BAADHI ya kauli alizotoa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta akiwatahadharisha wakazi wa Mlima Kenya dhidi ya kumchagua Rais William Ruto mwaka 2022 zinaonekana kutimia, kutokana na gharama kubwa ya maisha ambayo inaendelea kuwaandama Wakenya wengi.
Kwenye majukwaa tofauti mwaka uliopita, Bw Kenyatta alinukuliwa akiwatahadharisha wakazi kwa lugha ya Gikuyu, kwamba ikiwa wangemchagua Dkt Ruto, wangemkumbuka, kwani hali ya maisha ingeendelea kuwa ngumu.
Kutokana na hali ilivyo, wakazi wengi wanasema kuwa hatimaye ‘utabiri’ wake unaonekana kutimia, kwani hali gharama ya maisha inaendelea kupanda.
Kwenye mahojiano na vituo vya redio vinavyopeperusha matangazo yake katika ukanda wa Mlima Kenya Februari 2022, Bw Kenyatta alisema wakazi hao wangemkumbuka kwani “tahadhari zake hatimaye zingetimia”.
“Andu aitu, thikiririai. Ni mukaandirikana rimwe, tondu mauundu maya ndimwiiraga ni magakinyanira,” akasema Uhuru, tafsiri yake ikiwa: “Watu wetu, sikilizeni. Mtanikumbuka siku moja, kwani mambo haya ambayo huwa nawaambia yatatimia.”
Mnamo Agosti 2, 2022, alipokuwa akihutubu katika Kaunti ya Kiambu, alisema Bw Kenyatta: “Nyinyi wakazi wa Mlima Kenya, mkimchagua Ruto mtajuta, kwani yeye si mzuri.”
Akaongeza: “Mtu anayeongozwa na tamaa, huwa anazungumza yaliyo moyoni na yale atakayofanya akiwa uongozini.”
Akihutubu tena katika Kaunti ya Kiambu, Juni 2022, alisema Bw Kenyatta: “Mutuure ukamurituhira. Mukaanjiraga, munene ni kurituhire muno. No hingo iyo ngaamwira, ngaang’anai toondu hingo iyo ngaakorwo ngirora mauundu maakwa.” (Hali ya maisha itakuwa ngumu. Mtakuwa mkiniambia, mkubwa, hali ya maisha imekuwa ngumu sana. Lakini wakati huo, nitaambia mng’ang’ane kwani wakati huo nitakuwa nikiangalia mambo yangu kama mzee.”
Kutokana na kauli hizo, baadhi ya wakazi wanasema huenda semi za Bw Kenyatta zimeanza kutimia, kwani gharama ya maisha inaendelea kupanda kuliko hali ilivyokuwa.
“Ingawa kauli zake zilikuwa za kisiasa, kwani alikuwa akimpigia debe kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, huenda utabiri wake umeanza kutimia kwani kama alivyotutahadharisha, hali imeendelea kuwa ngumu,” akasema Bi Mercy Njoki, ambaye ni mkazi wa Kaunti ya Kiambu.
Kauli hiyo iliungwa mkono na wakazi wengine, baadhi wakikiri kwamba wanatamani uongozi wake.
Hata hivyo, wengine walisema kuwa ni mapema kuuweka kwenye mizani utendakazi wa serikali ya Rais Ruto, kwani imemaliza mwaka mmoja uogozini majuzi.
“Nadhani si haki kusema utabiri wa Bw Kenyatta umetimia, kwani alikuwa akiufanyia kampeni mrengo wa Azimio. Maisha yamekuwa magumu kila sehemu duniani. Naamini mikakati aliyoweka Rais Ruto kuufufua uchumi itazaa matunda,” akasema Bw Jamleck Mwangi, aliye pia mkazi wa Kiambu.