Ukanda wa Gaza ni eneo la urefu wa kilomita 41- (maili 25) na upana wa kilomita 10 kati ya Israeli, Misri na Bahari ya Mediterania.
Ni nyumbani kwa wakazi wapatao milioni 2.3 na lina mojawapo ya msongamano mkubwa zaidi wa watu duniani.
Israel inadhibiti anga juu ya Gaza na ufuo wake wa bahari na imeweka vikwazo vya ni nani na bidhaa gani zinazoruhusiwa kuingia na kutoka kupitia vivuko vya mpaka wake.
Vile vile, Misri inadhibiti wanaopita na kutoka katika mpaka wake na Gaza.
Takriban 80% ya wakazi wa Gaza wanategemea misaada ya kimataifa, kulingana na Umoja wa Mataifa, na takriban watu milioni moja wanategemea chakula cha kila siku.
Kwa nini Israel na Hamas wanapigana?
Kuna mvutano wa mara kwa mara kati ya Israel na Hamas, lakini mashambulizi ya wanamgambo hao siku ya Jumamosi yaliwashangaza wengi
Hamas ilirusha maelfu ya roketi dhidi ya Israel huku makumi ya wapiganaji wakivuka mpaka na kuvamia jamii za Israel, na kuua makumi ya raia huku wengine wakichukuliwa mateka.
Israel ilianzisha mashambulizi ya angani mara moja, ikisema kuwa inalenga maeneo ya wanamgambo huko Gaza.
Je, shambulio hili halina kifani?
Kama Mhariri wetu wa Kimataifa Jeremy Bowen anavyoandika, hii ndiyo operesheni kabambe zaidi ambayo Hamas imewahi kuzindua kutoka Gaza na shambulio baya zaidi la kuvuka mpaka ambalo Israel imekabiliana nalo katika zaidi ya kizazi kimoja.
Wanamgambo walivuka waya unaotenganisha Gaza na Israel katika maeneo mengi.
Shambulio hilo ambalo halijawahi kutokea limekuja siku moja baada ya kumbukumbu ya miaka 50 ya shambulio la kushtukiza la Misri na Syria mnamo 1973 ambalo lilianzisha vita vikuu vya Mashariki ya Kati.
Umuhimu wa tarehe hiyo hautasahaulika kwa uongozi wa Hamas.
Je, Ujasusi wa Israel ulizembea?
Ndiyo, anasema mwandishi wetu wa usalama Frank Gardner.
Kwa juhudi za pamoja za Shin Bet, ujasusi wa ndani wa Israeli, Mossad, wakala wake wa kijasusi wa nje na mali zote za Jeshi la Ulinzi la Israeli, anasema inashangaza ukweli kwamba hakuna mtu aliyeona hili linakuja au alishindwa kulifanyia kazi
Israel ina huduma nyingi za kijasusi zinazofadhiliwa zaidi katika Mashariki ya Kati, ikiwa na watoa habari na maajenti ndani ya makundi ya wapiganaji wa Palestina, pamoja na Lebanon, Syria na kwingineko.
Chini, kando ya uzio wa mpaka kati ya Gaza na Israel kuna kamera, vitambuzi vya mwendo wa ardhini na doria za kawaida za jeshi.
Uzio wa juu wa waya unafaa kuwa "kizuizi mahiri" ili kuzuia kitu chochote kupenya .
Hata hivyo wapiganaji wa Hamas walijibanza tu kupitia humo, wakakata mashimo kwenye waya huku wengine wakiingia Israeli kutoka baharini na kupitia angani.
Palestina ni nini na matukio haya yana uhusiano gani nayo?
Ukingo wa Magharibi na Gaza, ambayo yanajulikana kama maeneo ya Palestina, pamoja na Jerusalem Mashariki na Israel zote ziliunda sehemu ya ardhi inayojulikana kama Palestina .
Maeneo haya yalikuwa himaya ya nchi za falme za Kiyahudi katika Biblia, na zinaonekana na Wayahudi kama nchi yao ya kale.
Israel ilitangazwa kuwa taifa mwaka 1948, ingawa ardhi hiyo bado inajulikana kama Palestina na wale ambao hawatambui haki ya Israel ya kuwepo.
Wapalestina pia hutumia jina la Palestina kama neno mwavuli la Ukingo wa Magharibi, Gaza na Jerusalem Mashariki.
Nini kinaweza kutokea baadaye?
Kamanda wa wanamgambo wa Hamas Mohammed Deif ametoa wito kwa Wapalestina na Waarabu wengine kujiunga na operesheni ya wanamgambo hao ili "kuangamiza uvamizi wa [Israeli]".
Swali kubwa sasa ni iwapo Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki inayokaliwa kwa mabavu au kwingineko katika eneo hilo watatii wito wake, anasema mwandishi wetu wa Jerusalem Yolande Knell.
Israel bila shaka inaona uwezekano wa vita ambavyo vinaweza kufunguka kwa pande nyingi.
Hali mbaya zaidi ni kwamba vita hivyo vinaweza kulivutia kundi lenye nguvu la wanamgambo wa Lebanon, Hezbollah.
Jeshi la Israel limeamuru kuimarishwa kwa kiasi kikubwa cha wanajeshi. Pamoja na mashambulizi yake makali ya anga dhidi ya Gaza, ilmedokeza kuwa linapanga kufanya operesheni ya ardhini.