Zomea zomea ya mashabiki katika Uwanja wa Azam Complex imeifanya klabu hiyo kusitisha kuingia bure katika michezo yao.
Tangu Ligi Kuu imeanza mashabiki walikuwa wakipewa ofa ya kuingia uwanjani bure ili kuisapoti timu hiyo, lakini mambo hayakuwa hivyo na ndipo mabosi wakaamua kuondoa utaratibu huo.
Kuanzia mchezo wa juzi dhidi ya Namungo ambao wenyeji Azam FC walilala kwa mabao 3-1, mashabiki walioingia walilipia kiingilio cha chini cha Sh3,000.
Habari ambazo Mwanaspoti lilipenyezewa ni kwamba uongozi haukufurahishwa na tabia ambayo ilionekana kuwatoa mchezoni wachezaji wanaopambana mwanzo hadi mwisho kupata matokeo badala ya kuwasapoti. “Sasa hivi hakuna tena huo utaratibu mtu unaingia bure halafu unamzomea aliyekufanya uingie bure. Siyo poa hata kidogo tukaona isiwe shida ingia kwa kiingilio chako uzomee vizuri,” kilisema chanzo chetu.
Kilisema baada ya kuona hivyo awali uongozi ulivumilia, lakini subira zimeshindwa kuleta matunda na ndio maana wakaamua kufanya uamuzi wa kuondoa ofa.
Mwanaspoti lilimtafuta Mkuu wa Idara ya Habari ya klabu hiyo, Zakaria Thabit ‘Zaka Zakazi’ ambaye alikiri kuwepo kwa sintofahamu hiyo ya mashabiki kuzomea timu yao na ndio maana wameondoa utaratibu huo.
“Ni kweli hizo habari ni sahihi kabisa. Walikuwa wanaizomea timu tukaona tuondoe ofa hiyo na sasa ni mwendo wa kulipa tu ili uingie uwanjani. Nafikiri umenielewa,” alisema.