Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amesema kuwa Yanga itamlipa kwa awamu aliyekuwa kiungo wao Gael Bigirimana raia wa Burundi.
Kulikuwa na mvutano kati ya uongozi wa Yanga na mchezaji huyo juu ya malipo aliyokuwa akihitaji ili kuvunja mkataba wake wa mwaka mmoja uliokuwa umebaki hivyo kupelekea pande hizo kupelekana FIFA kwa ajili ya kupata suluhisho.
FIFA ikatoa maamuzi ya kuitaka Yanga imlipe Bigirimana kiasi cha fedha walichokuwa wamekubaliana na kwa kuwa Yanga ilichelewa kukamilisha malipo ya awamu ya kwanza ambayo walipaswa kulipa ndani ya siku 45 tangu hukumu ilipotolewa, juzi TFF wakatoa taarifa kuwa Yanga imefungiwa na FIFA kusajili hadi hapo watakapomlipa mchezaji huyo.
Kamwe amethibitisha kuwa mchakato wa malipo ya Bigirimana unaendelea huku akiwatoa hofu Wanachama na Mashabiki wa Yanga kuwa jambo hilo litamalizwa hivi karibuni.
Dirisha la usajili linafungwa usiku wa juzi, ahueni kwa Yanga ni kuwa hukumu hiyo imetolewa wakati wakiwa tayari wamekamilisha michakato ya usajili katika dirisha hili.
Ili Yanga iweze kusajili wachezaji katika madirisha yajayo ni lazima ikamilishe malipo ya Bigirimana ambaye usajili wake ni kama Umesababisha hasara tu kwani hakufikia hata nusu ya kile ambacho wengi walitarajia kutoka kwake hasa ikizingatiwa ni mchezaji aliyewahi kucheza ligi kuu ya Uingereza.