Paroko wa Parokia Teule ya Mtakatifu Dionis Arobagita ya Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi, Padri Sosthenes Bahati au Soka (42) ameruka kihunzi cha kwanza baada ya kushinda kesi iliyokuwa ikimkabili ya kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 12.
Kuachiwa huru kwa Padri huyo ambaye kwa sasa amesimamishwa kutoa huduma zote za kipadri, kunamfanya abakiwe na kesi mbili za tuhuma za kubaka watoto wa mafundisho ya Kipaimara, matukio yanayodaiwa kutendeka kwa nyakati tofauti.
Padri Soka alikamatwa na Polisi Septemba 20, 2022 na alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani Septemba 26, 2022 na kufunguliwa kesi tatu tofauti za kubaka watoto watatu zilizosomwa kwa mahakimu watatu tofauti.
Baada ya hukumu ya kumuachia huru iliyotolewa jana na Hakimu Mkazi, Jenipha Edward aliyekuwa akiisikiliza, mama mzazi wa mtoto huyo alitoka nje na kuangua kilio, baadaye alianguka na kupoteza fahamu.
Wakati mama huyo akizirai kutokana na hukumu hiyo, Padri Soka baada ya kuachiwa huru alitoka nje ya chumba cha Mahakama na kuwakuta waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari waliofika kufuatilia mwenendo wa hukumu hiyo wakimsubiri, lakini alijifunika uso kwa kofia ya sweta, akapanda gari na kuondoka.
Mara baada ya kuondoka kwa padri huyo na baadhi ya watu waliokuwapo mahakamani hapo, mama aliyezirai alipepewa na wenzake na baada ya kuzinduka alishika Rozari na kusali akisema:
“Mungu nimechoka, nilikueleza shida zangu, Mungu simama na mimi, Mungu simama na hao walioko nyuma yangu, Mungu nisaidie, Mungu tazama madhabahu yako,” baada ya maneno hayo alizirai tena.
Hukumu ilivyokuwa
Akisoma hukumu ya shauri hilo, hakimu Edward alisema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shitaka pasipo kuacha shaka yoyote kwa sababu upande wa utetezi wameibua mashaka yaliyokosa majibu kutoka kwa mashahidi upande wa mashtaka.
Hoja nyingine ambayo imezingatiwa na Mahakama ni kwamba, ushahidi wa mwathirika (mtoto) umeibua mashaka juu ya ukweli wa kile alichokiongea mahakamani kwa sababu unatofautiana na wa mashahidi wengine.
“Lakini pia upande wa utetezi uliibua hoja ya mshtakiwa kutokuwapo eneo la tukio katika tarehe husika ambayo ni Agosti 26, 2022 na Septemba 9, 2022 ambapo walitoa notisi juu ya hilo na kuleta mashahidi wa kuthibitisha,” alisema.
Hakimu katika hukumu hiyo alisema: “Kulikuwa na tofauti ya ushahidi wake mwenyewe alioutoa mahakamani, lakini pia kulikuwa na tofauti baina ya ushahidi wake na mashahidi wa mashtaka na kulikuwa na tofauti baina ya ushahidi wake na maelezo aliyotoa polisi.”
Akichambua ushahidi huo, Hakimu Jenipha alisema upande wa mashtaka pia ulishindwa kuleta mashahidi muhimu wa kuthibitisha kama tarehe hizo mshtakiwa alikuwepo eneo la tukio na kama kweli muathirika naye alikuwepo.
“Kwa sababu mashaka yalishaibuliwa na upande wa utetezi kuwa tarehe iliyotajwa si siku ya shirika, ambapo tarehe zilizotajwa ni siku za Ijumaa na kutokana na ushahidi walioleta siku za mafundisho na shirika ni Jumamosi,” alisema.
Hakimu alisema hayo yameibua mashaka kama kweli tukio lilitokea siku hiyo ambayo imetajwa.
Akizungumza na wanahabari nje ya mahakama, wakili Edwin Silayo aliyemtetea mshtakiwa alisema wamefurahia hukumu hiyo.
Hii inaweza kuwa siku ya furaha kwa Padri Soka, kwa kuwa amesimamishwa kutoa huduma zote za kipadri katika Kanisa Katoliki na kuondolewa kwa muda katika nyumba ya kanisa aliyokuwa akiishi kabla ya tukio.
Mwaka jana, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima alinukuliwa na gazeti hili akisema tayari Askofu Ludovick Minde alikuwa amemsimamisha Padri huyo kufanya kazi na kuongeza;
“Kwa sasa Askofu amemsimamisha kutoa huduma za kipadri mpaka Mahakama ifanye maamuzi yake. Baada ya hapo ndipo maamuzi mengine juu ya upadri yatafanyika.”