Nawaona Yanga Hawa Wakileta Kombe la CAF Tanzania

Nawaona Yanga Hawa Wakileta Kombe la CAF Tanzania


Pengine sio msimu huu wala msimu ujao, lakini unaanza kuona dalili za timu inayopiga hatua kwenda mbele. Kitendo cha Yanga kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita hakikuwa kidogo. Ni hatua kubwa.


Hapa nchini Simba wamekuwa na utamaduni wa kupiga hatua nyingi sana mbele kimataifa, lakini wamekuwa pia na hatua nyingi sana za kurudi nyuma. Muda ambao unadhani Simba wanaweza kufika fainali tena ya CAF ndiyo muda ambao wanatolewa nyumbani na Jwaneng Galaxy F.C.


Muda ambao unadhani Simba hawezi kutoboa kwenye kundi lenye timu kama Al Ahly, Al Merreikh na As Vita anakwenda kiwa kinara. Ni vigumu sana wakati mwingine kujua kama Simba inakwenda mbele sana au inarudi nyuma. Naona utofauti mkubwa kwa namna Yanga inavyokuja kwenye kizazi hiki.


Nawaona Yanga wakiimarika zaidi karibu kwenye kila msimu. Naona kuna ukomavu unazidi kujengeka kwenye kila eneo. Yanga wanazidi kuwa wazoefu kuanzia kwenye maandalizi ya timu hadi aina ya usajili wa wachezaji wanaofanya.


Wanazidi kupiga hatua pia kwenye matokeo uwanjani. Misimu miwili nyuma walifungwa nje na ndani na Rivers United kwenye hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Msimu uliopita hali ilikuwa tofauti, Yanga hakupoteza mechi hata moja. Ni Yanga inayopiga hatua zaidi kwenda mbele.


Baada ya Simba kuwapoteza Luis Miquissone na Clatous Chama timu iliyumba. Simba inaparaganyika, lakini ni tofauti na Yanga. Yanga wamempoteza Fiston Mayele, Feisal Salim ‘Feitoto’ na Yannick Bangala, lakini bado wako imara.


Timu inaonekana ni kama hajaondoka mchezaji yetote. Mtu pekee ambaye bado anaonekana hawajafanikiwa kuziba pengo ni Mayele, lakini wanaendelea kufunga mabao. Ilikuwa hadithi tofauti na Simba walipoondoka Miquissone na Chama.


Kama ungeulizwa swali la timu gani unaiona ilicheza fainali ya CAF kutoka Tanzania miaka mitatu ya nyuma majibu yangekuja kuwa Simba. Unajua kwa nini? Ni rahisi tu.


Mfalme wa Soka la Tanzania ni Yanga kiasili. Ndiyo haishangazi kuwa ametwaa ubingwa mara nyingi zaidi kuliko timu nyingine yoyote. Lakini linapokuja suala la kimataifa Simba amekuwa na rekodi nzuri licha ya kuwa kuna muda anakwenda mbele na kuna muda anarudi nyuma.


Ni ukweli ulio wazi kuwa hadi sasa bado Simba ina rekodi nzuri kimataifa kuliko Yanga, lakini Yanga wanaonekana kuja juu kuliko kawaida. Yanga wanaonekana kuwa siriazi na michuano hii kuliko hata Simba. Kila msimu wanaweza kuwa bora zaidi. Ukiwatazama uwanjani unaona kabisa kuwa wanaume hawana utani. Vijana hawana masihara kabisa.


Hakuna kitu kigumu kwa mpira wa Afrika kama kushinda Ugenini, lakini sio kwa Yanga. Yanga wameshinda mechi sita za ugenini kimataifa mfululizo. Hakuna timu kutoka Tanzania imewahi kufanya hivyo. Huu ni uelekeo tofauti kabisa wanaokuja nao.


Haya ni mabadiliko makubwa ambayo hayaji kwa bahati mbaya. Hatua kama hizi sio rahisi kuzifikia. Wanaonekana sasa wanakwenda kuwa wakubwa Afrika. Wamekataa kuwa wateja kimataifa kila siku.


Na hapa walipo hata uwekezaji ndani ya klabu bado haujafanyika. Hapa walipo ni nguvu ya wafadhili na wadhamini. Hivi itakuwaje wawekezaji watakaponunua hisa ndani ya klabu hii? Balaa juu ya balaa.


Hapa walipo wapo kwenye mchakato wa kuruhusu wawekezaji kuweka mabilioni ya pesa ndani ya klabu. Hapa walipo wapo kwenye mchakato wa kutengeneza timu. Kwa mtindo huu kuna watu siku moja maji wataita mma. Yanga wanaonekana wako siriasi sana kipindi hiki kuliko wakati mwingine wowote.


Kwa hatua hizi nazoziona kwa Yanga inawezekana sio msimu huu wala ujao, lakini watakuja kuleta kombe la CAF nchini. Kumbuka walifika fainali msimu uliopita. Kumbuka hawa watu wanaimarika karibu kila msimu na uwekezaji bado haujafanyika. Nawaona mbali sana.


Moja kati ya changamoto kubwa za Simba ni kwenda mbele hatua mbili na kurudi nyuma hatua mbili. Suala lao la uwekezaji halijulikani kama linakwenda mbele au linarudi nyuma. Ni kama bado wanaishi mfumo wa zamani wa kutegemea pesa za mtu. Ni kama bado wanaishi maisha yaleyale.


Ni kama mbinu za kusajili wachezaji bado ni zilezile za kiongozi huyu kuleta wachezaji wawili na mwingine kuleta kocha. Nadhani bado kuna vitu haviko sawa pale Msimbazi. Kama mambo yasipobadilika kwa haraka Yanga inaweza kuja kuwatangulia.


Simba ilikuwa mbali sana misimu minne ya nyuma, lakini kwa sasa naona ni kama imeshuka tena. Hata ushindi wake umekuwa wa kuvizia sana. Sio Simba inayokupa uhakika kabla ya dakika 90.


Sio Simba ile yenye ubabe mwingi porini. Sio mfalme tena wa pori. Kuna wanyama watataka kufurukuta mbele yake kwa sasa. Wanaonekana Yanga wanakuja vizuri na eneo wanalowazidi Simba kwa sasa ni kwenye usajili wa wachezaji na utengenezaji wa timu.


Kwa kutazama uwezo wa mchezaji mmojammoja, Simba imefanya usajili mzuri, lakini kwa kutazama uchezaji wa timu hapa ndipo inapoachwa na Yanga. Yanga wamepunguza kutengemea uwezo wa mchezaji mmojammoja na sasa wameipata timu.


Ndiyo maana kwa sasa yeyote anaweza kufunga. Mabao yanatoka kila kona ya uwanja. Pale Simba kama kocha atapambana vizuri anaweza kuja kuipata timu nzuri. Ukishakuwa na wachezaji wazuri ni kazi sasa ya kocha kutengeneza timu, kitu ambacho nadhani pale Simba bado hakijafanikiwa.


Kwa mwendo huu wa Yanga. Kwa matokeo haya wanayoanza kupata. Kwa hatua hizi wanazopiga kila siku kuna makubwa yanakuja. Inawezekana isiwe msimu huu wala msimu ujao Yanga watakuja kuupata ubingwa wa Afrika.


Naiona timu inayopiga hatua kubwa kwenda mbele. Wamekubali kujifunza kwa timu zilizowatangulia kwa hiyo njia yao haiwezi kuwa ngumu. Walitazama mchakato wa Simba wa kutengeneza kikosi bora na wakajifunza. Walitazama mchakato wa uwekezaji wa Simba na kujifunza. Hawa Yanga wanachofanya ni kuboresha pale Simba walipokwama. Hakuna kitu rahisi kwenye dunia kama kuiga na kuboresha. Mara nyingi unapata kitu bora zaidi na kuwa mwalimu mzuri.


Nahisi kuna mahali Simba wamekwama. Kuna haja ya kurudi nyuma na kuzichanga karata zao upya. Walikuwa wanakuja vizuri kama wachonga barabara ya kimataifa nchini. Bado wana nafasi nzuri tu ya kwenda hatua ya makundi.


Bado wanaweza kucheza hata robo fainali, lakini zaidi ya hapo pengine mimi na wewe wote hatujui. Timu ni nzuri, lakini bado haitupi uhakika maana Simba ni kama inakwenda hatua mbili mbele na kurudi nyuma hatua mbili.


Yanga kuna namna unaweza kusema wameanza kujipata na hatua zao naona nyingi ni zile za kwenda mbele. Mpira wetu utakua sana hasa kama timu zetu zote hizi mbili zitapiga hatua kwenda mbele. Kama una maoni yotote kwenye hili nitumie ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad