Bei ya Mafuta Kupanda Zaidi Mwezi Huu Oktoba


 

Serikali imesema kuna viashiria vya kupanda kwa bei za mafuta katika bei zitakazotangazwa mwezi Oktoba, 2023 sababu zikiwa ni zilezile zilizoelezwa mwezi uliopita.


Kwa mwezi Septemba bei ya Petroli iliongezeka kwa Sh14 kwa lita moja huku dizeli ikiongezeka kwa Sh324 jambo lilioibua minong’ono miongoni mwa wananchi hususani watumiaji wa vyombo vya moto huku wachumi wakitahadharisha ongezeko la gharama za maisha.


Uwezekano huo ulidokezwa leo Jumamosi Septemba 30, 2023 na Msemaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Titus Kaguo ambaye amesema hakuna namna ya kukwepa ongezeko la bei mafuta kwani hata katika soko la dunia hali bado si nzuri.


Kaguo ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu EWURA kuvifungia vituo vya mafuta ambavyo vilionekana kukiuka sheria za manunuzi hata walipoelekezwa lakini walishindwa kufanya inavyotakiwa.


Akizungumza sababu za bei ya bidhaa hiyo muhimu kuendelea kupaa amesema mtikisiko bado ni mkubwa kwani wazalishaji wa mafuta bado wamepunguza kiwango cha kuzalisha.


“Kingine ni kuhusu meli za kusafirisha, ujue Urusi inazo meli zaidi ya 300 zinazosafirisha mafuta kati ya meli 1000 zinazofanya kazi hiyo duniani, kwa hiyo vita ya Urusi na Ukraine nalo ni tatizo lingine ambalo linapelekea bei ziendelee kuwa juu,” amesema Kaguo.


Msemaji huo alibainisha kuwa hivi sasa gharama za kusafirisha mafuta zimeongezeka kwa asilimia 62 jambo ambalo si la kawaida kwa hiyo, wiki ijayo wanapokwenda kutangaza bei mpya za mafuta wanaamini kuwepo na ongezeko.


Kutokana na uwezekano wa bei ya mafuta kupaa tena Oktoba, Chama cha wamiliki wa mabasi (Taboa) wako kwenye mchakato wa kuomba kuongezwa kwa nauli katika mabasi yao kwa madai bila kufanya hivyo wanakwenda kufunga biashara zao.


Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania, Mustafa Mwalongo amesema leo kuwa wameshaandaa andiko lao kwa ajili ya kuomba kuongezewa nauli kwani wameona biashara inakuwa ngumu na wanapata hasara.


Mwalongo amesema jukumu la mwisho katika gharama zote anayebebeshwa ni mlaji hivyo kinachofanyika ni maumivu ya mwisho kwa mtu ambaye anatajwa kuwa ni wa mwisho.


“Ni kweli wanaokwenda kuumia ni wananchi wa kawaida, kama Serikali haitakuwa na cha kufanya lazima wananchi wataumia zaidi, sisi tunatoa huduma na tukishindwa kutoa huduma nako inakuwa ni tatizo lingine ambao sasa litakuwa kubwa zaidi,” amesema Mwalongo.


Kuhusu bei ya nauli amesema hata kabla ya kupandishwa kwa gharama hizo tayari walishaanza kufikiria kupandisha bei hizo kwani hata bei ya mafuta ya sasa bado ina tatizo.


Akizungumza kuhusu bei hiyo, muuzaji wa mafuta katika kituo cha Oilcom Jijini Dodoma, Nuren Kareem amesema kupandishwa kwa bei ya mafuta kwao hakuna athari kubwa kwani kila wanapoongeza bei nao wanaongeza.


Nuren amesema anayeumia zaidi katika biashara hiyo ni mwananchi wa kawaida lakini kwa namna ilivyo akasema hakuna jinsi ni lazima kila jambo liende.


Hata hivyo amesema kwa sera ya Tanzania wanaona bado mambo hayajawa ya moto ukilinganisha na zingine zinazozunguka kwani wao wanakuwa na maumivu makali kutokana na sera zao kutokuwa nzuri katika kuwasaidia wananchi wa kawaida.


Vituo kufungiwa


Kaguo alizungumzia hatua ya kuvifungia baadhi ya vituo vya mafuta kufanya biashara hiyo, akisema hadi kufikia juzi mamlaka hiyo ilikuwa imevisimamisha kufanya biashara ya mafuta vituo saba kutokana na kukiuka sheria wanayotakiwa kuifuata.


Kati ya vituo hivyo, vinne vinatoka katika mkoa wa Morogoro na alieleza kosa kubwa kwamba linatokana na vitendo vyao vya kuficha mafuta jambo ambalo linakiuka sheria walizopewa kama sehemu ya mkataba wao.


Amesema hatua ya kuvifungia vituo hivyo ilianza mwisho wa Julai na mwanzoni mwa Agosti kutokana na kubaini baadhi ya vituo kuficha mafuta hasa wanapoona kuwa kuna muda bei inakuja kupanda.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad