WAKATI Yanga ikijiandaa kusafiri kwenda Kigali kwa ajili ya mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh ya Sudan, kiungo wa zamani wa Simba, Shekhan Rashid amembebesha mzigo mzito winga wa Yanga, Maxi Nzengeli akiamini akishirikiana na wenzake wataivusha timu makundi.
Maxi aliyefunga mabao mawili kwenye mechi mbili za raundi ya kwanza dhidi ya Asas ya Djibouti, alijiunga na Yanga msimu huu akitokea AS Maniema Union ya DR Congo na amekuwa akiwakosha mashabiki wa klabu hiyo kwa soka tamu, kasi na mabao aliyofunga hadi sasa kwenye mechi sita za mashindano.
Tangu atue kwenye timu hiyo, Maxi anayemudu kucheza wingi ya kulia, kushoto na kiungo mshambuliaji, amekuwa lulu katika kikosi cha kocha Miguel Gamondi na hilo limemfanya Shekhan aliyewahi kuzichezea pia Friends Rangers, Kilimani Zanzibar, Mji Mpwapwa na Singida United na Azam FC kushindwa kujizuia.
Shekhan anayeishi kwa sasa Sweden alisema ubora alionao Mkongomani huyo, ni wazi Yanga imelamba dume kwani amekuwa mhimili muhimu kwenye kikosi hicho akiwa na uwezo mkubwa wa kupiga pasi kwa usahihi na kwa wakati muafaka na anaamini ndiye atakayeibeba kwenye mechi mbili za Al Merrikh ya Sudan.
“Unajua kwenye soka ogopa sana mchezaji ambaye anajua kupiga pasi sahihi tena kwa wakati na mwenye uwezo wa kutembea eneo kubwa la uwanja kwa nguvu ile ile. Maxi ni karata dume, usajili mzuri sana uwepo wake utaongeza nafasi ya Yanga kufanya vizuri zaidi msimu huu,” alisema Shekhan na kuongeza;
“Naona anaenda kuwa mtawala mpya ndani ya Yanga, ana kila kitu cha kumfanya awe nyota wa timu ya Yanga kwa msimu huu kwa sababu hana uchoyo wa pasi na ana jicho zuri la pasi za mwisho, hivyo ni wazi anapaswa kuibeba timu akishirikiana na wenzake, Yanga iende hatua ya makundi kwa mara nyingine.”
Yanga ilicheza makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara ya mwisho mwaka 1998 na kwa miaka 25 imekuwa ikisota kuingia, japo 2016 na 2018 ilicheza makundi ya Shirikisho Afrika na msimu uliopita ilienda hadi fainali ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya klabu Afrika na kulikosa taji mbele ya USM Alger ya Algeria kwa faida ya mabao mengi ya ugenini.
Shabiki wa timu hiyo, Deogratias Steven ‘Deo Toto’ alisema winga huyo ni jembe la kazi kwani ameipa heshima timu yao na kuwaondolea hofu mashabiki baada ya kuondokewa na baadhi ya mastaa wao, huku akitamba kuwa Wasudani (Al-Marrekh) wajiandae kwani timu yao inakwenda kuwapiga nje ndani.