Mambo Saba ya Moto Yanayotikisa Taifa

 

Mambo Saba ya Moto Yanayotikisa Taifa

Ni bandika, bandua ya mijadala, ndivyo unavyoweza kuelezea kwa yanayoendelea nchini kupitia mitandao ya kijamii, mikutano ya hadhara na ya wanahabari ambapo mambo saba yakitikisa zaidi.


Mijadala juu ya mkataba wa makubaliano (IGA) kati ya Serikali za Tanzania na Dubai kuhusu uendelezaji wa bandari za bahari na maziwa kupitia kampuni ya DP World ya Dubai na haja ya Katiba mpya, ndiyo imeshika hatamu.


Mingine inayotikisa kwa sasa ni juu ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani na Uchaguzi Mkuu wa 2025, kuadimika kwa Dola ya Marekani na ukosefu wa mafuta katika baadhi ya miji sambamba na bei kupanda.


Pia suala la kuhama kwa wananchi wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro na kukatikatika kwa umeme katika maeneo mengi ya nchi. Mkoa wa Kilimanjaro ikitajwa huenda kuna mgawo usio rasmi kwa kuwa kila siku baadhi ya maeneo hukosa nishati hiyo kwa saa 12.


Laini inayoongoza kukatika umeme ni Boma2 wilayani Moshi. Katika kipindi cha miezi miwili ya Julai na Agosti pekee, kundi la Whatsapp la wateja wa Tanesco lina matangazo ya kuomba radhi zaidi ya 60 yakihusisha maeneo mbalimbali.


Hata hiyo, Wizara ya Nishati mara kadhaa imekuwa ikitoa ufafanuzi kuhusu tatizo hilo na kutoa maelezo ni kwa nini unakatika. Serikali kupitia wizara hiyo imekuwa ikitia saini mikataba mbalimbali ya ushirikiano katika uzalishaji umeme, huku ikiendelea na utekeleza wa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao utazalisha megawati 2,115, ikielezwa kuwa ni suluhisho la tatizo hilo.


Kwa takribani miezi mitatu sasa, mjadala wa IGA umeshika kasi pasipo kutulia, ukiwagawa wananchi katika makundi ya wanaounga mkono, wanaopinga vifungu na wanaotaka ufutwe wote.


Kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba ameamua kukaa kimya juu ya jambo hilo, inaendeleza mjadala makundi hayo yakitaka kujua msimamo wa Serikali kuhusu maoni yapi yalichukuliwa.


Hata hivyo, Serikali ilishaweka wazi kuwa inaandaa nyaraka kwa ajili ya utekelezaji wa makubaliano ya uwekezaji wa bandari kati yake na Dubai.


Akijibu maswali ya waandishi wa habari katika mkutano hivi karibuni, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alieleza hatua hiyo inafuata baada ya Serikali kushinda kesi.


“Hakuna ukimya, Serikali ilishasema kwamba inapokea maoni ya Watanzania, baada ya kukamilisha michakato yote, Bunge limeridhia, hatua inayofuata sasa ni kuandaa nyaraka. Zikikamilika sasa ndiyo tunakwenda kuandaa miradi ya utekelezaji.


“Kinachofanyika ni hivi, baada ya makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai ni mikataba ya utekelezaji. Hii mikataba ndiyo itakayosema sasa mradi wetu utakuwa namna gani, tunashirikiana kwenye eneo gani na mikataba hii itakuwa mingi hautakuwa mmoja,” alisema Msigwa.


Alisema, “Kama ni mkataba wa mifumo bandarini, ushushaji na upakuaji wa mizigo; kama ni mikataba ya kujenga maeneo ya kuhifadhi, kwa kadiri tutakavyokubaliana tutakuja kuwajulisha.”


Hata hivyo, alisema bado wanasikiliza maoni ya wananchi kupitia njia mbalimbali.


Kuhusu Katiba mpya


Mjadala unaendelea huku baadhi ya wachangiaji wakionyesha kutokuwa na imani kama Serikali ina dhamira ya dhati ya kuanzisha mchakato wa kupata Katiba mpya.


Kauli ya aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro kuwa Serikali imejipanga kwanza kutoa elimu ya Katiba kwa miaka mitatu, imeibua sintofahamu kwa wadau wa demokrasia wanaotaka ipatikane kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kufanyika mwakani.


Hili ndilo limesukuma pia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kupitia mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba, kupendekeza mabadiliko madogo katika Katiba ya sasa ya mwaka 1977 kabla ya kwenda kwenye chaguzi zijazo.


Mapendekezo hayo ni kuwezesha kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi, matokeo ya urais kuweza kuhojiwa mahakamani, mshindi kiti cha urais apate kura zaidi ya asilimia 50 na kuwapo ibara zinazoruhusu mgombea binafsi.


Licha ya maoni mengi kutolewa, hata na mawaziri wakuu wastaafu wakieleza kutounga mkono miaka mitatu ya kutoa elimu ya Katiba, Serikali bado haijatoa kauli tofauti na ya awali ya Dk Ndumbaro.


Wananchi Ngorongoro


Baadhi ya wananchi wanaoendelea kuishi ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na wadau wengine wamekuwa wakilalamika kupunguziwa huduma za jamii, madai ambayo Serikali imekuwa ikiyapinga.


Malalamiko yanatolewa ikiwa mwaka mmoja umepita tangu Serikali ilipoanza utekelezaji wa mradi wa kuwahamisha kwa hiari wakazi wa eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kuwapeleka kijiji cha Msomera wilayani Handeni, Tanga. Utekelezaji ulianza Juni 6, mwaka jana.


Kauli za wasomi


Dk Donald Mmari, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti na Sera (Repoa), aliliambia Mwananchi jana kuwa mijadala ni muhimu kwa kuwa inawezesha wananchi kutoa maoni na kupata taarifa zinazohusu masuala muhimu ya kitaifa.


Hata hivyo, alisema mijadala inapaswa kufanywa kwa umakini, kwa uwazi na kwa kutumia taarifa sahihi na zilizofanyiwa utafiti pale inapobidi.


Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, alisema mijadala ni vyema ikaachwa wazi ili wananchi watoe maoni bila hofu na Serikali ijibu hoja kwa hoja.


“Ni mambo yanayoleta athari chanya na hasi kwa wananchi hasa pale maamuzi yanapokuwa dhidi ya wananchi. Nikiangalia hata suala la DP World limewekwa kisiasa. Limewekwa kama vile tunataka wananchi wasituelewe vibaya 2025,” anasema.


Kuhusu kauli ya Serikali kutoa elimu ya Katiba kwa miaka mitatu, Henga alisema hilo ni changamoto kwa sababu haieleweki kwa nini ichukue miaka mitatu ambayo maana yake inakwenda mpaka mwaka 2026.


“Ukiangalia vizuri ni kama imetegewa kipindi cha uchaguzi. Isingekuwa mbaya kama wangekuwa tu wazi wakasema kuepusha hekaheka za uchaguzi tufanye baada ya uchaguzi au wangesema mchakato huu utachukua miaka mitatu,” alisema.


Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe alisema mijadala ni mizuri lakini Serikali ina wajibu wa kusikiliza wananchi na inapowasilikiza inaweza ikasaidia mijadala kutochukua muda mrefu na kuwagawa.


“Mfano mjadala wa Katiba mpya ni mrefu lakini athari yake ni kwamba wakati mwingine unaingilia shughuli za maendeleo. Kuna issue (suala) ya mkataba wa DP World ni suala tu ambalo Serikali haitaki kusikiliwa maoni ya watu.


“Kuna mijadala mingine ambayo inaendelea kwa muda mrefu kwa sababu Serikali haisikilizi maoni ya wananchi na hii inaleta athari. Jambo la msingi kabisa ambalo inaweza kuwa na maana kwa sasa ni Serikali kujenga utamaduni wa kusikiliza,” alisema.


Mwanataaluma ya uchumi, Ernest Boniface alisema suala la kukatikakatika kwa umeme lina athari kubwa za kiuchumi na zinaweza zisionekane haraka lakini viashiria viko wazi kuwa uzalishaji wa uchumi umeathirika.


Wanasiasa


Akijibu hoja hizo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM- Bara), Anamringi Macha alisema tafsiri ya kwanza kuhusu mijadala hiyo ni kufunguliwa kwa demokrasia na uhuru wa kujieleza nchini, chini ya uongozi wa Rais Samia.


“Hii nchi ni yetu sote tunawajibika kuijenga. Lakini kuna hoja nyingine hazijengi na ziko kisiasa bila masilahi ya Taifa.”


Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje ya Chadema, John Mrema alisema wanachokiona ni kama Serikali haina utayari wa kutoa ratiba ya kupata Katiba mpya au kuifanyia marekebisho ili kupata Tume Huru ya uchaguzi.


Jambo hili linaweza kuipelekea nchi yetu kuwa katika kipindi kigumu na hasa kutokana na ukweli kuwa wananchi hawana imani na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa itasimamia uchaguzi huru na haki kutokana na muundo na inavyopatikana.


Kuhusu kuadimika kwa Dola ya Marekani, Mrema alisema inatokana na ukweli kuwa Taifa halina mipango thabiti ya kuikwamua nchi kiuchumi na mipango yake na miradi yake mingi ni kutoa fedha za kigeni nje zaidi ya kuingiza nchini.


“Mathalani, ujenzi wa SGR na bwawa la Nyerere badala ya Serikali kuwekeza kwenye chuma cha ndani, wanatumia fedha nyingi kuagiza chuma kutoka nje ya nchi. Hata utalii, hakuna mbinu mpya za kuvutia watalii kuja nchini,” alisema.


Kwa upande wake, Katibu mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alisema ni jambo la faraja kwamba utamaduni wa mijadala ya kitaifa umereja Tanzania na kwamba hivi sasa kwa kiasi fulani watu wana uhuru wa kutoa maoni yao.


“Hata masuala ya Katiba mpya na chaguzi za Serikali za Mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025 yana matokeo ya muda mrefu ya kisiasa na matumaini ambayo wadau wanayo juu ya Serikali ya awamu ya sita, kuwa utakuwa wa huru na haki”


Shaibu alisema ni muhimu utamaduni wa kujadiliana uwekewe ulinzi na misingi imara ya kisheria na kikatiba kuhakikisha sheria zinazosimamia uhuru na uwazi zinaimarishwa hasa zinazosimamia vyombo vya habari na mitandao.


“Majadiliano ni afya katika kila jambo, husaidia kuboresha nyanja mbalimbali hivyo tusikubali aina yoyote ya kuminya na kuzuia mijadala” alisema

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad