Kufuatia kusambaa kwa Video iliyowaonesha Watoto wakitoa Burudani kwenye Sherehe wakati wa Usiku na katika Miondoko isiyofaa kwa Umri wao, Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amewatafuta Wazazi wa Watoto hao na kukemea kitendo hicho huku akiwataka Washereheshaji na Jamii kuzingatia Sheria inayokemea Udhalilishaji wa Watoto
Sheria ya Mtoto Namba 21 ya Mwaka 2009 (iliyorekebishwa Mwaka 2019), kifungu cha 158 (1) (c) inazuia kumtumia Mtoto kwenye Maonesho ya Harusi, Mitindo ya Nguo au Maonesho mengine kama hayo wakati wa Usiku.
Adhabu yake ni faini ya Tsh. Laki 5 au kifungo cha Miezi 6 jela au vyote kwa pamoja
Waziri Gwajima amesema;
"Napenda kukumbusha wanajamii kuwa: Ni kosa kisheria kuwatumia hivyo Watoto kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto na 21 ya Mwaka 2009 (iliyorekebishwa Mwaka 2019) na kipande cha sheria hiyo nimeambatisha hapo kwenye bango lenye sehemu ya picha.
1) Naomba tusaidiane nani anawajua wazazi wa watoto hawa? Anitumie SMS kwenye 0765345777 tafadhali.
2. Tutakaa kikao na Chama cha washereheshaji (MCs) tuzungumze kuhusu mchango wao kwenye kulinda maadili ya watoto katika kazi zao kwa mujibu wa sheria ya watoto iliyotajwa hapo juu.
3. Pia, tutakaa kikao na Wadau wengine wote ambao kupitia shughuli zao wanaweza kusababisha kuvunjwa kwa sheria hii.
Hata hivyo, wakati tukiandaa hayo, natanguliza rai kuwa, jamii yote TUWENI MAKINI na KUMLINDA MTOTO. Sheria iko mtandaoni, TUSOMENI na TUZINGATIE vinginevyo kuna sehemu ya jamii itakutana na changamoto endapo Sheria itatekelezwa kikamilifu."