Tayari ratiba iliyokuwa ikisubiriwa sana ya michuano mipya yenye hadhi kubwa barani Afrika inayoitwa African Football League ambayo inazishirikisha timu nane bora barani Afrika imepangwa, huku macho na matumaini yetu Watanzania yakiangalia nani atapangwa na Simba.
Ilikuwa haina Simba ni lazima ingepangwa na timu kubwa barani Afrika kati ya Al Ahly ya Misri, Esperance ya Tunisia, Wydad Casablanca Morocco au Mamelod Sundowns ya Afrika Kusini, lakini Simba imeangukia kwa Al Ahly ya Misri ambapo katika hizo timu kubwa nne ni Esperance na Mamelodi ndizo hazijawahi kutana na Simba kwenye michuano mikubwa barani Afrika.
TUWAANGALIE WAKUBWA HAWA
Bila shaka mchezo huu ambao kwa mara nyingine Simba itaanzia nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa katika mechi karibia ya tatu sasa, utakuwa bora hasa kwa kuwa rekodi inaipa nafasi zaidi Simba kupata ushindi kwenye mchezo huo wa ufunguzi barani Afrika.
Rekodi kama nilivyosema zinaibeba Simba inapokuwa nyumbani kwa kushinda michezo miwili iliyochezwa huko nyuma siku kwa ushindi wa bao moja kila mchezo.
ZINAMALIZIA ZILIPOISHIA
Al Ahly ndio mabingwa wa soka barani Afrika na Simba ilitolewa kwenye hatua ya robo fainali huku ratiba ikionyesha kuwa timu hizi zingeweza kukutana kama Simba ingeitoa Wydad Casablanca kwenye hatua ya robo fainali lakini haikufanikiwa
Simba ilibadilika sana kutoka michezo yake ya awali kwenye hatua ya makundi ambapo ilimaliza ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Raja Casablanca huko nyuma ilipoteza michezo miwili dhidi ya Raja na Horoya lakini ikaja kufanya mapinduzi makubwa kuelekea robo fainali.
Al Ahly nayo ilifanya kitu kama hicho ikianza vibaya kwenye kundi lake na kina Mamelod Sundown, Al Hilal ya Sudan na Cotonou Sportive, ikiambulia kipigo kutoka kwa Mamelod na Al Hilal lakini ikamaliza nafasi ya pili, ikaanza kubadilika kwa kasi kwa kuifunga Raja Casablanca hatua ya robo fainali, Esperance na kuifunga Wydad Casablanca kwenye fainali kwa jumla ya mabao 3 - 2.
EMBU TUANGALIE SILAHA ZAO
Simba inaingia kwenye mchezo huu hasa ikitegemea silaha zake za aina mbili.
MFUMO: Simba ina matumizi mbalimbali kwa sasa kwenye uchezaji wa timu chini ya Kocha Robertinho, kuna kipindi inaanza na 4 : 2 : 3 : 1 hapo ikiwa na Fabrice Ngoma na Mzamiru Yassin huku mbele ikiwa na Said Ntibazonkiza nyuma ya mshambuliaji Jean Bareke huku pembeni ikiwatumia Clotous Chama na Essomba Onana na kuna muda inawatumia washambuliaji wawili mbele kwenye mfumo wa 4 : 4 : 2 Diamond.
Al Ahly inapenda sana kwenda na mfumo wa 4 : 2 : 3 : 1 hapo kati kuna wachezaji mahiri kama Alilou Dieng na Amr EliSolia hapo mbele ikiwatumia Percy Tau, Mohamed Magdy Afsha na Ahmed Abdel Kader kuwasumbua mabeki wa timu pinzani ili kumrisha Mshambuliaji Mohmoud Abdel Kahraba.
VITA YA WALINZI WA PEMBENI
Hizi ni silaha za kila timu kwa pande zote hizi mbili, Simba na Al Ahly kwa kuwa zimekuwa zikizalisha mabao mengi kupitia pembeni ama kulia au kushoto .
Simba kwa Shomary Kapombe na Mohamed Hussein: Hawa ni mabeki wawili walioweka heshima kwenye michuwno mbalimbali barani Afrika, Shomari bado anaendeleza mwendo kulia huku Mohamed Hussein akipanda kila mara kushambulia kupitia kushoto .
Nayo Al Ahly ina silaha kama hizo upande wa kulia na kushoto ambako utawakuta Ali Maalou upande wa kushoto na Mohamed Gamal upande wa kulia, hawa wamekuwa bora sana wanapopanda kuongeza mashambulizi na wana macho ya kupiga krosi sahihi.
AL AHLY HUPOTEA KWA MKAPA
Moja ya vitu ambavyo huwapa tabu sana Al Ahly wakiwa kwenye Uwanja wa Mkapa ni saikolojia ambayo imeishikilia kwa muda sasa kuwa huu ni moja kati ya viwanja vigumu kwao, hiyo ndio silaha nyingine ambayo Simba imekuwa ikiitumia kuwaadhibu Al Ahly.
Pili, Al Ahly ikiwa nje ya Misri hasa inapocheza mchezo kama huo wa kwanza ugenini huingia na lengo la kuzuia zaidi na kupoteza muda huku ikijaribu kuupozesha mchezo, kitu ambacho Simba imekuwa ikikitumia kuwaadhibu.
SIMBA WASICHEZE KWA MAZOEA
Ni ukweli usiopingika kuwa tayari Simba imekuwa ikiwamudu sana Al Ahly hapa nyumbani ingawa hupata tabu kwenye hatua ya mwisho ya kuitoa, hata hivyo Simba inatakiwa kuwa makini kwa sababu hizi.
Timu zinaingia kuweka rekodi: Hii ni michuano ya kwanza kwa ukubwa barani Afrika kuwa na utajiri wa pesa nyingi. Timu zinaingia kuhakikisha zinashinda ili kupata zawadi itakayoambatana na pesa nyingi.
Pia timu zinataka kuweka rekodi ya kuchukua ubingwa wa michuano hii kwa mara ya kwanza .
Sababu hizi zitafanya michezo miwili ya Simba dhidi ya Al Ahly nyumbani na ugenini kuchezwa kwa uhuru zaidi huku timu zikicheza kwa kushambuliana bila kurudi nyuma.
Hivyo, Simba inaweza kupotea iwapo tu itaamini Al Ahly itakaa nyuma ya mpira kwa muda mrefu badala yake inaweza kupata mshtuko kutokana na jinsi Al Ahly inavyoweza kubadilika kwa kushambulia bila kurudi nyuma.