Mwanamuziki mashuhuri wa Kenya Kelvin Kioko almaarufu Bahati amekashifu wanamtandao waliomkejeli kwa kuandamana na mke wake Diana Marua hadi kwenye chumba cha urembo kwa kunyolewa na kusafishwa sehemu za siri na kurekodi matukio.
Akizungumza katika kikao cha hivi majuzi na waandishi wa habari, mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili alihoji ni kwa nini watu wana shida na mambo anayofanya na mkewe.
Alibainisha kuwa Diana Marua ni mke wake halali na wana haki ya kufanya wanachotaka kufanya kama wanandoa.
“Kwani mnataka hadi vitu nafanya na bibi yangu ziwafurahishe? Si ni bibi yangu,” Bahati alisema.
Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 30 pia alibainisha kuwa wanaume wengine pia hufanya mambo sawa na wake zao ingawa hawashiriki kwenye mitandao ya kijamii.
"Tofauti kati yangu na wewe ni kwamba hujaweka picha mitandaoni lakini ndivyo unavyofanya.. sijui kwa nini mtu akiangalia bibi yake akitengenezwa ni shida na mimi nimeset camera," alisema.
Bahati alisema aliandamana na mke wake kwenye chumba hicho cha urembo akiwa na shauku kubwa ya kutaka kujua ‘wax’ ni nini na inafanywaje. Pia alifichua kuwa alitaka mkewe awe sawa kabla hajampa zawadi.
“Mke wangu alitaka kwenda. Sikuwa najua hiyo waxing ni nini. Nikasema wacha nikaone, hivyo tu,. Nilitaka nikienda kumpea zawadi akuwe ako tu sawa,” Bahati alisema.
Mapema wiki iliyopita, mwanamuziki huyo na mkewe Diana Marua walijipata kwenye upande wa kushambuliwa katika mitandao ya kijamii baada ya kupakia mwanzo wa mwendelezo wao wa kile walichokiita tafrija ya kusherehekea miaka 7 kwenye uhusiano.
Katika mwendelezo huu, Bahati alidai kwamba angempa mkewe zawadi saba kuadhimisha miaka saba ya kuwa pamoja na kumzalia watoto watatu.
Lakini zawadi yake ya kwanza kwa Diana Marua iliwazuzua mashabiki mitandaoni.
Bahati aliongozana na Diana Marua hadi kwenye spa moja ambapo picha na video zilirekodiwa akishuhudia mke huyo wake akifanyiwa usafi kwenye sehemu zake za siri.
Picha hizo zilisambaa mitandaoni baadhi wakiuliza maswali kuhusu maadili ya wanandoa hao kwa wanao wanaokua na pengine kuja kushuhudia kile ambacho wazazi wao walikuwa wanakifanya kwa ajili ya kupata umaarufu na kuzungumziwa mitandaoni.