Wakati Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi akitamba kwa sasa mchezaji yoyote kwenye kikosi chake anaweza kufunga mabao, timu hiyo inaonyesha makali zaidi katika kipindi cha pili cha kila mechi, imefahamika.
Yanga iliendelea kutoa vichapo katika Ligi Kuu Bara baada ya kuichapa JKT Tanzania mabao 5-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam usiku, huku wafungaji wakiwa ni Stephenie Aziz Ki, Kennedy Musonda, Kouassi Yao na Maxi Nzengeli aliyepachika mawili.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wanaonekana bora zaidi katika kipindi cha pili, rekodi inaonyesha wamepachika wavuni mabao 12 kati ya 17 kwenye kipindi hicho ndani ya michezo minne iliyocheza mpaka sasa.
Ushindi wa mabao 5-0 walioupata ilipocheza dhidi ya JKT Tanzania katika mechi ya Ligi Kuu Bara juzi usiku, imekamilisha idadi ya mabao nane kati ya 10 ya kipindi cha pili katika mechi zake mbili za Ligi Kuu Bara.
Kwa mujibu wa dawati la takwimu la TanzaniaWeb, Yanga imecheza mechi nne mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Ali Sabieh ASAS na mbili za Ligi Kuu dhidi ya KMC na JKT Tanzania, imefunga jumla ya mabao 17, lakini mabao 12 yakiwekwa kimiani katika kipindi cha pili.
Katika mechi za Ligi Kuu ni mabao mawili tu kati ya 10 ambayo yamefungwa kipindi cha kwanza, ambayo yamefungwa na Dickon Job dakika ya 16 kwenye mechi dhidi ya KMC ikimaliza kwa ushindi wa magoli 5-0, na juzi la Stephane Aziz Ki dakika ya 45 dhidi ya JKT Tanzania.
Mabao manne katika kila mechi yalifungwa kipindi cha pili, Aziz Ki akifunga dakika ya 58, Hafiz Konkoni (69), Mudathir Yahya (75) na Pacome Zouzoua (80) katika mechi dhidi ya KMC, na Kennedy Musonda (54), Yao Kouassi (64), na Maxi Nzengeli (79) na 88 katika mchezo dhidi ya JKT Tanzania.
Mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika hat ua ya awali ambapo ilicheza dhidi ya ASAS Djibouti FC, imefunga mabao manne kati ya saba katika kipindi cha pili.
Agosti 20, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex iliichapa ASAS mabao 2-0, moja likifungwa kipindi cha kwanza na Aziz Ki dakika ya 22 na Musonda kipindi cha pili dakika ya 53.
Mechi ya marudiano Agosti 26, mwaka huu iliposhinda mabao 5-1, magoli mawili yalifungwa kipindi cha kwanza na matatu yalifungwa kipindi cha pili kupitia kwa Pacome dakika ya 51, Mzize (68) na Nzengeli (90).
Yanga sasa ndio vinara katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya kwanza ikiwa na pointi sita sawa na Azam FC na Simba, lakini yenyewe ikiwa na idadi kubwa ya mabao ya kufunga.
Kikosi hicho cha Jangwani kimefunga mabao 10 katika mechi mbili, Azam inafuata katika msimamo ikiwa na magoli saba na Simba iko katika nafasi ya tatu.
Akizungumza nasi baada ya kufunga mabao 10 katika mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara alizocheza, Gamondi aliweka wazi kila mchezaji wa Yanga anaweza kufunga mabao ambayo yataisaidia timu hiyo kufikia malengo.
Gamondi alisema anahitaji kuona kila mchezaji ndani ya timu hiyo anafunga pale nafasi ya kufanya hivyo inapopatikana na hiyo itasaidia kuwaimarisha kufanya vizuri katika kila mechi.
Kocha huyo alisema ili kuachana na hali ya kutegemea washambuliaji peke yake, amebadilisha mfumo alioukuta na anataka kuona kila mchezaji aliyekuwa kwenye nafasi ya kufunga anatumia vyema nafasi wanazotengeneza.
“Hatuwezi kuwategemea washambuliaji pekee kutufungia mabao, nimebadili mfumo na kuwataka wachezaji wangu kila aliyekuwa katika nafasi basi anauwezo wa kufunga.
Ukiangalia katika mchezo ule wa JKT Tanzania kipindi cha kwanza walicheza kwa kuzuia lakini tulipofanikiwa kupata bao la kwanza kupitia kwa Aziz Ki tulitengeneza hali ya kujiamini na kupambana kuelekea katika kipindi cha pili ambacho tulifanikiwa kufunga magoli zaidi,” alisema Gamondi.
Aliongeza mchezo ulikuwa wa ushindani mkubwa kwa sababu wapinzani wao (JKT Tanzania) walivyokuwa wanacheza kabla ya kuanza kupata bao la kwanza na baada ya bao la kwanza nyota wake walijiamini na kutengeneza nafasi na kufanikisha kile alichokifanya mazoezini.
Kiungo wa Yanga, Khalid Aucho, alisema siri kubwa ya kufanikiwa kufunga mabao matano katika kila mechi ni kufuata maelekezo ya benchi la ufundi na wachezaji kuonyesha kiwango kizuri kwa kutumia nafasi wanazotengeneza.
“Ni kweli tumefanikiwa kufunga mabao 10 katika mechi mbili za ligi, magoli matano katika mechi ya marudiano ya kimataifa, haya ni mafanikio ya kocha kuhitaji kuona kila mchezaji anacheza mpira na kufuata maelekezo na kutumia vizuri kila nafasi tunazotengeneza, na yoyote aliyekuwa kwenye nafasi anafunga,” alisema Aucho.