Kocha Taifa Stars Awahakikishia Watanzania Kufuzu AFCON 2023

 

Kocha Taifa Stars Awahakikishia Watanzania Kufuzu AFCON 2023

Kocha Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania Taifa Stars’, Adel Amrouche amesema matumaini ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika AFCON 2023, ni makubwa kutokana na utayari unaooneshwa na wachezaji wake kwenye kambi ya mazoezi nchini Tunisia.


Taifa Stars iliyopo nafasi ya pili kwenye Kundi F, imejichimbia nchini Tunisia kujiandaa na mchezo wa marudiano dhidi ya vinara wa kundi hilo Algeria, mchezo unaotarajiwa kuchezwa Alhamisi ya wiki hii nchini Algeria.


Katika mchezo huo, Taifa Stars yenye pointi saba inahitaji kushinda au sare ili kupata nafasi ya kushiriki fainali hizo za Afrika kwa mara ya tatu ambazo zinatarajia kufanyika nchini Ivory Coast mapema mwaka 2024.

Akizungumza kupitia Mtandao wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Amrouche alisema tangu wamefika Tunisia wachezaji wameonesha juhudi kubwa za kujituma mazoezini na kufuata kile anacho waelekeza kitu ambacho kinampa matumaini ya kushinda mchezo huo bila kujali ubora waliokuwa nao wapinzani wao.


“Nina imani tutashinda na kufuzu AFCON ya mwakani, tuna kikosi kizuri lakini wachezaji wameonesha uzalendo kuipigania nchi yao tusubiri siku ya mchezo, lakini matumaini yangu na wenzangu wa benchi la ufundi ni makubwa,” amesema Amrouche.


Kocha huyo amesema tangu wamefika Tunisia wamekuwa wakifanya mazoezi ya mbinu zaidi pamoja na Gym lengo ni kuhakikisha wanacheza kwa mkakati na mipango na kutengeneza nafasi ambazo anaamini watazitumia vizuri kutokana na ubora wa safu yake ya ushambuliaji.

Amesema anawajua wapinzani wao Algeria wana wachezaji wazuri wenye uzoefu wanawaheshimu kwa hilo, lakini hata wao wana mkusanyiko wa wachezaji wenye uzoefu na mashindano ya kimataifa ndio maana anaamini watawashangaza watu kwenye mchezo huo.


Wakati Tanzania inacheza na Algeria Alhamisi washiriki wengine wa kundi hilo Niger watakuwa nyumbani kucheza na Uganda, na endapo Taifa Stars itapata hata sare itafikisha pointi nane ambazo hazitoweza kufikiwa na Uganda iliyopo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi hilo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad