Hii Hapa Mikoa Wanawake Wake Vinara Magonjwa ya zinaa




Dar es Salaam. Kushamiri kwa ngono zembe miongoni mwa watu nchini kunatajwa kusababisha kuongezeka kwa idadi ya magonjwa ya ngono, hasa kwa wanawake.

Takwimu za Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi, Mtoto na Viashiria vya Malaria nchini ya mwaka 2022 (TDHS-MIS 2022) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya zinaonyesha asilimia 14 ya wanawake wana magonjwa yanayoambukizwa kwa ngono, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia saba mwaka 2010.

Pia, wanaume nao maambikizi hayo yameongezeka kutoka asilimia sita mwaka 2010 hadi asilimia 13 mwaka 2022.

Kwa jumla, takwimu hizi ni sawa na mtu mmoja kati ya 10 nchini ana maambukizi ya magonjwa ya ngono.


Ripoti hiyo iliyozinduliwa jana na Rais Samia Suluhu Hassan ilihusisha uchunguzi wa kaya 16,354, washiriki wakuu walikuwa watu wenye rika la miaka 15 hadi 49.

Mikoa vinara

Wakati maambukizi ya magonjwa hayo yakiongezeka kwa asilimia saba kwa wanawake na asilimia saba nyingine kwa wanaume mwaka 2022 ikilinganishwa na mwaka 2010, Mkoa wa Katavi unatajwa kuwa kinara, hususan kwa wanawake wenye tatizo hilo kwa asilimia 11.4.

Rukwa inafuatia kuwa na wanawake wenye maambukizi hayo kwa asilimia 11, huku Shinyanga ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na maambukizi asilimia 9.6.


Kilimanjaro unafuatia kwa kuwa na asilimia 9.5 na Dar es Salaam inafunga orodha hiyo kwa kuwa na maambukizi ya asilimia 9.1.

Takwimu hizo zinaonyesha katika mikoa hiyo mitano mwanamke mmoja kati ya 10 ana maambukizi ya magonjwa ya ngono yanayotajwa kuwa miongoni mwa viashiria vya Virusi Vya Ukimwi.

Uhusiano na ndoa

Ripoti hiyo ya TDHS-MIS 2022 inaonyesha watu waliotalikiana au kutengana wanaongoza kwa maambukizi ya magonjwa hayo kwa asilimia 11, wakifuatiwa na walioko kwenye ndoa kwa asilimia saba.

Wasioolewa na ambao hawajawahi kukaa pamoja na mwenza, wana ahueni ya maambukizi kwa wastani wa asilimia 6.7.


Ripoti inaonyesha wakazi wa mijini wanaongoza kukutwa na dalili au maambukizi ya maradhi hayo kwa asilimia 6.2, wakifuatiwa na wakazi wa vijijini ambao asilimia tano pekee hupata changamoto hiyo.

Maoni ya wananchi

Daktari wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Dodoma, Zainab Abdallah alisema sababu kubwa ya mtu kuambukizwa magonjwa ya zinaa ni kutotumia kondomu wakati wa kujamiiana.

“Lakini tabia hatarishi pia zimeongezeka, hasa maeneo ya mijini ambapo watu wakienda baa wakilewa wanashiriki tendo hilo (kujamiiana) bila tahadhari wala kufahamiana,” alisema.

Mwajuma Buremo, mkazi wa Mabibo jijini Dar es Salaam, alisema ongezeko hilo linasababishwa na mtindo wa maisha ambao watu wengi wanaogopa Ukimwi kuliko magonjwa ya zinaa.

“Sasa hivi vijana wengi wanaogopa Ukimwi kuliko hata hayo magonjwa, ndiyo maana unakuta wengi wanajipima Ukimwi na wenza wao (kwa kutumia Rapid test) na hawavai kondomu, kwa hiyo anajikinga Ukimwi lakini anapata magonjwa hayo,” alisema.

Msimamo wa Serikali

Wiki moja iliyopita katika mahojiano maalumu na gazetil hili, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya, Profesa Paschal Rugajjo alisema idadi ya waliopimwa na kubainika kuwa na kaswende ilipanda kutoka 16,015 mwaka 2017 hadi 26,592 mwaka 2019.

“Bado uelewa ni mdogo kwa jamii juu ya magonjwa ya zinaa na vijana wapo katika hatari kubwa kuambukizwa,” alisema.

Profesa Rugajjo alisema jitihada za makusudi zitaendelea kuchukuliwa na kusisitiza kuhusu ngono salama, yakiwamo matumizi ya kondomu ili kujikinga na maradhi hayo, mimba zisizotarajiwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad