MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Arusha, ikiwa ni siku moja tangu azuiwe kuingia katika hifadhi ya Ngorongoro kwa ajili ya kufanya mikutano ya hadhara kwa lengo la kuzungumza na wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumapili na Mwenyekiti wa Chadema Arusha, Elisa Mungure, Lissu pamoja na walinzi wake walikamatwa akiwa katika Hoteli moja ya Nyota Tano Ngorongoro wilayani Karatu.
“Polisi wamekuja kwenye hoteli na kuingia kwa nguvu wakamkamata Makamu Mwenyekiti Chadema Bara, Lissu na walinzi wake,” imesema taarifa ya Mungure.
MwanaHALISI Online imemtafuta kwa njia ya simu Mungure ili kujua sababu za Lissu na walinzi wake kukamatwa lakini alisisitiza atafutwe baadae kwani yuko na polisi.
“Nitafute baadae saa hizi niko na polisi, niko busy,” amesema Mungure.
Hata hivyo, jitihada za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, kujua undani wa tukio hilo hazikuzaa matunda baada ya namba zake za simu kutokuwa hewani.
Mwanasiasa huyo kabla ya kukamatwa, alipanga kwenda Ngorongoro kwa ajili ya kuzungumza na wananchi wanaodaiwa kugoma kuondoka hifadhini hapo kwenda katika eneo la Msomera Handeni lililotengwa na Serikali kwa ajili yao.