Ambangile Afunguka "Jamani Aucho wa Yanga Apewe Maua yake"
Mchambuzi wa masuala ya soka nchini kupitia Wasafi Media, George Ambangile amempa maua yake kiungo wa Yanga SC, Khalid Aucho kutokana na uwezo wake mkubwa wa kimiki Dimba na kuamua timu yake ichezeje.
Aucho ambaye ni raia wa Uganda amekuwa mhimili mkubwa katika kuilinda timu yake isishambuliwe na hata wakati wa kutengeneza mashambulizi kwenda kwa mpinzani wake.
Ambangile amesema hayo mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa ligi kati ya Geita Gold na Yanga ambapo Wananchi waliibuka na ushindi wa bao 3-0, manao yakifungwa na Pacome Zouzoua Aziz Ki na Maxi Nzengeli.
Ameandika George Ambangile; "Unajua katika timu yoyote ile Duniani, kila mchezaji ana umuhimu wake, maana timu haijengwi na mchezaji bali muunganiko wa wachezaji wengi (wengi wanapenda wachezaji wazuri, nani hapendi?)
"Lakini ukweli ni kwamba kila timu ina yule mchezaji / wale wachezaji ambao wanaitwa "Key Players" wale ambao ndio wanakuwa uti wa mgongo."
"Ndani ya Yanga SC, mtazamo wa George Ambangile unaamini huyu kiungo Khalid Aucho ndio anahitimisha nini maana ya Yanga, taswira nzima ya Yanga, jinsi wanavyocheza, kama ni ujenzi basi tunasema Aucho ni MSINGI wa Nyumba.
"Kuna wachezaji huwa wanacheza namba 6, baadhi yao huwa wanazuia tu lakini Mganda huyu anafanya vitu vingi sana.
1: Anazuia 2: Anaunganisha safu ya ulinzi na kiungo 3: Mpigaji pasi mzuri za kuelekeza 4: Uwezo wa ku control mechi (kasi ya mchezaji) 5: Haiba ya kukubali kusimama na kuhesabiwa pale timu inapomuhitaji 6: Ongeza hapo na Uongozi wake uwanjani. 7: Anawapa uhuru wa kiakili fullbacks na viungo wake washambuliaji kufikiria mbele tu.
"Nafikiri ukimuuliza mwana Yanga akuambie kuhusu Yanga yenye Aucho na Yanga ambayo haina Aucho utajua maana ya huyo kiungo umuhimu wake.
"Angalia siku akikosekana au akiwa na mechi mbaya, kuna siku zipo huwa anazidiwa angalia timu yake pia inavyokuwa.
"Siku ambazo anakosekana au anazidiwa hapo sasa ndio kazi ya Gamondi na benchi lake la ufundi wanafanyaje. Geita Gold wanayo majibu yake," amesema George Ambangile.