Ushahidi wa Mtoto Ulivyommaliza Baba Aliyemuua Mkewe na Kisu

 

Ushahidi wa Mtoto Ulivyommaliza Baba Aliyemuua Mkewe na Kisu

Ally Balanda ameingia katika orodha ndefu ya wauaji baada ya mahakama kumhukumu adhabu ya kifo kwa kosa la kumuua mkewe, huku ushahidi wa mashahidi wanane, akiwemo mtoto wake wa kambo, ukitumika kumtia hatiani.


Kulingana na ushahidi huo wa upande wa mashtaka, Balanda alichukua uamuzi huo wa kumuua mkewe, Selan Kondo kwa kumchoma kwa kisu kwenye bega la kushoto, baada ya mwanamke huyo kukataa kurudiana na mshtakiwa.


Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga aliyeongezewa Mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya mauaji, ambayo kwa mazingira ya kisheria, husikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania.


New Content Item (1)


Mauaji hayo yalifanyika Mei 6, 2019, katika eneo la Tabata Liwiti, ambapo siku ya tukio saa 12 jioni, Balanda alimchoma kisu Kondo na kusababisha kutoka damu nyingi ambayo iliingia katika mapafu, huku tukio likishuhudiwa na mtoto wa miaka minane.


Katika hukumu hiyo, hakimu Kiswaga alisema upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi wanane na kielelezo kimoja pamoja na nyaraka nane, kuthibitisha shtaka hilo na kulingana na uchambuzi, ushahidi huo ulikuwa ni mzito. Hakimu alisema ushahidi huo unaonyesha mshtakiwa alikuwa na nia ovu ya kufanya mauaji hayo, kwani alijiandaa kwa kubeba kisu kwenye begi lake na alimuita mkewe huyo waliyekuwa wametengana, ili amuombe msamaha.


Uchambuzi wa ushahidi


Akichambua ushahidi huo, Hakimu Kiswaga alisema mshtakiwa na mkewe, Selan Kondo waliishi pamoja kwa muda wa miaka saba maeneo ya Tabata Liwiti, Jijini Dar es Salaam, hadi Februari 2019, walipotengana na Kondo kuhama. Kwa mujibu wa ushahidi huo uliotolewa mahakamani, hakimu Kiswaga alisema baada ya kutengana, Kondo aliondoka na kwenda kupanga sehemu nyingine akiwa na mtoto wake ambaye alikuwa siyo wa mshtakiwa huyo.


Mshtakiwa aliendelea kuwasiliana na mkewe na Mei 6, 2019, walipanga kukutana kwa ajili ya kuzungumza na kumuomba msamaha ili warudiane.


Siku hiyo waliyopanga kuonana saa 12 jioni, mke (Kondo) alimuomba mtoto wake mwenye umri wa miaka minane anayesoma shule ya Tabata Liwiti amsindikize dukani. "Wakiwa njiani, mama na mtoto wake walikutana na mshtakiwa huyo. Baba huyo wa kambo (mshtakiwa) alimtuma mtoto huyo kwenda kununua juisi dukani, huku akisisitiza kuwa anataka kuongea na mama yake," alisema Hakimu.


Mtoto huyo baada ya kupewa maelekezo na baba yake wa kambo, alikwenda kununua juisi na wakati anarudi akiwa mita saba kutoka walipo wazazi wake, alisikia majibishano ya kutoelewana kati yao. Mtoto huyo alidai kuwa alisikia baba wa kambo akimwambia mama yake kuwa anataka warudiane, lakini mama yake alikuwa anakataa.


Baada ya mama yake kukataa na kuanza kutembea, baba yake huyo aliyekuwa nyuma ya mama yake alitoa kisu kutoka katika begi alilokuwa amevaa na kumchoma katika bega la kushoto na kisha kukichomoa na kukitupa chini.


Mtoto huyo alisema kuwa mama yake baada ya kuchomwa kisu aliangua chini na wakaanza kupiga kelele za kuomba msaada huku mshtakiwa akikimbia.


Katika ushahidi wa daktari kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, alibainisha sababu za kifo kuwa ni kutoka damu na nyingine kuingia kwenye mapafu iliyotokana na jeraha


Jeraha hilo lilikuwa sehemu ya bega la kushoto lililotokana na kuchomwa na kitu chenye ncha kali, likiwa na urefu wa sentimita 1.8 kwenda chini.


Hakimu Kiswaga alisema ushahidi wa mtoto na mashahidi wengine ambao ni pamoja na askari Polisi waliokwenda eneo la tukio, unaungwa mkono hivyo Mahakama inamtia hatiani mshtakiwa.


Alisema hiyo ni kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani na upande wa Jamhuri, hakuna shaka mshtakiwa aliua kwa kukusudia kwa kuangalia eneo alipofanya mauaji na silaha aliyokuwa nayo, hivyo Mahakama ilimtia hatiani.


Jamhuri yaomba adhabu kali


Awali, kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Grace Mwanga aliomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hiyo. Alipopewa nafasi ya kujitetea, mshtakiwa kupitia kwa wakili wake, Romani Lamwai aliomba Mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ni kosa lake la kwanza na ana watoto wawili wanaomtegemea.


Hata hivyo, Hakimu Kiswaga alitupilia mbali maombi hayo na kukubaliana na maombi ya upande wa mashtaka na kisha kumhukumu adhabu ya kifo akisema hakuna mafuu ya adhabu inayotolewa kwa kosa la mauaji ya kukusudia.


“Adhabu pekee kwa kosa hilo ni kunyongwa hadi kufa, hivyo mshtakiwa naye anapewa adhabu ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hii.”


Alifafanua kuwa haki ya kukata rufaa ipo wazi iwapo mshtakiwa atakuwa hajaridhika na adhabu hiyo.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad