Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahemd Ally amesema kuwa mashabiki wa klabu hiyo wanatakiwa kutembea vifua mbele kwani timu yao ni miongoni mwa timu Bora Barani Afrika ndiyo maana imekuwa miongoni mwa timu 8 pekee Afrika nzima ambazo zitashiriki mashindano ya African Football League.
Ahmed amesema hayo kuelekea mchezo wa ufunguzi wa michuano hiyo utakaofanyika Ijumaa ijayo Oktoba 20, 2023 katika Dimba la Mkapa kati ya Simba SC na Al Ahly ya Misri.
"Kuna jambo kubwa Afrika hii ambalo ni AFL linaihusisha Simba na Al Ahly. Ni heshima kubwa Simba tumepewa kuandaa mechi ya ufunguzi wa mashindano haya kwa mara ya kwanza.
"Wengine wataishi maisha ya shida sana wiki hii, na sisi sio shida zetu tutazidisha dozi.
"Tumepewa wenyeji wa michuano hii sababu ya ubora ambao tupo nao, zipo timu nyingi Tanzania, zipo timu nyingi Afrika lakini walikaa kujadili timu gani inafaa wakaona Simba Sports Club.
"Hatujapata nafasi hii kwa bahati mbaya, tumepata kwa ubora tulionao. Kama sio Simba kuwepo Tanzania basi Tanzania kusingekuwa na timu inayoshiriki African Football League kwa sababu baada ya Simba hakuna mwingine mwenye mafanikio kimataifa zaidi yetu.
"Ukweli unabaki kuwa sisi Wenye Nchi ndio tumeleta AFL hapa. Wanasimba mna nafasi kubwa ya kujipongeza, kufurahi sababu tumekomboa nchi kupata nafasi ya michuano hii, na kwenda mbali zaidi ya kuwa mwenyeji wa michuano," amesema Ahmed Ally.