Mahakama yafunga mjadala Rais kumuongezea muda Jaji Mkuu



Dar es Salaam. Mahakama Kuu nchini imefunga mjadala wa uhalali wa Rais Samia Suluhu Hassan kumuongezea Jaji Mkuu Profesa Ibrahimu Juma muda wa utumishi wa wadhifa huo baada ya kutupilia mbali kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Mwanasheria, akipinga uamuzi huo wa Rais.

 Uamuzi huo umetolewa jana Ijumaa, Septemba 22, 2023 na Jaji Godfrey Isaya aliyesikiliza kesi hiyo, ambaye amesema kuwa hoja za mwombaji katika shauri hilo hazina mashiko ya kisheria na kwamba uamuzi huo wa kumuongezea muda Profesa Juma ni halali.

“Baada ya hayo ninatupilia mbali shauri hili kwa kutokuwa na ustahilifu,” amesema Jaji Isaya baada ya kupitia hoja zilizowasilishwa na mawakili wa pande zote na kuzichanganua huku akirejea ibara za zilizokuwa zinabishaniwa, kesi mbalimbali zenye maudhui yanayofafana na kesi hiyo nchini na nje ya nchi.

Kesi hiyo ilifunguliwa na wakili wa kujitegemea Humphrey Simon Malenga, Mahakama Kuu Masjala Kuu, siku chache baada ya Jaji wa Mahakama ya Rufani, Stella Mugasha kumwandikia barua Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisanye Ole Gabriel kupinga uamuzi huo wa Rais kumuongezea muda Profesa Juma.


Profesa Juma, ambaye alizaliwa Juni 15, 1958 amekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania kwa miaka mitano na miezi tisa kuanzia  Septemba 10, 2017, alimaliza utumishi wake kwa nafasi hiyo Juni 15, 2023 baada ya kufikisha umri wa miaka 65, kwa mujibu wa Katiba.

Hata hivyo Rais Samia alimwongezea muda wa kuelendelea na utumishi katika nafasi hiyo kwa mua ambao hata hivyo bado haujawekwa wazi.

Taarifa za Rais kumwongezea muda Profesa Juma ziliianza kusambaa na kuibua mjadala mkali baada ya kuvuja kwa barua hiyo ya Jaji Mugasha katika mitandao ya kijamii.


Katika barua hiyo iliyovuja na kusambaa katika mitandao ya kijamii, Jaji Mugasha ambaye alilithibitishia Mwananchi kuandika barua hiyo, alikuwa anapinga uamuzi huo wa Rais kuwa ni ukiukwaji wa Katiba ya Nchi.

Barua na msimamo huo wa Jaji Mugasha uliibua mjadala mkali wa kisheria huku kukiwa na mitazamo ya aina mbili inayokinzana hata miongoni jamii ya wanataaluma ya sheria, huu wengine wakisema kuwa uamuzi huo ni ukiukwaji wa Katiba na wengine wakisema ni halali.

Katikati ya mjadala huo ndipo Juni 28, 2023 mwanasheria huyo akachukua hatua zaidi akifuata mkondo wa sheria kwa kufungua shauri hilo akiiomba mahakama hiyo itoe tafsiri ya Ibara za Katiba zinazozungumzia uamri wa Jaji Mkuu kustaafu.

Katika shauri hilo namba 7 la mwaka 2023, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Malenga anaiomba mahakama itoe tafsiri ya ibara za Katiba kuhusiana na mamlaka ya Rais kuahirisha au kuongeza umri wa kustaafu wa utumishi wa Jaji Mkuu.


Ibara hizo ambazo Malenga alikuwa anaiomba mahakama hiyo iziotolee tafsiri ni ibara ya 118(2) na 120 (2) na (3).

Ibara ya 118(2) inaeleza kuwa Jaji Mkuu ambaye ni mkuu wa Mahakama ya Rufani na wa Mhimili wa Mahakama  kwa ujumla atatumikia wadhifa huo mpaka atakapotimiza umri wa kustaafu wa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Ibara ya 120 (2) na (3) inabainisha kuwa umri wa kustaafu wa Jaji wa Mahakama wa Rufani ni miaka 65, lakini inabainisha kuwa Rais akiona inafaa anaweza kumuongezea muda maalumu mpaka mwisho wa muda huo wa nyongeza utakapoisha.

Ibara 120(4) inafafanua kuwa pia Jaji wa Mahakama ya Rufani anaweza kuendelea na majukumu yake hata baada ya kufikisha umri wa miaka 65 mpaka pale atakapokamilisha kuandaa na kutoa hukumu za mashauri kesi alizozisikiliza au shughuli au mashauri aliyokwishaanza kuyasikiliza.


Hivyo kiini cha mjadala ulikuwa ni kama masharti ya ibara 120(2) (3) kuhusu jaji wa Mahakama ya Rufani kuongezewa muda wa utumishi na Rais inasomwa pamoja na ibara ya 118(2), kwamba masharti hayo yanamhusu pia Jaji Mkuu au la.

Kwa mujibu wa Jaji Mugasha, Ibara ya 118(2) inayohusu umri wa kustaafu wa Jaji Mkuu, ambao ni sawa na jaji mwingine wa kawaida wa Mahakama ya Rufani (miaka 65), inasimama pekee yake wala haihusiani na ibara ya 120(2) na (3).

Kutokana na mjadala huo Malenga katika kesi hiyo alikuwa anaiomba mahakama hiyo itoe tafsiri masharti ya Ibara ya 118(2) kuhusiana na umri wa kustaafu wa Jaji Mkuu kwamba ni miaka 65 na si umri wa kustaafu wa jaji wa kawaida wa Mahakama ya Rufani.

Aliiomba pia mahakama hiyo itoe tafsiri kwamba Ibara ya 118(2) ni ibara inayosimama peke yake, haihusiani na Ibara ya 120(1), (2), (3) na (4) katika kuamua umri wa kustaafu utumishi wa Jaji Mkuu.

Vilevile aliiomba mahakama itafsiri kwamba mamlaka ya Rais kuzuia kustaafu au kumuongezea muda wa utumishi jaji wa Mahakama ya Rufani kwa maslahi ya umma kwa mujibu wa ibara hiyo ya 120(2) na (3) hayatumiki kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Jaji Mkuu.


Mwisho aliiomba itamke kwamba kuahirishwa kwa umri wa kustaafu au kuongezewa muda wa utumishi wa Jaji wa Mahakama ya Rufani wa sasa, ambaye pia ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Juma kwa mujibu wa Ibara ya 120(2) na au 120(3), ni kinyume cha Katiba.

Katika kesi hiyo iliyosikilizwa kwa njia ya maandishi, Malenga aliwakilishwa na jopo la mawakili watatu, Ipilinga Panya, Aliko Mwamanenge na Joyce Brown, na Serikali siku ya kutajwa iliwakilishwa na mawakili wa Serikali Alice Mturo na Bravoo Junus.

Hata hivyo Jaji Isaya katika uamuzi wake amesema kuwa haoni kama 118(2) ni Ibara inayoweza kusimama yenyewe pekee au kujitegemea kwa kuwa inarejea 120(1) na kwamba ili kupata umri wa kustaafu Jaji Mkuu lazima kushirikisha pia na Ibara ya 120(1).

Amesema kwamba Mahakama inaridhika kwamba Ibara ya 120(1) inahusiana na ibara nyingine na kwamba katika kuzitafsiri zinapaswa zitafsiriwe kwa kuzihusianisha na kuzishirikisha.

“Kwa hiyo baada ya kutafakari ninaona kwamba Ibara ya 118(2) na 120(1) zina uhusiano na hivyo Jaji Mkuu lazima pia awe JA. Kama watunga Katiba walikusudia kusema kwamba Jaji Mkuu hahusiki (na nafuu zinazotolewa katika Ibara ya 120(1) basi wangesema kwa dhahiri kabisa”, amesema Jaji Isaya.

Amefafanua zaidi kuwa Ibara ya 120(1) inasomwa pamoja na Ibara ndogo mpaka (2-4), na kwamba kwa hiyo Ibara 120(1) na ibara nyingine zote zinamhusu pia Jaji Mkuu kama walivyo majaji wengine wa Mahakama ya Rufani.

Akizungumzia uamuzi huo, wakili Panya wameupokea uamuzi wa mahakama hivyo watakwenda kukaa na mteja wao waone kama atakuwa ameridhika na baada ya kupitia uamuzi mzima wataona kama kuna haja ya kulipeleka suala hilo Mahakama ya Rufani.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad