Bunge limesimamisha shughuli zake kwa sekunde 68 wakati wabunge walipokuwa wakipiga makofi alipokuwa anaingia bungeni Naibu Waziri Mkuu Dk Doto Biteko.
Aliingia bungeni wakati Bunge lilipokuwa kwenye kipindi cha maswali na majibu na Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwan Kikwete alikuwa akijibu swali namba 58 kuhusu wanaojitolea kupewa ajira ambalo likiulizwa na Mbunge wa Kiteto (CCM) Edward Kisau.
Dk Biteko ameingia bungeni saa 3.47 asubuhi ambapo Moja kwa Moja alikwenda kuketi katika kiti cha mstari wa mbele ambacho hutumiwa na Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia bunge na Uratibu Jenister Mhagama ambaye leo alibadilishiwa kiti.
Alipoingia alianza kuwasalimia Profesa Joyce Ndalichako na George Simbachawene na kisha akaelekezwa kiti cha kukaa.
Dk Biteko aliapishwa Septemba Mosi 2023 katika shughuli iliyofanyika Zanzibar.
Mbali na nafasi ya Naibu ya Naibu Waziri Mkuu, Dk Biteko pia ni Waziri wa Nishati.
Spika wa bunge, Dk Tulia Ackson ametoa pongezi kwa kiongozi huyo katika cheo kipya ambapo amemuahidi kumpa ushirikiano katika majukumu yake.
Mbali na ahadi hiyo, amewataka wabunge kutambua cheo kipya cha kiongozi huyo hata pale wanapomuita kwenye vikao vya kamati zao.
Kwa upande wa Mawaziri na Naibu Mawaziri ambao walichwa, amewaomba kuwa watulivu kwani nafasi hizo ni sawa na timu ya mpira ambapo mchezaji anayeingia na anayeachwa wote ni sawa isipokuwa kocha ameona mchezo unamtaka nani.
Amesema wapo mawaziri ambao waliwahi kuachwa kwenye uteuzi lakini wakateuliwa tena na kuendelea na majukumu pale ilipofika zamu yao.