BAADA ya uvumi kuwa Yanga Princess iliyopo Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), imesajili nyota Mmarekani, Kaeda Wilson kutoka 7 Elite Academy, baba mzazi wa kiungo mshambuliaji huyo anayetumia miguu yote miwili kwa ufasaha, ambaye ndiye msimamizi wake amefunguka akisema kuwa bado yupo.
Akizungumza na Mwanaspoti Web, baba wa mchezaji huyo, Reggie Wilson amesema mchezaji anafanya mazoezi na Yanga kwa muda, kwani aliamua kuchagua timu hiyo kulingana na ubora wao.
Wilson amesema Kaeda anaipenda timu hiyo na kama Yanga watamuona anafaa basi anaweza kujiunga nao muda wowote na kufichua mtu wa kwanza kumuunganisha na timu hiyo ni nyota wa zamani wa Simba na Yanga aliyewahi kung'ara na Taifa Stars, Amri Kiemba na pamoja na ndugu yake anayeishi hapa nchini.
"Mama yake mzazi ni kocha wa timu za vijana na aliwahi kufanya mazoezi na Simba Queens 2020, sisi tunaishi Marekani jiji la U.H.A.T tumekuja mara moja naye anasoma kidato cha sita, hivyo nikaona nimtafutie timu ya kuendelea kucheza ndipo Kiemba akatuunganisha na Yanga," amesema Wilson.
Kwa upande wa Kaeda amesema anafurahi kukutana na Yanga kwa sababu ni timu kubwa na anaamini siku moja atajiunga nao.
Kaeda ni kiungo mshambuliaji akiwa na uwezo wa kutumia miguu yote na ni mzuri pia kupiga mashuti ya mbali kama ilivyo kwa Stephane Aziz Ki anayekipiga Yanga.