Dar es Salaam. Aliyekuwa mfanyakazi wa kazi ndani (house girl), wa marehemu Aneth Elisaria Msuya, hatimaye leo ameanza kutoa ushahidi wake katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwajiri wake.
Shahidi huyo Getruda Peniel Mfuru (38), mama wa watoto watatu, amepanda kizimbani kutoa ushahidi wake leo Septemba 13, 2023, ambapo pamoja na mambo mengine, ameelezea sehemu ya matukio yaliyojiri kabla ya mauaji ya mwajiri wake huyo.
Washtakiwa katika kesi hiyo namba 103 /2018 ni Miriam Steven Mrita ambaye ni mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara tajiri na maarufu wa madini mkoani Arusha, marehemu Erasto Msuya, maarufu kama Bilionea Msuya; na mwenzake Revocatus Everist Muyella maarufu Ray.
Aneth ambaye aliuawa Mei 26, 2016 kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, wilayani Temeke (wakati huo), jijini Dar es Salaam, alikuwa mdogo wa Bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi eneo la Mijohoroni, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, Agosti 7, 2013.
Ushahidi wake
Getruda ametoa ushahidi kwake akiwa shahidi wa 25 wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Katika ushahidi wake akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Paul Kimweri, kwanza alijitambulisha kuwa kwa sasa anajishughulisha na kilimo cha mbogamboga na ufugaji kuku na mbuzi Kijijini kwao Masama Sonu, Wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa maelezo yake Getruda ambaye ni mzaliwa wa pili kati ya watoto watatu katika familia yao, baada ya kuhitimu elimu ya kidato cha nne aliyoipata Shule ya Olorien Arusha mwaka 2005, hakufanikiwa kuendelea na masomo zaidi.
Hivyo alirudi nyumbani kwao kijijini Masama Sonu, lakini akaenda kuishi na bibi yake, aitwaye Shikalisandee Lema kwa kuwa baba na mama yake walifarakana.
Mwaka 2007 alipata mtoto wake wa kwanza baadaye akapata watoto wengine wawili, wa pili 2009 na wa tatu 2013, lakini kwa sasa wamebaki wawili kwa kuwa mmoja alishafariki dunia.
Mwaka 2015 aliamua kutafuta kazi za ndani na alikutana na mama mmoja aitwaye mama Manka ambaye baada ya kumweleza hitaji lake alimweleza kuwa kuna mama mmoja anaishi Cairo Mererani, anaitwa bibi Msuya anatafuta msichana wa kazi.
Hivyo mama Manka alimuunganisha na bibi Msuya baada ya kumpatia bibi Msuya namba zake na kisha bibi Msuya akampigia (Getruda).
Baada ya mazungumzo bibi Msuya alimtumia Sh10, 000 kupitia M-pesa kuwa ya nauli ya kwenda kwake Cairo Mererani.
Hivyo Februari 15, 2015 alisafiri kwenda kwa bibi Msuya huko Mererani, ambako walikubaliana kufanya kazi kwa malipo ya Sh40, 000 kwa mwezi. Mbali na yeye, walikuwepo wafanyakazi wengine watatu wa kike.
Alifanyakazi hapo mpaka Agosti 28, 2015, alipoondoka kurudi nyumbani kwa bibi yake Masama Sonu, kuangalia watoto wake.
Kwa muda alioishi kwa bibi Msuya, alifanikiwa kuwaona watoto wake wanne, Antuja, Bahati, Joyce na Aneth.
Baada ya kurudi kwa bibi yake hiyo Desemba 2015, bibi Msuya alimpigia simu akamweleza kuwa mtoto wake Aneth, anahitaji mfanyakazi na yeye Getruda akasema anaweza kwenda, hivyo bibi Msuya akamwambia asubiri amuunganishe na Aneth aliyekuwa akiishi Dar es Salaam.
Aneth alimpigia simu na baada ya mazungumzo, alimtumia Sh22, 000 kwa ajili ya nauli. Sh10, 000 alimwachia bibi yake na Sh10, 000 nyingine alitumia kama nauli ya kwenda kwa bibi Msuya huko Mererani Cairo.
Alifika Cairo Mererani kwa bibi Msuya, Desemba 25, 2015 na alikaa mpaka Januari 4, 2016; na tarehe ambayo aliondoka na Antuja, dada wa Aneth kwenda Kigamboni Dar Es Salaam kwa Aneth Msuya.
Alipofika kwa Aneth, Kigamboni alielezwa na Aneth majukumu ya kazi na wakakubaliana mshahara wa Sh60, 000 kwa mwezi. Pia Aneth alimuahidi kuwa ikifika mwezi Juni 2016 angemuongezea mshahara.
Hivyo alianza kazi na maisha katika familia ya Aneth iliyokuwa ni ya watu watatu, Aneth mwenyewe, mtoto wake Allan na yeye mwenyewe Getruda.
Kwa muda aliokaa pale hakuwahi kumuona rafiki au mume wa Aneth pale nyumbani isipokuwa Aneth aliishia kumuonesha mumewe kwenye picha tu.
Wakati wote waliishi maisha ya furaha na amani na hata mahusiano ya Aneth na majirani zake walikuwa wakiishi vizuri kwa kusikilizana.
Mei 15, 2016 majira ya mchana alitokea geti la nyuma ya nyumba hiyo kwenda dukani kununua toilet paper, njiani alikutana na gari la dark blue.
Kioo cha nyuma cha pili kutoka kwa dereva wa gari hilo, kilishushwa na akamuona mama mmoja aliyevaa suti ya bluu singlend nyeusi na shingoni alikuwa amevaa cheni mbili moja kubwa moja nyembamba zenye mwonekano wa dhahabu na hereni za dhahabu.
Alikuwa ni mwenye uso wa mviringo na alikuwa amesuka nywele za kitimutimu.
Yule mama alimwambia samahani, anaomba kuongea naye, naye akamjibu kuwa bila samahani kisha akamfuata.
Alipofika kwenye ile gari aligundua kuna mtu mwingine wa kiume, alikuwa upande wa dereva wa hiyo gari.
Yule mama alimuuliza kama anapajua kwa Aneth Msuya naye akajibu kuwa ndio anapajua. Kisha akimuonesha kwa ishara ya kidole nyumba na akamwambia kuwa anaishi naye ni dada yake.
Yule mama alisema ni ndugu yake (Aneth) na kwamba ana siku nyingi hajamuona lakini akamwambia kuwa wataonana keshokutwa, Mei 17, 2016. Siku hiyo Mei 15, Aneth alikuwa kazini.
Mei 18, 2016 majira ya saa 4 asubuhi alipotoka kuchota maji alimkuta huyo mama wamesima nje ya geti akiwa na yule mwanaume aliyekuwa naye kwenye gari Mei 15.
Siku hiyo yule mama alikuwa amevaa suti ya cream, viatu vya purple, cheni kubwa mbili, na hereni na kichwani alikuwa amesuka weaving.
Chini alikuwa amevaa sketi fupi ya suti na miguu yake haikuwa nyembamba na juu alikuwa mnene
Yule mwanaume alikuwa amevaa suti nyeusi, shati jekundu, viatu vyeupe, miwani juu ya paji la uso. Kwa umbo alikuwa mrefu wa kati, mnene wa kati na mweusi.
Yule mama alipomuita ilibidi arudishe ndoo ndani akafunga geti kisha akawafuata, lakini iliporudi aliwakuta wameshaingia kwenye gari ya kifahari aina ya Rangerover yenye rangi ya Silver waliyokuwa nayo.
Alipofika yule mama alimtaka aingie kwenye gari na alipoingia alikuta watu watatu na yeye akawa wa nne. Kulikuwa na mwanaume mwingine ndani ya gari. Alikuwa amevaa tshirt nyekundu na suruali ya Jeans ya bluu.
Ndani ya gari alikaa katikati ya yule mama na yule kijana mwingine mwenye t-shirt ya bluu na yule mama alichukua pochi akafungua upande wa zipu ndogo akatoa simu aina ya Nokia ndogo, akampa.
Alimwambia ashike hiyo simu watakuwa wanawasiliana naye mara na asiwasiliane na mtu mwingine yeyote na kwamba wakijua kuwa anawasiliana na mtu mwingine yeyote watamuwajibisha.
Yule mama aliongea na dereva, "mali nitafute mimi na mume wangu wengine wanazihangaikia za nini?"
Yule mwaume alimjibu kwa kuguna, "mmmh,” kisha akasema hao ni wapumbavu tu.
Yeye Getruda alimuuliza yule mama hiyo simu ni ya nini na yule mama akamjibu kuwa watakuwa wanawasiliana mara kwa mara.
Yule mwanaume wa t-shirt nyekundu alichukua bastola akamuwekea shingoni upande wa kushoto.
"Nilijisikia vibaya na kuingiwa na hofu kubwa sana," alisema Getruda.
Simu ile aliyopewa ilikuwa na mtandao wa Airtel lakini namba zake hakuzishika kichwani.
Baada ya kumpatia hiyo simu pia walimwambia kuwa wana kazi na Aneth, alipomuuliza yule mama kuwa ni kazi gani hiyo alimjibu kuwa yeye haimhusu.
Kisha yule mama alimuuliza kama anapafahamu nyumbani kwa kina Aneth Msuya, yeye akajibu kuwa hapana. Yule mama akamuuliza kama anamfahamu yeye akajibu hapana kisha akamuuliza yeye anatokea wapi? Akamjibu Machame Hospitali.
Alimjibu hivyo kuwa hapafahamu kwao Aneth kwa sababu tayari walikuwa wameshamtishia kwa bastola shingoni.
Wakati anamuuliza hayo maswali, alivuta kumbukumbu kuwa aliwahi kumuona wapi na akakumbuka kuwa wakati anafanya kazi kwa bibi Msuya, waliwahi kwenda na bibi Msuya akatambulishwa na bibi na babu Msuya kuwa huyo ni mke wa marehemu Erasto, aliyekuwa mtoto wao.
Baada ya hapo yule mama na mwanaume aliyekuwa amevaa suti nyeusi waliongea kwa lugha ambayo hakuweza kufahamu walichokuwa wanaiongea.
Kisha alishuka kwenye gari na kuelekea nyumbani na wale waliokuwa kwenye gari waliondoka kuelekea barabara kuu.
Alipoingia ndani (ya geti) alizima ile simu, akaificha kwenye kochi dogo ambalo lilikiwa nje barazani lililokuwa halitumiki, ili Aneth asisikie akiwasiliana na mtu mwingine yeyote yule.
Kesho yake (Mei 19) Aneth alipoondoka kwenda kazini yeye aliiwasha ile simu.
Hakuweza kumueleza Aneth chochote kuhusu matukio hayo kwa madai kuwa vitisho vile alivyopewa aliogopa sana na alikuwa na hofu.
Mei 23 2016 akiwa nyumbani alipigiwa simu na yule mama katika simu ile aliyopewa, akamwambia kuwa waonane nje. Alitoka akawakuta mbele ya nyumba lakini yule mama akamuomba wasogee pembeni kidogo. Walikuwa na ile gari ya Rangerover ya rangi ya Silver.
Alipofika alichungulia ndani ya gari yule mama akamwambia aingie ndani ya gari.
Kesi hiyo itaendelea kesho ambapo shahidi huyo ataendelea na sehemu ya pili ya simulizi yake kabla ya kuwekwa katika kiaango cha maswali ya dodoso kutoka kwa mawakili wa utetezi, Peter Kibatala na Nehemiah Nkoko.