Siri ya Mauaji ya Bilionea wa Madini na Mwanaye Huku Ruvuma, Watuhumiwa Wakamatwa



Songea. Siku moja baada ya kifo cha mfanyabiashara wa madini, Marwa Masese (45) na mwanaye, John Marwa (28), dada wa marehemu, Grace Marwa amesimulia mkasa huo akidai kuwa mdogo wake alisaini mkataba wa Sh2 bilioni na alikuwa anasubiri fedha iingie benki.

Marehemu hao, wakazi wa Kunduchi jijini Dar es Salaam, wanadaiwa kuuawa na marafiki zao mkoani Ruvuma walikokwenda kwa shughuli za kibiashara.

Akisimulia mkasa huo kando mwa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea (HOMSO), Grace alidai kuwa kaka yake alikuwa ametoka kununua dhahabu Mbeya, kwenye gari alikuwa na mali nyingine nyingi na fedha taslimu.

Alidai kuwa baada ya kuuawa, watuhumiwa walitoroka.

Grace alisema wameitambua miili ya ndugu zao na wameona walivyoumizwa lakini wanasubiri uchunguzi wa daktari.

Alisema wakikabidhiwa miili hiyo wataamua kama watapata nafasi ya ndege waisafirishe kesho kwenda Dar es Salaam na wakikosa watasafirisha kwa magari.

Grace alisema kifo hicho ni pigo kubwa kwa familia kwa sababu marehemu ni mdogo wake anayemfuata, alikuwa msaada mkubwa kwake na juzi walikuwa waende India kwenye matibabu yeye na mwanaye na walishakata tiketi za ndege kwa ajili ya safari hiyo.

“Nimeumizwa sana na hili tukio, ni baya na linaumiza sana, sina cha kusema ila nawashukuru Jeshi la Polisi, wametusaidia na wameonyesha uaminifu mkubwa,” alisema Grace.


“Kabla ya kuuawa, aliniambia ameshasaini mkataba wa Sh2 bilioni na alikuwa anasubiri pesa zake ziingie benki na tayari alishanunua hisa.

“Nimeumia kumpoteza mdogo wangu na mwanaye, najua wameuawa kikatili ila Mungu atawalipia,” alisema Grace.

Mwanamke huyo alisema kabla ya Marwa kukumbwa na mkasa huo, alikuwa akiwasiliana naye kila siku, lakini baadaye alipompigia simu, haikupatikana.


Alisema anawashukuru polisi kwa kuwapatia mkufu wa dhahabu wa marehemu wenye thamani ya Sh3 milioni waliouokota ndani ya gari lake.

“Nahisi ulikatika ukadondoka chini wakati wa purukushani,” alisema Grace.

Alisema mdogo wake huyo alikuwa akiishi na watoto wake wawili wa kiume, John ambaye ameuawa na Samson (18), kwa sababu mkewe walitengana.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa ya Rufaa ya Songea, Edson Francis alisema wamefanya uchunguzi na ripoti kamili itatolewa na Jeshi la Polisi.

Ofisa Madini Mkoa wa Ruvuma, Hamis Kamando alisema wamelipokea tukio hilo kwa masikitiko kwa sababu Marwa alikuwa mwekezaji na tayari alikuwa amepata leseni ya udalali wa madini.

Wakili wa familia hiyo, Gregory Ndanu alisema tukio la mauaji ya mfanyabiashara huyo na mwanaye limemsikitisha kwa sababu wauaji wamefanya unyama usiokithirika kwa rafiki yao.

Juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya aliliambia Mwananchi kuwa mfanyabiashara huyo na mwanaye wameuawa kwa kupigwa kichwani na kitu kizito chenye ncha kali.

Alisema tukio hilo lilitokea Kitongoji cha Mkerema, Kijiji cha Lilondo, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma.

Alisema John (mtoto) alikutwa na jeraha kubwa kichwani na uchunguzi wa awali ulionyesha kapigwa na kitu kizito chenye ncha kali kilichosababisha ubongo kutoka nje.

“Baada ya mauaji hayo, wauaji hao waliichukua miili yao na kuiweka kwenye gari la Marwa ambalo ni Jeep lenye namba za usajili T241 DSX kisha wakalisukuma hadi kwenye korongo,” alidai kamanda huyo.

Alidai lengo la kulisukumia gari hilo ni kutaka ionekane kuwa walipata ajali.

Hata hivyo, Kamanda Chilya alisema makachero walipolikagua gari hilo halikuwa limepata ajali.

“Baada ya kufanya utafiti tumefanikiwa kumkamata dereva aliyekuwa akiliendesha lile gari aliyetuambia kuwa baada ya tukio, wenzake walimsindikiza hadi kituo cha mafuta kusudi aende polisi akatoe taarifa kwamba kapata ajali,” alidai kamanda Chilya.

Alidai ili kupoteza ushahidi, dereva huyo alipigwa na kitu chenye ncha kali mguuni ili naye aonekana kapata majeraha kwenye ajali hiyo ya kutengeneza.

Anadai baada ya kumhoji alimtaja mtuhumiwa mwingine ambaye naye ametiwa mbaroni akihusishwa na tukio hilo.

“Lakini tumebaini watuhumiwa hawa wote ni wakazi wa Kunduchi, Dar es Salaam na wanafahamiana vizuri na marehemu Marwa na walisafiri naye Agosti 17, 2023 kuja Songea wakaenda mpaka Kijiji cha Amani Makolo kulikokuwa na machimbo ya Marwa,” alidai kamanda huyo.

Alisema Marwa alikuwa akimiliki vitalu 10 vya madini aina ya safaya alivyoviwekeza kwa mwekezaji.

“Na huyu muuaji tumeambiwa ndiye aliyefanikisha kupatikana kwa mwekezaji huyo na ilitakiwa apatiwe asilimia 30 ya hisa katika mradi huo,” alidai kamanda huyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad