Tundu Lissu Awasifu Polisi Kwa Kumkamata

Tundu Lissu Awasifu Polisi Kwa Kumkamata


Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu na viongozi wengine wa chama hicho waliokuwa wamekamatwa wilayani Karatu mkoani Arusha wamepewa dhamana baada ya kuandika maelezo kituo kikuu cha Polisi Arusha na Polisi Wilaya ya Karatu.


Viongozi hao walikuwa wanatuhumiwa kufanya mikusanyiko bila kuwa na kibali na kufunga barabara ya Karatu kuelekea Ngorongoro huku Lissu akiwasifu polisi kwa ustaarabu.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 11,2023 baada ya kumaliza kuandika maelezo, Lissu ambaye alikuwa na kaka yake Wakili Alute Mughwai amesema baada ya kuandika maelezo ametakiwa kurejea baada ya mwezi mmoja.


Lissu amesema tuhuma ambazo alikuwa akihojiwa kuanzia saa 3:15 asubuhi hadi saa 7:20 mchana ni kufanya mkusanyiko usio halali na kufunga barabara.


"Nimewaeleza mimi sijafanya mkusanyiko na sikufunga barabara kwani waliofunga ni polisi wakati wanatuzuia kuendelea na safari kwenda Ngorongoro," amesema.


Amesema baada ya polisi kufunga barabara na kuona wanataka kupiga watu ndipo waliamua kukaa barabarani na hawakufunga barabara.


Hata hivyo, amesema safari hii Jeshi la Polisi tangu lilipowakamata juzi jioni hawakuwafanyia kitu kibaya badala yake wamewahoji kistarabu.


"Hii sio mara yangu ya kwanza kukamatwa safari hii sikulala ndani tangu waliponikamata hadi saa hizi hawajanifanyia chochote ambacho naweza kusema sio kizuri polisi wamekuwa wastaarabu sana tangu waliponikamata jana," amesema.


Lissu amesema, hata hivyo kukamatwa kwake na viongozi wengine hakutawazuia kurejea kufanya mikutano Ngorongoro na Karatu.


"Tunakwenda kujipanga kwa ajili ya mikutano ya kanda ya kaskazini tutakwenda Ngorongoro kwani sio gereza na tutakwenda Karatu," amesema.


Wakili Munghwai akizungumza na Mwananchi pia alieleza mteja wake kupewa mwezi mmoja kuanzia leo ndipo kurejea kuripoti polisi ambapo ni Oktoba 10.


Viongozi wengine waliokuwa wanashikiliwa na polisi na wamepewa dhamana ni Katibu wa Taifa wa baraza la wanawake Taifa, Catherine Ruge, Suzan Kiwanga Mjumbe wa Kamati Kuu, Mzee Hashim, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema Taifa.


Pia walikamatwa viongozi wa Karatu, Katibu wa Chadema wilaya ya Karatu, Eliya Kibola, Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, Wakili Valerian Qamara, Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Karatu mjini, Joseph Mtui.


Wengine ni Wajumbe wa Kamati Utendaji Wilaya, John Mallelnw na Fabiola Niima ambao wametakiwa kuripoti Ijumaa polisi wilayani Karatu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad