Viongozi sita wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya Kata wakiwemo Viongozi watatu wa UWT kutoka Kata mbalimbali za Wilaya ya Makete Mkoani Njombe wamefariki kwa ajali ya gari wakati wakitoka kwenye mkutano wa Mlezi wa Chama hicho Mkoa wa Njombe Halima Mohamed Mamuya uliokuwa ukifanyika Wilayani humo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe John Makuri Imori amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo katika ajali ya gari iliyotokea Kijiji cha Ndulamo “Gari Namba T 733 BBP aina ya Toyota Hiece likiwa linatokea Makete kuelekea Tandala likiwa na abiria 18 lilipata ajali kwenye kona likapinduka na kuanguka na baada ya ajali kutokea Watu 6 wamefariki (Watatu Wanaume na watatu ni Wanawake), chanzo cha ajali ni mwendokasi na Dereva akashindwa kulimudu gari hilo na kulikuwa na mteremko"
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe Juma Mfanga amesema majeruhi wengi wamevunjika viungo na wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Ikonda na wengine wakiendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Makete ambapo pia tayari Madaktari wengine kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe wamefika katika Hospitali hizo kuongeza nguvu.
Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM Halima Mamuya ambaye pia ni Mlezi wa CCM Njombe ametoa pole kwa Familia na majeruhi ambapo amesema ajali hiyo imekuwa ni pigo kwake huku akiishukuru Serikali kwa hatua za haraka zinazochukuliwa kwa ajili ya matibabu “Waliofariki ni Viongozi wa Chama wawili, Kiongozi wa Jumuiya ya Wazazi mmoja na Viongozi wa Jumuiya ya Wanawake watatu”