Waziri Mkuu Majaliwa Ampa Wiki Moja Dk Biteko Sakata la Mafuta

 

Waziri Mkuu Majaliwa Ampa Wiki Moja Dk Biteko Sakata la Mafuta


Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Naibu Waziri Mkuu, Dk Dotto Biteko kukaa na wadau wa mafuta ili washughulikie changamoto ya upatikanaji ndani ya siku saba.


Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Septemba 7, 2023 alipokuwa anajibu maswali ya papo kwa hapo kutoka kwa wabunge katika kipindi cha asubuhi.


Katika swali la msingi, Mbunge wa Lushoto (CCM) Rashid Shangazi alitaka kujua Serikali inaweka mkakati gani kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unakuwa ni mzuri nchini.


Mbunge huyo amesema kumekuwa na sintofahamu kuhusu suala la mafuta kwani licha ya bei zinazopanda kila wakati lakini mafuta hayo huwa hayapatikani kila inapofika jumatano ya kwanza ya mwezi ambayo ni siku ya kutangaza bei mpya ya bidhaa hiyo.


“Nikiri tunayochangamoto ya mafuta nchini, lakini zipo jitihada mbalimbali ambazo zinachukuliwa na Serikali kuondokana na tatizo hilo kwani nishati hiyo ndiyo injini ya uchumi,” amesema Majaliwa.


Waziri Mkuu amesema tayari Rais alishamteua Naibu Waziri Mkuu ambaye ni Waziri wa Nishati pia ambaye ameanza kushughulikia jambo hilo kwa kukaa na wadau mbalimbali.


“Niendelee kumuagiza Naibu Waziri Mkuu aendelee kushughulikia hili ndani ya wiki moja tuwe na majibu na katika hilo wapanue wigo kwa waagiza mafuta ili tuwe na mafuta ya kutosha na suala la bei tutaangalia huko mbeleni,” amesema Majaliwa.


Mjadala huo umeibuka ikiwa ni siku moja tu tangu Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya za mafuta zitakazotumika Septemba ambazo zimepaa ikilinganishwa na Agosti.


Katika taarifa kwa umma iliyotolewa jana Jumanne Septemba 5, 2023 saa 4 usiku na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Dk James Mwainyakule imeonesha kuwa kuanzia Jumatano Septemba 6 jijini Dar es Salaam petroli itauzwa Sh3,213 na dizeli itauzwa kwa Sh3,259.


Bei hizo zinamaanisha kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam petroli imeongezeka kwa Sh14 kutoka Sh3,199 ya Agosti huku dizeli ikiongezeka zaidi kwa Sh324.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad