Revocatus Muyela ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi ya mauaji ya dada wa marehemu Erasto Msuya maarufu Bilionea Msuya, Aneth Msuya amemtaka Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha, SSP David Mhanaya kuacha kumchafua kwa kumwita mhalifu mzoefu.
Muyela alitoa kauli hiyo jana mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Jaji Edwin Kakolaki wakati SSP Mhanaya akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Paul Kimweri kujibu maswali kizimbani.
Katika kesi hiyo mstakiw a mwingine ni mke wa Bilionea Msuya, Miriam Mrita.
Mshtakiwa Muyela alifika hatua ya kutoa kauli hiyo baada ya shahidi SSP Mhanaya kutakiwa aeleze tofauti ya majina ya mshtakiwa huyo ambayo ni Revocatus Molel na Revocatus Everest .P. Mollel.
SSP Mhanaya alidai kuwa alipokwenda kufanya upekuzi kwa hati ya dharura nyumbani kwa mshtakiwa namba mbili (Revocatus) alikuta cheti cha kuhitimu mafunzo ya mgambo chenye jina la Revocatus Mollel na kitabu cha miliki ya bastola chenye jina la Revocatus Everest .P. Mollel.
Alidai kuwa mtuhumiwa huyo hakukataa kuyatumia hayo majina kwa sababu alisaini hati ya upekuzi pamoja mashahidi huru.
"Ki msingi hizi ndizo tabia za wahalifu wazoefu kutumia majina tofauti tofauti," alidai SSP Mhanaya
Hata hivyo baada ya SSP Mhanaya kutamka maneno hayo, Mshtakiwa Revocatus alianza kuzungumza kwa sauti ya chini huku akionesha kukerwa na kuchukizwa na matamshi hayo.
Kufuatia hali hiyo, Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala alisimama na kupinga vikali kilichosemwa na shahidi huyo.
Kibatala alisema kauli ya shahidi (SSP Mhanaya) inakinzana na Katiba ya Tanzania na kwamba kwa maneno hayo shahidi anakuwa anamhukumu mtuhumiwa.
Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali Kimweri alidai kuwa haoni kama kuna jambo tofauti ambalo amelizungumza kwa sababu tangu aanze ushahidi amekuwa akilisema
Wakati Kimweri akiyaeleza hayo, Mshtakiwa Revocatus alitoa sauti na kudai kuwa shahidi anamchafua kwa kumwita yeye ni mhalifu mzoefu wakati hamjui.
"Hapa kuna waandishi wa habari halafu anasema maneno haya huku si kuchafuana, kwa sababu anijui kabisa," alidai Mshtakiwa Revocatus