Tundu Lissu Anahitajika Polisi Tena na leo

 

Tundu Lissu Anahitajika Polisi Tena na leo

Jeshi la polisi mkoani Arusha limewapa dhamana viongozi wa Chadema waliokuwa wanashikiliwa akiwemo Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Tundu Lissu huku wakiwahitaji kuripoti leo asubuhi Jumatatu Septemba 11, 2023.


Taarifa za kukamatwa kwa viongozi hao wa chama cha upinzani zilitolewa na Kamanda wa Polisi mkoa Arusha, Justine Masejo mchana Septemba 10, 2023 kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko usio halali na kuzuiwa Jeshi la Polisi kutekeleza wajibu wake.


Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Elisa Mungure amesema viongozi hao wameachiwa kwa dhamana na kesho saa tatu wametakiwa kurudi polisi.


"Muda huu tunamsindikiza Lissu kwenda kwa kaka yake Wakili Alute Mungwai na viongozi wengine tutawapeleka hoteli na tumetakiwa kesho asubuhi saa tatu (Jumatatu) warudi,"amesema.


Amesema pia viongozi waliokuwa wanashikiliwa vituo vya polisi Karatu  akiwepo Katibu wa Baraza la Wanawake Taifa(Bawacha), Catherine Ruge pia wameachiwa.


Awali Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alisema tangu alipokamatwa Lissu mchana walikuwa hawajuwi alipopelekwa.


"Tulikuwa tunamtafuta ili kujua alipo lakini usiku huu tulipata taarifa yupo Arusha ndipo tukaanza kushughulikia dhamana,"amesema


Amesema kukamatwa kwa Lissu na viongozi wote Karatu kulizuia kufanyika mkutano mkubwa wa hadhara mjini hapo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad