiyo ya Polisi namba 4 (PF4).


Hata hivyo wakati akihojiwa na Ijumaa na Wakili Kibatala, shahidi huyo alikiri taarifa nyingi katika vielelezo vyote kufanana isipokuwa mambo machache kama vile namna ya kuandika namba ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO) Temeke, wenye DE3 kuandikwa Temeke lakini PE17 ni TMK.


Eneo lingine ni kuhusu watuhumiwa ambapo DE3 ilimtaja aliyekuwa mfanyakazi wa ndani wa kike wa marehemu Aneth, Getruda Peniel Mfuru wakati na tarehe ya kukamatwa wakati PE17 inaeleza kuwa hajulikani mlalamikaji ambapo kwenye DE3 ni Richard D. SP, wakati kwenye PE17 ni Richard Mwaisemba SP.


Ifuatayo ni sehemu ya maswali ya dodoso aliyoulizwa shahidi huyo leo katika kuhitimisha ushahidi wake, ikiwa ni mwendelezo wa maswali hayo aliyoulizwa kuanzia Ijumaa iliyopita:


Kibatala: Kibatala: Shahidi nakuonesha kielelezo DE3, kuna tarehe imeandikwa hapo ambayo ndio tarehe kilipokewa hapa mahakamani, isomee mahakama ni tarehe ngapi hiyo?


Shahidi: Tarehe 01/03/2023 Kibatala: Sasa nakuonesha kielelezo PE17, ambacho ulikitoa wewe hapa siku unatoa ushahidi, ilikuwa ni lini? Shahidi: Tarehe 8/9/2023


Kibatala: Ni baada ya muda gani tangu sisi tulipoleta kielelezo DE3 mpaka ninyi mlipotoa PE17? Shahidi: Karibu mwaka mmoja. Kibatala: Kwa hiyo unafahamu kwamba mlileta kielelezo PE17 mwaka mzima baada ya sisi kuleta DE3? Shahidi: Sijui


Kibataka: DE3 ni fomu namba ngapi? Shahidi: PF4 Kibatala: Na PE17 ni namba ngapi? Shahidi: PF4


Kibatala: Nimekusikia unasema hii (DE3) ni nakala kivuli, unafahamu kanuni za kuleta ushahidi huó mahakamani? Shahidi: Sifahamu Kibatala: Unafahamu kuwa hata nakala kivuli pia inaweza kutumika mahakamani kama ushahidi? Shahidi: Kama mahakama ikiona inafaa.


Kibatala: Unafahamu kanuni za kuleta kielelezo cha upande wa pili? Shahidi: Sifahamu Kibatala: Unafahamu nakala halisi ya DE3 nani anayo? Shahidi: Sifahamu.


Kibatala: Ulijitambulisha kuwa mwaka 2016 ulikuwa ofisi ya DCI (Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai) kitengo cha kupokea kumbukumbu, una uthibitisho gani wa hilo ulioipa mahakama kuwa 2016 ulikuwa hiyo sehemu?  Shahidi: Kuna kitabu huwa tunaandika, kiko ofisini lakini pia mabosi zangu wapo.


Kibatala: Ahaa kumbe kuna kitabu lakini hujakileta hapa pengine ni kizito sana. Sasa soma kielelezo DE3, sehemu iliyoandikwa other difficulties. Shahidi: Mheshimiwa Jaji pameandikwa bado hatujapata taarifa ya Dr sijui alimaanisha dokta au nini, na Mkemia Mkuu. Kibatala: Ni tarehe ngapi ya kuingiza hizo taarifa? Shahidi: Tarehe 26/5/2016


Kibatala: Saa ngapi? Shahidi: Saa 12:10 asubuhi Wakili Nehemiah Nkoko:  Shahidi hebu angalia vielelezo vyote viwili utakubaliana maelezo mengi yanafanana? Shahidi: Hapana, ni baadhi tu


Nkoko: Hebu iambie mahakama hicho kielelezo ambacho unakijua (PE17) ni lini uliwahi kukifanyia kazi wewe mwenyewe kwa kuiandika? Shahidi: Hilo swali niliulizwa hata Ijumaa, sijakiandika mimi. Nkoko: Kwa hiyo utakubaliana nami wewe huna uhusiano na hicho kilelezo maana hujakiandaa?


Shahidi: Kwa maana ya kukiandaa uko sahihi lakini nina uhusiano nacho maana nilikipokea na kukitunza. Nkoko: Utakubaliana nani wewe huwezi kukizungumzia hicho kielelezo maana hukuwepo wakati hizo taarifa zinaandaliwa? Shahidi: Si kweli?


Nkoko: Wewe unajua hizo taarifa zilipatikanaje? Shahidi: Ndio Nkoko: Ulikuwepo Kigamboni? Shahidi: Hapana


Nkoko: Unajua hizo taarifa zilipatikanaje? Shahidi: Wakili hii ni waraka wa  Polisi Nkoko: Kwa hiyo ulizifahamu.kwa kuisoma hiyo taarifa? Shahidi: Hapana, siyo kwa kusoma tu maana nilihusika nayo.


Nkoko: Utakubaliana nami vielelezo hivyo vyote vinamuongelea mtu mmoja ambaye ni Mwaisemba? Shahidi: Hapana Nkoko: Hebu zisome zote kipengele cha complainant Shahidi: Kielelezo DE3 kineandikwa Richard D. SP na kielelezo PE 17 kineandikwa Richard Mwaisemba SP. Nkoko: Utakubaliana nami huyu Richard Mwaisemba kipindi hicho ndiye alikuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kigamboni? Shahidi: Ni kweli


Nkoko: Utakubaliana nami Richard Mwaisemba pekee ndio yuko kwenye position (nafasi) nzuri ya kuziongelea hizo nyaraka kuwa ipi ni ya kweli na ipi si ya kweli? Shahidi: Naifahamu hii moja tu ambayo aliijaza ambayo niliiipokea Nkoko: Wewe na Mwaisemba nani bosi kwa mwingine? Shahidi: Mwaisemba ni bosi wangi


Nkoko: Unaufahamu mwandiko wa Mwaisemba? Shahidi: Siufahamu Nkoko: Kwa hiyo PE17 wewe huwezi kusema kama ndiye aliyeijaza au la? Shahidi: Siwezi kusema lakini kwa mujibu wa utaratibu yeye haijazi. Nkoko: 2016 wewe ulikuwa wapi?


Shahidi: Nimeshasema nilikuwa makao makuu Nkoko: Kwa hiyo yaliyotokea Kigamboni wewe huyajui? Shahidi: Kimya.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad