Serikali nchini, imewatahadharisha wananchi kuacha kujenga na kufanya shughuli za kijamii kwenye maeneo ya bondeni, ili kuepukana na athari za mafuriko zinazoweza kutokea na kuwasababishia madhara na kudai kuwa elimu itaendelea kutolewa ikilenga kuwaepusha na dhana ya mabondeni kuwa makazi.
Tahadhari hiyo hii leo Septemba 5, 2023 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Stella Ikupa aliyetaka kujua Serikali imejipangaje kukabiliana na athari za mvua za El – Nino zinazotarajiwa kunyesha kuanzia Oktoba, 2023.
Amesema, “ni kweli panapokuwa na mvua kubwa kama hizi mara nyingi hutokea madhara ambayo yanaharibu makazi na kugharimu maisha ya watu, hivyo Serikali katika kipindi hiki tunawapa elimu wasijenge kwenye maeneo ambayo yanakaa maji na kama wana mpango huo basi waondoke ili mvua zitakaponyesha wasipate madhara.”
Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Nungwi, Simai Hassan Sadiki aliyetaka kujua mkakati wa dharura wa kunusuru athari za mabadiliko ya tabianchi eneo la Nungwi, Zanzibar, Naibu Waziri Khamis aliwahimiza wananchi kuendelea kupanda mikoko katika fukwe za bahari ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ameongeza kuwa, kwa kutambua changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi, tayari Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeanza kuchukua hatua za kukabiliana nazo na kwamba katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24, SMZ imetenga kiasi cha shilingi milioni mia sita na hamsini kwa ajili ya kufanya tathmini ya awali ya kuzuia changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, Naibu Waziri Khamis amesisitiza kuwa Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na SMZ zitashirikiana katika kutafuta fedha zaidi ili kudhibiti uharibifu unaotokea eneo la Nungwi na hivi karibuni Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania – TMA, ilitangaza kuanza kwa mvua za El – Nino Oktoba hadi Desemba 2023 na kutahadharisha kuweza kusababisha madhara kwa binadamu na mazingira ikiwemo mafuriko